Na Jovina Bujulu-
Maelezo
SERIKALI kupitia
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM)
na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES)
imeendelea kuboresha na kurekebisha miundo mbinu katika shule za msingi
na sekondari nchini ili kufikia azma ya kutoa elimu bora kwa Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa
na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.
George Simbachawene alipokuwa akizungumzia mikakati ya Serikali katika
kuboresha miundo mbinu ya shule za msingi na sekondari.
“Kupitia programu za
MMEM na MMES, Serikali inaendelea kujenga, kukarabati, na kuimarisha miundo
mbinu katika shule zake hapa nchini kwa manufaa ya watoto wetu na taifa kwa
ujumla” alisema Simbachawene.
Simbachawene alisema
kuwa changamoto kubwa zipo katika shule za msingi hali inayotokanana na sera ya
elimu bure ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi
wanaojiunga na shule za msingi. Ongezeko hilo linapelekea miundombinu mingi
kupungua ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi.
Changamoto hizo ni
pamoja na upungufu wa madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu.
Katika kulipatia
ufumbuzi suala hilo, Simbachawene alitaja baadhi ya Mikakati kuwa ni kuimarisha
miundombinu na kuziagiza Halmashauri zote nchini kuongeza bajeti ya elimu
katika bajeti ya mwaka jana 2016/17.
“Halmashauri
zilielekezwa kutoa kipaumbele katika miundombinu ya shule ili kuwa na mazingira
rafiki kwa walimu na wanafunzi kwa kufundishia na kujufunzia ambayo yatapelekea
ufaulu mzuri” Aliongeza Simbachawene.
Aidha, kuhusu ukosefu
wa matundu ya vyoo, Simbachawene alisema suala hilo kwa sasa halipo kwa sababu
sera ya elimu inasema kuwa shule isiyokuwa na vyoo ni lazima ifungwe, na alitoa
agizo katika kikao alichofanya hivi karibuni na wataalamu kuwa kila shule
inapojengwa ni lazima iwe na vyoo venye hadhi na nyumba za walimu ambazo
angalau zina samani muhimu.
No comments:
Post a Comment