Afisa Habari Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana,
Ajira na Wenye Ulemavu Bw. Ridhiwani Wema akiongea na waandishi wa habari
kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini. Kulia ni Mkurugenzi
Msaidizi Huduma za Ajira kutoka Ofisi hiyo Bw. Robert Masingiri.
Na Fatma Salum – Maelezo
SERIKALIimetoa wito kwa vijana kote nchini
kuchangamkia fursa ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali kupitia Programu ya
Kukuza Ujuzi Nchini inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Huduma
za Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Bw.
Robert Masingiri wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
kuhusu programu hiyo.
Masingiri alibainisha kuwa programu hiyo ni muhimu
kwa vijana kwani itawawezesha kupata ujuzi na stadi stahiki ili kumudu
ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Utekelezaji wa programu hii ni hatua za makusudi
za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi
ya Taifa.” Alisema Masingiri.
Aliongeza kuwa kiwango cha ujuzi hakijafikia hatua
nzuri ya kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati hivyo Serikali imetenga
shilingi bilioni 15 kwa ajili ya programu hiyo na utekelezaji wake umeanza
mwaka wa fedha 2015/2016 hadi 2020/2021.
“Programu hii inalenga kuziba pengo kubwa lililopo
la ukosefu wa ujuzi katika sekta za utalii, ujenzi, viwanda, nishati na madini
ambapo utawawezesha vijana wengi kuajirika na kujiajiri.” Alisema Masingiri.
Akifafanua kuhusu mfumo wa utekelezaji wa programu
hiyo, Afisa Habari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ridhiwani Wema alisema kuwa
programu hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali kwa njia ya
uanagenzi (apprenticeship) ambapo lengo ni kuwafunza vijana 3000 katika viwanda
vya nguo na vijana 1000 katika sekta ya ngozi.
Wema aliongeza kuwa program hiyo pia inatekelezwa
kupitia urasimishaji wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi (Recognition of
Prior Learning) na vijana 3900 watarasimishwa kupitia sekta ya ujenzi, utalii
na ukarimu.
Aidha kupitia program hiyo wahitimu 4000 watapata
mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi na wafanyakazi 13400 watapatiwa mafunzo ya
kuongeza ujuzi.
“Ofisi ya Waziri Mkuu imesaini mikataba na VETA na
Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ili watoe ujuzi kwa vijana kote
nchini na kupitia programu hiyo mafunzo hayo yanagharamiwa na Serikali , hakuna
malipo.” Alieleza Wema.
Serikali imejipanga kuendelea kukamilisha miongozo
ya ukuzaji ujuzi kwa njia mbalimbali itakayowezesha wadau kushiriki katika
utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili kufikia sera ya kukuza
viwanda na kujenga uchumi wa kati.
No comments:
Post a Comment