TANGAZO


Tuesday, January 24, 2017

TAASISI YA MOYO YAFANYA UPASUAJI WA KUZIBUA MISHIPA YA MOYO ILIYOZIBA KWA ASILIMIA 100 NA KUSHINDWA KUPITISHA DAMU

Jengo la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) 

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Madaktari Afrika kutoka nchini Marekani kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization Procedure) kwa mgonjwa na kuzibua mshipa wa Moyo uliokuwa  imeziba kwa zaidi ya miezi mitatu (kwa lugha ya kitaalamu Chronic Total Occlusion).

Upasuaji huo ambao unatumia mishipa ya damu ulichukuwa muda wa saa moja kwa  kuzibua mshipa mmoja wa damu ambao ulikuwa umeziba kwa asilimia 100 na   kushindwa kupeleka  damu upande wa kushoto wa moyo.

Kambi ya Madakari wa Afrika imeanza tarehe 23/1/2017 na inatarajiwa kumalizika tarehe 29/1/2017. Hadi sasa jumla ya  wagonjwa sita wameshapatiwa huduma za matibabu ya moyo ambayo ni kuzibua mishipa ya moyo iliyokuwa imeziba. Hali za wagonjwa zinaendelea vizuri na wanatarajiwa kuruhusiwa siku yoyote kuanzia kesho.

Tangu kuanza kwa mwaka huu wagonjwa 29  wameshafanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kati ya wagonjwa hao 23 wamefanyiwa upasuaji katika kambi za ndani na wagonjwa sita wamefanyiwa upasuaji katika kambi ya Madaktari Afrika.

Taasisi inaendelea kuwaomba  Madaktari wote nchini wenye wagonjwa wao wa matatizo ya  moyo wawatume wagonjwa hao katika Taasisi ya Moyo  ili waweze kupatiwa matibabu. Kwa mawasiliano zaidi wawasiliane na Dkt. Peter Kisenge kwa namba 0713 236 502 na  022-2151379 ambaye atawaelekeza  utaratibu wa kuwatuma  wagonjwa hao.

Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

24/01/2017

No comments:

Post a Comment