Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe.
Semistocles Kaijage (Katikati) akitoa Risala kuhusu upigaji wa Kura katika
uchaguzi mdogo wa Ubunge jimbo la Dimani Zanzibar na Kata 19 za Tanzania Bara leo mjini Zanzibar. Kushoto ni Makamu
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Hamid M. Hamid na
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe (kulia).
Waandishi wa Habari wakiuliza maswali mbalimbali wakati wa
Mkutano huo.
Na Aron Msigwa –NEC, Zanzibar.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewataka wananchi wanaoishi katika kata 19
zitakazofanya Uchaguzi mdogo wa Madiwani
kwa upande Tanzania Bara na
Ubunge katika jimbo la Dimani Zanzibar, Januari 22, 2017 wajitokeze kwa wingi
kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka watakaowaongoza kwa kipindi cha
miaka 3.
Akizungumza
na vyombo vya Habari leo mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) Jaji wa Rufaa, Mhe. Semistocles kaijage amesema kuwa maadalizi ya
Uchaguzi huo yamekamilika na wananchi wote wenye sifa za kupiga kura katika
uchaguzi wajitokeze wingi kutimiza wajibu wao wa Kikatiba.
Mhe. Kaijage amewapongeza wananchi wanaoishi katika Jimbo la Dimani, Zanzibar na wale wa Kata 19 za Tanzania Bara
watakaofanya uchaguzi mdogo hapo kesho (Januari 22, 2017) kwa utulivu waliouonyesha
katika kipindi chote cha Kampeni za wagombea wa vyama mbalimbali vya Siasa.
Amesema licha ya kuwepo kwa
dosari za hapa na pale zilizojitokeza zikiwemo za ukiukwaji wa Maadili ya
Uchaguzi kwa baadhi ya Vyama na wagombea wao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
ilichukua hatua za kukemea vitendo hivyo ili kuwezesha Kampeni za Uchaguzi
kufanyika kwa Usalama na Amani.
“Licha ya kwamba kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia
kura, Ni matumaini ya Tume kuwa hali ya Amani na Utulivu ambayo imekuwepo hadi
sasa na kama ilivyokuwa katika Chaguzi zilizopita itaendelea kudumishwa ili
kuhakikisha uchaguzi huu unafanyika kwa Utulivu, Amani na Ustawi wa Taifa letu”
Amesema Jaji Kaijage.
Ameeleza kuwa katika uchaguzi huo jumla ya
Wapiga Kura 9,280 wa Jimbo la Dimani Zanzibar wanatarajiwa kupiga kura ili
kumchagua Mbunge atakayewaongoza kwa kipindi cha miaka 3 kupitia vituo 29 vya
Kupigia Kura katika Jimbo hilo.
Kwa upande wa Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika Kata 19 za Tanzania
Bara Wapiga Kura 134,705 walioandikishwa wanatarajia kupiga kura katika vituo 359 ambavyo vilitumika katika
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Naomba nitumie fursa hii kutoa rai kwa wananchi waliojiandikisha wajitokeze
kwenye vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili waweze
kupiga kura kuwachagua viongozi mnaowataka bila hofu, woga, wasiwasi au
ushawishi” Amesisitiza.
Kuhusu mchakato mzima upigaji wa kura ikiwemo taratibu za kuzingatiwa
na wananchi kwenye vituo vya kupigia Kura, uhesabuji wa Kura, ujumlishaji wa
Kura na Utangazaji wa matokeo amesema kuwa hatua zote zitafanywa na Wasimamizi
wa Uchaguzi kwa kuzingatia Sheria.
Amesema kuwa siku ya uchaguzi Januari 22, 2017 vituo vyote vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa
saa 10:00 jioni na kufafanua kuwa iwapo wakati wa kufunga Kituo watakuwepo
Wapiga Kura katika mstari ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga
wataruhusiwa Kupiga Kura.
Jaji Semistocles amesisitiza kwamba mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga
katika mstari wa Wapiga Kura baada ya saa kumi (10:00) jioni muda ulioainishwa kisheria.
Ameeleza kuwa kwa kila mpiga kura katika jimbo hilo akumbuke kubeba
Kadi yake ya Mpiga Kura kwa kuwa Sheria ya Uchaguzi inaelekeza kuwa ili Mpiga
Kura aruhusiwe kupiga kura ni lazima awe na kadi ya Mpiga Kura.
“ Naomba ieleweke wazi kuwa Fomu Na. 17 sio mbadala wa Kadi ya Mpiga
Kura, Wapiga Kura ambao wana Kadi ya Mpiga Kura lakini
taarifa zao hazimo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Kituoni, hawataruhusiwa
kupiga kura” Amesisitiza Jaji Kaijage.
Amesema kuwa ni marufuku na ni
kosa la jinai kumkataza mtu kwenda Kupiga Kura akisisitiza kwamba siku hiyo ya
kupiga kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wanawake
wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee ambao hawatatakiwa kupanga mstari.
Jaji Semistocles amefafanua kuwa wakati wote wa Kupiga Kura na Kuhesabu
Kura, Mawakala wa Vyama vya Siasa watakuwepo kwenye vituo kwa kuwa wajibu wao
ni kulinda maslahi ya Vyama vyao vya Siasa na Wagombea wao.
Hata hivyo amesema hawatakiwi
kuingilia masuala ya utendaji ambayo yamekabidhiwa kwa Msimamizi wa Kituo.
Amesema Mawakala hao wataruhusiwa kuwepo Vituoni
kwa mujibu wa Sheria na Kanuni na kusisitiza kwamba Wakala asiyekuwa na barua
ya utambulisho kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi na ambaye hatakula kiapo cha
kutunza siri hataruhusiwa kuingia katika Kituo cha Kupigia, Kuhesabia na
Kujumlishia Kura.
Katika hatua nyingine Jaji Kaijage amebainisha kuwa Kura zilizopigwa zitahesabiwa katika Kituo cha Kupigia Kura
mara tu Upigaji Kura utakapokamilika na
matokeo husika ya Kituo kujazwa kwenye
Fomu za Matokeo Na. 21B kwa upande wa Ubunge na Fomu Na. 21C kwa upande wa Udiwani kisha fomu hizo kutiwa saini na
Msimamizi wa Kituo/Msimamizi Msaidizi wa Kituo, Mawakala wa Vyama au Mgombea
aliye Kituoni.
Amesema nakala moja watapewa Mawakala/Mgombea na nakala nyingine
itabandikwa nje ya Kituo cha Kuhesabia kura ambapo Wakala wa kila Chama cha
Siasa na mlinzi wa Kituo watakaokuwa Kituoni wataruhusiwa kusindikiza msafara
wa kupeleka matokeo ya Uchaguzi kwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi/Msimamizi Msaidizi
wa Uchaguzi wa Kata kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Msimamizi wa
Uchaguzi/Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Dimani kwa upande wa
Zanzibar.
Amefafanua kuwa matokeo yote yakishapokelewa na Msimamizi wa Uchaguzi
kwa upande wa Uchaguzi wa Ubunge na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kwa upande
wa Uchaguzi wa Udiwani, yatajumlishwa mbele ya Mawakala na wote wanaoruhusiwa
kuingia kwenye vituo vya Kujumlishia Kura.
“ Kama ilivyokuwa wakati wa Kuhesabu Kura, baada ya Ujumlishaji
kukamilika matokeo ya Ubunge ngazi ya Jimbo yatajazwa katika Fomu Na. 24B na
yale ya Diwani katika Kata yatajazwa katika Fomu Na. 24C, Fomu za Matokeo hayo
zitatiwa saini na Msimamizi wa Uchaguzi na Mawakala watakaokuwepo watapewa nakala
za Fomu za Matokeo na Nakala moja itawekwa mahali pa wazi nje ya Kituo cha
Kujumlisha Kura”
Akitoa ufafanuzi kuhusu kampeni za uchaguzi huo
amesema zitamalizika leo (Januari 21) saa 12 jioni na Vyama, Wagombea na mashabiki
hawataruhusiwa kufanya kampeni za aina yoyote ikiwa ni pamoja na kutumia alama
zozote zinazoashiria Kampeni kama vile bendera na mavazi ya vyama vyao.
Kuhusu uwazi katika uendeshaji wa uchaguzi huo
amefafanua kuwa vyama vyote vya Siasa vinavyoshiriki katika Uchaguzi vinatakiwa kuhakikisha kwamba vinaweka
Mawakala katika vituo vyote vya Kupigia Kura na Kujumlishia Kura ambao
watatimiza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.
Jaji Kaijage amesisitiza kuwa kwa kuzingatia
Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 yaliyokubaliwa na Vyama vyote vya Siasa,
Wapiga Kura wanatakiwa kuondoka Vituoni mara baada ya kupiga kura ili kuendelea
na shughuli zao kwa kuwa Vyama vya Siasa
vyenye wagombea vitakuwa na Mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya Vyama na
Wagombea wao huku watu waliotajwa kwenye Sheria ya Uchaguzi wakiwemo Wagombea, Mawakala,
Afisa wa Tume, Msimamizi wa Uchaguzi na Afisa Usalama ndiyo watakaoruhusiwa
kuingia kwenye Vituo vya Kupigia, Kuhesabia na Kujumlishia Kura.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za
Sheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe amewaaeleza waandishi wa Habari kuwa kwa
mujibu wa sheria mwenye mamlaka ya kumtangaza Mshindi ngazi ya Ubunge ni
Msimamizi wa Uchaguzi na kwa ngazi ya Udiwani mwenye mamlaka ya kufanya hivyo
ni Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.
Amesema kuwa zoezi la Kupiga Kura, Kuhesabu kura
,Kujumlisha Matokeo na Kutangaza matokeo litafanywa kwa uwazi na kwa kuzingatia
Sheria na kutoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kuwachagua viongozi wao.
Amesema kuwa wananchi watakaoruhusiwa kupiga kura
ni wale wenye sifa ambao watakuwa na kadi za kupigia kura na ambao majina yao
yameonekana kwenye Daftari la kudumu la kupigia Kura na kusisitiza kwamba
mwananchi ambaye jina lake halitakuwa kwenye Daftari la Kudumu la kupigia kura
hataruhusiwa kupiga kura.
“Utaratibu wa kupiga kura umeelezwa katika Sheria,
Ukisoma kifungu cha 63 kifungu kidogo cha 3 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi A,
kinaeleza wazi mwananchi anapofika kituoni alipopangiwa na Tume anaonyesha kadi
yake ya kupigia kura na kisha jina lake linaitwa kwa sauti na ikiwa amekidhi sifa
anaruhusiwa kupiga kura asipokidhi sifa Msimamizi wa Uchaguzi anayo Mamlaka ya
kumzuia asipige Kura” Amesema.
No comments:
Post a Comment