TANGAZO


Tuesday, February 28, 2017

SMZ YAKABIDHIWA VIFAA VYA MILIONI 78 KUBORESHA HUDUMA YA MACHO

Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo (katikati) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Chwaka, Bhagwanji Meisuria (kushoto) wakikabidhiwa moja ya vifaa vya huduma za macho vilivyotolewa na Mkurugenzi wa SightSavers, Gosbert Katunzi. Makabidhiano hayo yamefanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar. 
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo akitoa neno la shukrani baada ya kukabidhiwa vifaa vya huduma ya macho kutoka shirika la SightSavers, kutoka kulia ni Mkurugenzi wa shirika hilo, Gosbert Katunzi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Chwaka, Bhagwanji Meisuria. Makabidhiano hayo yamefanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar. 
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo (Kushoto), Mbunge wa Jimbo la Chwaka, Bhagwanji Meisuria (katikati) pamoja na Mkurugenzi wa SightSavers, Gosbert Katunzi (kulia) wakifurahia jambo baada  kumalizika kwa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya huduma za macho visiwani Zanzibar. 
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo akiwa katika picha ya pamoja na wadau na wafanyakazi wa Shirika la SightSavers baada kumalizika kwa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya huduma za macho visiwani Zanzibar.
Na Jacquiline Mrisho – Maelezo.
SHIRIKA la kimataifa lisilo la kiserikali la Sightsavers limekabidhi vifaa vyenye   thamani ya shilingi 78,765,898 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili visaidie katika kuboresha huduma za macho na kutokomeza upofu unaoweza kutibika.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa hivi karibuni Mjini Unguja na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Gosbert Katunzi ambaye alisema msaada huo ni mwendelezo wa mkakati wa shirika hilo kusaidia juhudi za Serikali katika kuinua huduma za Afya.
Katunzi alisema tangu mwaka 2012-2016 jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimetumika katika kutoa misaada kwenye sekta ya afya ambapo vifaa pekee vimegharimu jumla ya kiasi cha shilingi 309,419,399.
Pia jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimetumika katika kukarabati majengo ya matibabu ya macho katika Hospitali za Mnazi Mmoja, Wete na Chakechake Vision Centre, kusomesha wataalam wa macho wa kada mbalimbali, manunuzi ya dawa, kufanya uhamasishaji jamii pamoja na kuwezesha huduma karibu na wananchi.
“Katika kipindi cha miaka mitano wananchi takribani 1,065,060 wamenufaika na huduma za uchunguzi wa macho ambapo kati ya wananchi 4,307 waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho watoto ni 408, waliopatiwa miwani ni 18,529 na waliopatiwa matibabu mengine ya macho ni 300,640,” alisema Katunzi.
Aidha, Katunzi alivitaja baadhi ya vifaa vilivyotolewa na taasisi yake kuwa ni kifaa cha kuchunguza saratani ya macho pamoja na  vifaa vya uchunguzi wa macho(uoni) kiujumla pamoja na lensi mbalimbali za kutengenezea miwani ya watoto na watu wazima.
Amefafanua kuwa Sightsavers imekuwa mstari wa mbele kutoa huduma za afya ya macho na kuendelea kufanya maboresho zaidi katika vituo mbalimbali vya afya ili kutokomeza upofu unaozuilika hivyo kuwa na Taifa lisilokuwa na magonjwa yanayozuilika.
Pia Katunzi alimshukuru Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo pamoja na watendaji wa Wizara yake kwa kudumisha ushirikiano na taasisi yake pamoja na wadau mbalimbali wa afya katika kuhakikisha wananchi wa visiwani wanafikiwa na huduma za afya.
Shirika la Sightsavers ni shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linalofanya kazi kwa ushirikiano wa nchi zinazoendelea katika kuzuia upofu unaozuilika, pamoja na kusaidia wagonjwa wa macho wenye uoni hafifu na ulemavu unaotokana na magonjwa ya macho,Sightsavers ilianza kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment