TANGAZO


Sunday, January 22, 2017

BALOZI SEIF IDDI AZINDUA UVUNAJI WA MPUNGA WA UMWAGILIAJI WA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA SHADIDI BONDE LA CHEJU KISIWANI UNGUJA

Moja miongoni mwa Ploti za Mpunga uliooteshwa kupitia Mradi  wa kuongeza Tija na uzalishaji katika zao la Mpunga Zanzibar kwenye Bonde la Cheju Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ) 
Mkulima Rashid Khamis  (mwenye kipaza sauti), akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  kulia yake jinsi alivyafaidika na Kilimo cha Mpunga kupitia Mradi wa kuongeza Tija na uzalishaji katika zao la Mpunga Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mheshimiwa Hamad Rasid Mohamed. 
Balozi Seif na Mkewe Mama Asha Suleiman kati kati wakijumuika pamoja na Mawaziri, Viongozi wa Serikali, Wakulima na Wananchi katika uzinduzi wa  Uvunaji wa Mpunga wa Umwagiliaji Maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi. Wa kwanza kutoka kulia ni Waziri anayesimamia Tawala za Mikoa Mh. Haji Omar Kheir, Waziri wa Fedha Dr. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Moh’d Aboud Moha’d na Waziri wa Kilimo Mh. Hamad Rasid Mohamed. Nyuma ya Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziki Pembe Juma. 
Balozi Seif akimuangalia Mkeke Mama Asha Suleiman akiwajibika katika uvunaji wa zao la mpunga kwenye uzinduzi rasmi wa mpunga wa Umwagiliaji maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi. 
Balozi Seif akizungumza na Viongozi, watendaji wa sekta ya Kilimo, Wananchi na Wakulima katika Bonde la Cheju mara baada ya kuzindua rasmi Uvunaji wa Mpunga wa Umwagiliaji Maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi. 
Balozi Seif akifurahia kazi kubwa inayofanywa na wakulima wa Mpunga katika Bonde la Cheju aliposimamisha ghafla  msafara wake  kwa lengo la kusaidia ubutaji wa Mpunga  kwenye moja ya mashamba yaliyomo ndani ya Bonde la Cheju.

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/1/2017.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar kuanzisha Duka Maalum litakalohusika na uuzaji wa mchele unaotokana na Mpunga unaozalishwa na Wakulima pamoja na Taasisi  za Zanzibar.

Alisema hatua hiyo muhimu itawapa hamasa  zaidi Wakulima wa zao hilo kuongeza juhudi za uzalishaji kupitia Mradi wa kuongeza Tija na uzalishaji wa Mpunga Zanzibar { ERPP } unaoonekana kuleta mafanikio makubwa ya kipato tokea kuanzishwa kwake katika kipidi kifupi kilichopita.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akizindua rasmi uvunaji wa Mpunga wa Umwagiliaji maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi inayosimamiwa na Benki ya Dunia hapo katika bonde la Mpunga Cheju Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema Zanzibar inaweza kupunguza uagizaji wa bidhaa za vyakula kama mchele kutoka nje ya nchi kutoka asilimia 80% hadi 40% ifikapo mwaka 2020 iwapo mkazo utaongezwa na wananchi walio wengi Vijijini wanaojihusisha na Kilimo katika kutekeleza mradi huo.

Balozi Seif aliwaagiza wataalamu wote wa Sekta ya Kilimo Nchini kuanzia sasa watalazimika kutumia muda wao wa kazi kuwa karibu zaidi na wakulima ili kufanikisha mradi huo na kuacha tabia ya kubakia Ofisini.

Alieleza kwamba Kilimo cha mradi wa shadidi ndio mkombozi pekeeunaoweza kuipunguzia Serikali kutumia fedha nyingi za Kigeni kwa ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara kuagiza bidhaa hiyo nje ya Nchi.

“ Lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kupunguza uagizaji wa bidhaa za vyakula kutoka nje ya nchi kwa kuongeza uzalishaji mara dufu “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru washirika wa Maendeleo wa Kimataifa kwa jitihada zao za kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika kuimarisha Miradi ya Maendeleo.

Alisema Zanzibar bado inaendelea kuungwa Mkono na Washirika mbali mbali wa  Maendeleo Duniani na kuiomba Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuendelea kutafuta washirika wengine wa Maendeleo watakaoweza kusaidia mipango ya Taasisi hiyo ili kuwaongezea nguvu zaidi za uzalsiahji wakulima wa Visiwa hivi.

Akisoma Risala kwa niaba ya wakulima wa Mradi wa Kilimo cha Mpunga  wa umwagiliaji Maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi  Mmoja wa Wakulima   hao alisema mradi huo umeleta mafanikio makubwa yaliyopelekea Robo eka kuvuna kati ya Polo 13 na 14 ikilinganishwa na kilimo cha zamani walichoambulia Polo 8 hadi 9.

Alisema pamoja na mfanikio hayo alizitaja changamoto zilizojitokeza  katika harakati zao za kilimo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usawa wa ardhi katika mabonde ya Kilimo hicho unaosababisha baadhi ya  ploti kukosa maji ya uhakika ya  kuimarisha kilimo hicho.

Wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iongeze wawekezaji zaidi watakaoshirikiana nao katika  kuimarisha miundombinu itakayosaidia kufanikisha Mradi huo wa Kuongeza Tija na uzalishaji katika zao la Kilimo.
Mapema Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid Mohamed alisema Teknolojia hiyo ya Shadidi ndio pekee inayoweza kuwakomboa Wakulima wakizingatia kufundishana kwa hatua ya awali ya kuona.

Mh. Hamad Rashid alisema  Hekta 500 pekee  ndio zenye miundombinu ya Kilimo cha Umwagiliaji Maji kati ya Hekta 8,500 za Mabonde yote ya yaliyomo Visiwani  Zanzibar.

Alisema  ushirikiano wa pamoja kati ya Viongozi, Wataalamu  wa Kilimo, Wananchi  na wakulima wenyewe katika  kuyatumia vyema mabonde yaliyobakia ya kilimo kwa kuendeleza Mradi wa Shadidi unaweza kupunguza au kuondosha kabisa uagizaji wa mchele kutoka nje ya Zanzibar.

Waziri wa Kilimo alifafanua kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo tayari imeshafanya mazungumzo ya pamoja na Muwekezaji Mzalendo watakaosimamia ufungaji bora wa Bidhaa za Zanzibar kwa kutumia nembo maalum  ili ziingie katika soko la Kimataifa kiuhakika.

No comments:

Post a Comment