TANGAZO


Saturday, January 21, 2017

MAKALA:"KUENDELEZA MILA ZA UKEKETAJI NI KINYUME CHA HAKI ZA MTOTO"-SIHABA NKINGA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Sihaba Nkinga

Na Hassan Silayo-Maelezo
MKOA wa Mara ni Moja ya Mikoa ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikiendelea na utamaduni wa kukeketa watoto wa kike jambo ambalo ni kinyume na haki za mtoto na sheria mbalimbali duniani.

Kila mwaka takribani watoto milioni mbili wako katika hatari ya kukeketwa ambako kwasasa Tanzania ina asilimia 32 ya hali ya ukeketaji suala ambalo Serikali hairidhiki nalo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga alifanya ziara ya siku 2 Mkoani Mara katika Wilaya za Tarime na Musoma.

Katika ziara hiyo Bi. Sihaba ambayo alimuwakilisha Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika mahafali ya 9 ya Kituo cha kulea watoto waliokimbia ukeketaji cha Masanga (ATFGM) katika kata ya Masanga Tarime Vijijini.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu Bi. Sihaba alionesha kushangazwa na vitendo vya ukeketaji vinavyofanywa na wenyeji wa Mkoa wa Mara na kuviita ni vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wa kike, kwani inakatisha ndoto na matarajio ya watoto hao.

Akitoa kauli ya Serikali Bi. Sihaba alisema kuwa Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria watakaogundulika kuendeleza vitendo vya ukeketaji kwani ni kinyume na Sheria ya Nchi na nikinyume na mikataba mbalimbali ya Kimataifa iliyojielekeza katika kulinda haki mbalimbali za mtoto.

Akionesha kudhamiria kukabiliana na tatizo la ukeketaji katika mkoa wa Mara Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga alikutana na Wazee wa kimila kutoka Koo tano za Bukenye, Nyabasi, Bukira, Butimbaru, Buhunyaga.

Katika mazungumzo hayo yaliyolenga kuweka mikakati ya kukomesha tamaduni ya ukeketaji mkoani Mara, Mzee wa kimila kutoka Koo ya Bukenye Mzee Elias Maganya alisema kuwa walishapata elimu kutoka kwenye Jukwaa la Kulinda Utu wa watoto(CDF) na changamoto ni jinsi ya kuzifikia koo nyingine Mkoani huko ili kuwezesha kuondoa kabisa mila hiyo.

Mzee Elias alisema kuwa sasa ni jukumu la Serikali kuona umuhimu wa kuwawezesha kutembea Koo hadi Koo kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji.

Naye Mzee wa Kimila kutoka Koo ya Bukira Mzee Sinda Nyangore ameishauri Serikali na mashirika mengine kutoa elimu katika vipindi vyote vya mwaka na kuacha utaratibu wa kutoa elimu katika msimu wa ukeketaji kwenye koo mbalimbali.

Aidha,Mzee kutoka koo ya Butimbaru Mwita Nyasibora alishauri mpango wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji yafanyika kwa wakati wote badala ya kusubiri kipindi cha ukeketaji ndipo serikali na asasi nyingine za kiraia kujitokeza kutoa elimu.

Akijibu hoja hizo Bi. Sihaba Nkinga amesema kuwa, kweli upo umuhimu wa kutekeleza suala hilo la kupeleka elimu juu ya madhara ya ukeketaji ili kuweza kuwasaidia watoto wakike katika koo hadi koo kwani tofauti na hapo lengo kusudiwa haliwezi kufikiwa na itakuwa ni tofauti na malengo ya serikali katika kupambana na tamaduni ya ukeketaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tarime Bw. Glorius Luoga katika hotuba yake aliyoitoa katika mahafali hayo, aliyataja majina ya mangariba maarufu ambao wanatafutwa na vyombo vya dola kwa vitendo vya ukeketaji katika maeneo mbalimbali wilayani Tarime.

Mkuu wa Wilaya huyo pia, alisema ofisi yake imeshawapeleka katika vyombo vya Sheria baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji na kuahidi kuendelea kuwachukulia hatua kali za Kisheria wale watakaoendelea na vitendo hivyo vya ukeketaji.

Aidha, Bw. Luoga alioneshwa kuchukizwa na aina ya wazazi na walezi wanaolazimisha kuwatahiri watoto wa kiume kwa mara ya pili baada ya tohara salama kwani kitendo hicho ni sawa na kumjeruhi mtoto.

Akiongea na wahitimu, wazazi, walezi na mangariba wastaafu, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bi. Lydia Bupilipili alisema, wazazi na walezi wanapaswa kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wa kike shuleni ili waweze kutimiza ndoto walizojiwekea katika maisha yao.

Akiongea mbele ya Mkurugenzi wa Kituo cha Kulea Watoto waliokimbia Kukeketwa cha (ATFGM-Massanga) Sister Stella Mgaya aliishukuru Serikali ya Wilaya na Wizara ya Afya kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa ushirikiano wanaoupata pale wanapohitaji.

Aidha, Sister Stella Mgaya alisema kuwa kituo hicho kimekuwa kikikumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kuwa na idadi kubwa ya watoto kituoni hapo baada wanaokataliwa na wazazi/walezi pindi wanapotoka kituoni hapo hivyo kuongeza gharama ya kuwapeleka shuleni, Sister Mgaya

Wakisoma risala kwa mgeni rasmi wahitimu wa kituo cha kulea watoto cha masanga walitoa maombi yafuatayo kwa Katibu Mkuu Bi. Sihaba Nkinga waliomba kuendelezwa kielimu pindi wanapomaliza kituoni hapo wakati mwingine wanakataliwa na kutengwa na wazazi/walezi wao.

Aidha, Watoto hao waliiomba pia serikali kukamata wazazi/walezi wanaowalazimisha kukeketwa pindi wanapotoka kituoni hapo na kuendelea na kuutilia mkazo utaratibu wa kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wazazi,walezi na mangariba wanaojihusisha na kazi ya ukeketaji ikiwemo kifungo cha miaka 5-10 jela.

Rai yangu kwa watanzania na hasa makabila yanayoendeleza mila ya ukeketaji wa watoto wa kike ni kuacha tamaduni hii ambayo ni kinyume na sheria za nchi na hata mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kumlinda mtoto wa kike. Pia ni muda wa kujikita katika kumuendeleza mtoto wa kike kielimu ili waweze kutimiza malengo na ndoto walizojiwekea kwani “Tanzania Bila ukeketaji inawezekana”

No comments:

Post a Comment