TANGAZO


Monday, March 13, 2017

Carlos the Jackal kushtakiwa tena Ufaransa


Carlos the Jackal (file pic Dec 2013)Haki miliki ya pichaAFP
Image captionRamirez alikuwa anatetea haki za Wapalestina na wakomunisti

Carlos the Jackal, gaidi kutoka Venezuela, anayedaiwa kuhusika katika mashambulio kadha Ufaransa miaka ya 1970 na 80, atashtakiwa tena kuhusiana na shambulio lililotekelezwa katika duka moja.
Tayari anatumikia vifungo viwili vya maisha jela kwa kutekeleza visa kadha vya mauaji, akidai alikuwa anatetea haki za Wapalestina na wakomunisti.
Carlos, ambaye jina lake kamili ni Ilich Ramirez Sanchez, alipewa jina hilo alipokuwa mmoja wa magaidi waliotafutwa sana duniani.
Alikaa miaka kadha akiwa mtoro kabla ya kukamatwa mwaka 1994 nchini Sudan.
Anashtakiwa nini?
Ramirez, 67, atafikishwa mbele ya majaji watatu mahakamani Paris Jumatatu kuhusiana na shambulio la guruneti lililotekelezwa katika jumba moja la kibiashara mtaa wa Latin Quarter mjini Paris Septemba 1974.
Watu wawili waliuawa na wengine 34 wakajeruhiwa wakati wa shambulio hilo.
Ramirez amekanusha mashtaka hayo na wakili wake, Isabelle Coutant-Peyre, amesema kesi hiyo ni kupoteza wakati wa pesa bure.

Ilich Ramirez SanchezHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionNi mara ya tatu kwa Ramirez kushtakiwa Ufaransa

"Kuna maana gani kumfikisha kortini muda mrefu hivyo baada ya matukio kutekelezwa?" alishangaa.
Lakini Georges Holleaux, wakili wa waathiriwa, amesema jamaa za waathiriwa wanasubiri sana na wangefurahia kumuona akiwa kizimbani.
"Waathiriwa wamesubiri sana kumuona Ramirez akishtakiwa na kuhukumiwa. Vidonda vyao havijawahi kupona," amesema.
Katika mahojiano na gazeti moja, Ramirez anadaiwa kusema alitekeleza shambulio hilo kuishurutisha Ufaransa kumwachilia huru mwanaharakati wa kikomunisti kutoka Japan.
Carlos the Jackal ni nani hasa?
Ramirez alipewa jina la utani Carlos the Jackal na wanahabari, kutokana na mhusika gaidi katika riwaya ya 1971 iliyoandikwa na Frederick Forsyth kwa jina The Day of the Jackal.
Riwaya hiyo baadaye iligeuzwa na kuwa filamu ambayo ilivuma sana.
Alizaliwa Venezuela, na alichukuliwa kuwa mmoja wa magaidi hatari zaidi wa kisiasa miaka ya 1970 na 80.
Akiwa na miaka 24, alijiunga na kundi la Popular Front for the Liberation of Palestine (PFLP) na akaanza kupokea mafunzo kama mwanamgambo mwanamapinduzi.
Miaka michache baadaye, alitekeleza shambulio lake la kwanza dhidi ya Joseph Edward Sieff, aliyekuwa rais wa maduka maarufu ya Marks and Spencers jijini London.
Sieff, Myahudi maarufu, alinusurika jeraha la risasi kichwani.

Ilich Ramirez Sanchez in dated pictureHaki miliki ya pichaEPA
Image captionRamirez alikuwa mhusika mkuu katika kundi la Popular Front for the Liberation of Palestine

Alipatikana na makosa ya kutekeleza mashambulio manne ya mabomu Paris na Marseille mwaka 1982 na 1983, yaliyoua watu 11 na kujeruhi wengine 150.
Alipatikana na hatia mara ya kwanza kortini Ufaransa mwaka 2011 na tena 2013.
Akipatikana na makosa ya mauaji, basi huenda akahukumiwa kifungo cha tatu cha maisha jela.
Ramirez alikamatwa mjini Khartoum na maafisa wa usalama wa Ufaransa mwaka 1994, miaka 20 baada yake kutekeleza shambulio lake la kwanza.

No comments:

Post a Comment