TANGAZO


Tuesday, March 7, 2017

BILIONI 568 KUNUFAISHA WABUNIFU SEKTA YA AFYA

Kutoka kulia ni Mtendaji Mkuu wa Atamizi ya DTBi yenye lengo la kuleta mapinduzi katika Sekta ya Afya, Mhandisi George Mulamula, Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda, Mratibu wa Kikanda wa MCC/PEPFAR Bwana Mitch Blasser pamoja na Meneja Mkuu wa Mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI), Agapiti Manday wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mradi huo.Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda, akikabidhi Hundi ya millioni 568 kwa wajasiriamali wavumbuzi 12 waliovumbua miradi mbalimbali ya kuiendeleza Sekta ya Afya chini ya mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI) unaofadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya marekani ya Changamoto za Millenia (MCC).Wajasiriamali vijana 12 waliovumbua miradi mbalimbali ya kuiendeleza Sekta ya Afya chini ya mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI) unaofadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya marekani ya Changamoto za Millenia (MCC) wakiwa katika picha ya pamoja na hundi ya mfano ya millioni 568 walizokabidhiwa. 
Na Jacquiline Mrisho – Maelezo.
TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inategemea kukabidhi jumla ya shilingi bilioni 568.575, 000/= kwa vijana 12 waliobuni mawazo bora yatakayosaidia kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya Afya hapa nchini.
Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hassan Mshinda aliyasema hayo hivi karibuni Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua mradi wa Data for Local Impact Innovation Challenge (DLI) uliopo chini ya Atamizi ya DTBi yenye lengo la kuleta mapinduzi katika matumizi ya taarifa na takwimu mbalimbali katika sekta ya Afya.
Dkt. Mshinda alisema shughuli za ujasiriamali na ubunifu ni muhimu na chachu ya maendeleo ya nchi yoyote kwa kuwa zinasaidia kutengeneza ajira, kuongeza wigo wa shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuchangia katika pato la taifa.
Alisema Serikali kupitia COSTECH iliamua kuanzisha Atamizi ya DTBi mwaka 2011 ili kuwasaidia wajasiriamali wanaoshughulika na suala la TEHAMA.
“Nafahamu mradi huu umejikita katika changamoto za matumizi ya taarifa katika sekta ya afya, maendeleo ya kiuchumi na usawa wa kijinsia kama yalivyotanabaishwa katika malengo ya maendeleo endelevu, ubunifu hasa katika eneo la TEHAMA ni muhimu sana kwa sababu unasaidia kuongeza tija na ufanisi wa utoaji huduma katika sekta mbalimbali nchini”,Alisema.
Aidha Dkt. Mshinda alisema nia ya DTBi ni kuwawezesha Vijana, kuwajengea uwezo na kuwapa misaada ya msingi wataalam na wabunifu wa kitanzania waliopo katika eneo la TEHAMA ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya kitanzania kwa kutumia teknolojia.                              
Dkt. Mshinda aliwahakikishia wajasiriamali hao kuwa COSTECH itaendelea na juhudi zake za kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikali na taasisi za fedha kukabiliana na changamoto ya masharti ya mikopo kwa wajasiriamali.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa DTBi, Agapiti Manday alisema wanapokea mawazo mbalimbali ya vijana na kuyachuja na baadae wanachukua vijana wachache walio na mawazo bora zaidi na kuwawezesha ili waweze kuweka mawazo yao katika vitendo.
“Tunafahamu kuwa wapo vijana wengi mtaani wanaomaliza elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu ambao wana mawazo bora ya kuipeleka Tanzania mbele kimaendeleo lakini fursa hiyo wanaikosa kutokana na kukosekana kwa fedha na miongozo ya kuyafanya mawazo yao kuwa katika vitendo hivyo mradi huu unawasaidia vijana kuweka mawazo kuwa vitendo,”alisema Manday.
Bw. Manday Amefafanua kuwa changamoto kubwa ya wajasiriamali wa kitanzania ni ukosefu wa mitaji ya kufanikishia au kuendeleza shughuli zao za kiujasiriamali hivyo kwa kupitia mradi huo wataendelea kusaidiwa hadi pale watakapoweza kusimama kwa nguvu zao wenyewe.
Mradi huo mpya kwa Tanzania, umefadhiliwa na Mfuko wa Rais wa Marekani katika Vita dhidi ya Makali ya UKIMWI (PEPFAR) na kusimamiwa na taasisi ya serikali ya marekani ya Changamoto za Millenia (MCC), Mradi huu umeanza utekelezaji mnamo mwezi Aprili mwaka 2016.

No comments:

Post a Comment