Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu
wa Rais Profesa Faustin Kamuzora (kulia), akitoa Tamko la Siku ya Mazingira Afrika kwa
niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.
January Mkamba, Leo katika mkutano na waandishi wa Habari Mtaa wa Luthuli
Jijini Dar es Salaam, Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira wa Ofisi hiyo
Bw. Richard Muyungi.
TAMKO LA WN-OMR - MMZ BW. JANUARY Y. MAKAMBA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wananchi,
Tarehe 3 Machi kila mwaka watanzania wote huungana
na nchi nyingine za Afrika katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Afrika, ambayo
huadhimishwa barani Afrika kila mwaka. Siku
hii imetengwa kwa lengo la kukumbuka umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira
barani Afrika.
Azimio la kuadhimisha Siku hii lilipitishwa
na kuamuliwa na Baraza la Mawaziri wanaosimamia Mazingira wa nchi za Afrika
kwenye mkutano uliofanyika Durban, Afrika Kusini Mwaka 2002. Siku hii
iliamuliwa iwe kielelezo cha kukuza weledi kuhusu kupambana na uharibifu wa
mazingira pamoja na kuenea kwa hali ya jangwa Afrika. Kuanzia wakati huo siku
hii ilikuwa inaadhimishwa nchini Ethiopia kwenye makao makuu ya Umoja wa
Afrika.
Ndugu
Wananchi,
Kikao
cha 12 cha Baraza la Mawaziri wa Mazingira (AMCEN) kiliamua kwamba maadhimisho
ya siku hii yawe yanafanyika kikanda. Hivyo kuanzia mwaka 2009 maadhimisho ya
siku ya Mazingira Afrika yalianza
kufanyika kikanda katika nchi za Afrika na ndipo, mwaka 2010 nchi yetu ikapata fursa
ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya yaliyofanyika
jijini Arusha.
Aidha,
Umoja wa Afrika kwa kutambua juhudi na kazi iliyofanywa na Prof. Wangari
Maathai kutokana na mchango
wa mwanamke huyu katika hifadhi ya mazingira na
kuwezesha wanawake katika usimamizi endelevu wa maliasili na mazingira
kwa ujumla waliamua tarehe 3 Machi kila mwaka iwe pia ni siku ya
kumkumbuka yake iende sambamba na maadhimisho ya siku ya Mazingira Afrika.
Hivyo tangu mwaka 2012 maadhimisho ya Siku ya Mazingira Afrika yamekuwa
yakienda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wangari Maathai ili kutambua mchango wake katika
utunzaji wa Mazingira. Mwanamke huyu alipata Tuzo ya heshima ya Nobel Laureate's green legacy kutokana
na juhudi alizofanya.
Ndugu
Wananchi,
Tunapoadhimisha siku hii tutafakari kwa kina
changamoto mbalimbali zinazochangia uharibifu mkubwa wa Mazingira. Changamoto
hizo ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kuongezeka kwa hali ya jangwa na
ukame, uchafuzi wa mazingira, ongezeko kubwa la idadi ya watu, kuwepo kwa shughuli
za kiuchumi zisizoendelevu ambazo husababisha uharibifu wa mazingira.
Hali hizo
husababisha ongezeko la joto, ongezeko la ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko,
ongezeko la magonjwa mbalimbali ya mlipuko, upotevu wa bioanuai, uhaba wa
chakula na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko la umaskini kwa jamii.
Ndugu
Wananchi,
Tunafahamu kabisa hali ilivyo sasa katika maeneo mengi
nchini kwamba majira ya mvua yamebadilika na kusababisha ukame. Hivyo, inabidi
tuhakikishe tunavilinda vyanzo vya maji kwa gharama yoyote ile. Aidha, katika
kuadhimisha maadhimisho haya, kila mmoja awawajibike ipasavyo katika
kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi yasiyoendelevu
ya bioanuai na rasilimali zake.
Hivyo kila mtu afanye shughuli za kiuchumi
zisizoharibu mazingira ikiwa ni pamoja na kutumia nyenzo za uvuvi endelevu, kutumia
nishati jadidifu, majiko sanifu na banifu, nishati mbadala, kudhibiti uchafuzi,
kupunguza uzalishaji wa taka na kusimamia ukusanyaji wa taka ili kuhakikisha
miji yetu inakuwa safi.
Ndugu
wananchi,
Natoa wito kwa watanzania tuadhimishe Siku ya Mazingira
ya Afrika kwa kuendeleza na kusisitiza kampeni ya usafi katika maeneno yetu. Aidha,
ninawagiza wananchi wote kuanzia ngazi ya Kaya, Mitaa, vikiwemo vikundi vya
watu binafsi kushiriki kwenye shughuli za usafi ili kuhifadhi mazingira yetu.
Nitumie
fursa hii kuwakumbusha viongozi kuanzia
ngazi ya kijiji hadi mkoa kutumia fursa hii kuhuisha Kamati za Mazingira
ili ziweze kusimamia shughuli za utunzaji mazingira katika maeneo yao.
Aidha, mikoa,
halmashauri za wilaya, sekta zote, pamoja na taasisi mbalimbali, mashirika
yasiyo ya kiserikali na wananchi wote
kwa ujumla kushiriki katika shughuli za hifadhi na usafi wa mazingira wakati wote.
Ndugu
wananchi,
Katika kuadhimisha siku hii, natoa wito pia kwa
viongozi na watendaji katika ngazi zote kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya
utunzaji wa mazingirakwa kuzingatia sheria
ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na Kanuni
zake.
Baada ya kusema hayo, nawatakieni maadhimisho ya
Siku ya Mazingira Afrika yenye ufanisi.
Asanteni
kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment