Mzee Said
Mohamed Mannoro, Mkazi wa Wilaya ya Kilwa - Kivinje akitoa ufafanuzi kuhusu nafasi
ya wazee na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Na Aron Msigwa – Dar es Salaam
WATANZANIA hususan
vijana wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa
vitendo kwa kufanya kazi kwa bidi, kulinda na kudumisha amani iliyopo na
kufanya matendo yenye tija na manufaa kwa Taifa.
Wito huo umetolewa leo
jijini Dar es salaam na Mzee Said Maohamed Mannoro, Mkazi wa wilaya ya Kilwa - Kivinje
wakati akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu
nafasi ya wazee na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Amesema yeye kama mzee
anao wajibu wa kuwaeleza na kuwashauri vijana kuepuka kutumika kama chanzo cha kufanya
vitendo vinavyochochea vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo.
“Mahali ambapo panahatarisha
amani hakuna mjadala, suala la amani linapewa nafasi ya kwanza mambo mengine
yanafuata, hata kama kungekuwa na jambo zuri namna gani linalotaka kufanyika
linapohatarisha amani kwa upande mmoja au mwingine ni afadhali kuliacha”
Amesisitiza mzee Monnoro.
Amesema kuwa maandamano
yaliyopangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya Siasa Septemba mosi hayana sababu
ya kufanyika kwa kuwa yana ajenda ya kukosa uvumilivu kuhusu usahihi wa uongozi
wa nchi hivyo ni vyema wananchi wakayaepuka kwa kuendelea na shughuli zao za
kujiingizia kipato kwa kuwa amani haina mjadala.
Amesisitiza kuwa ni vyema
viongozi wa vyama vya hivyo wakatumia njia zinazostahili kutafuta ufumbuzi wa
kero zao kupitia mazungumzo ili kupata haki kuliko kuwahamasisha wananchi
kuandamana na kupambana na vyombo vya dola na jambo ambalo mwisho wake ni
kuleta vurugu zisizo na maana.
Aidha, amewaomba
viongozi hao wawe na busara na waheshimu maisha ya watu wanaowaongoza pia
waepuke kuwa na kiburi cha kujiona wao ni bora kuliko wanachama wao.
“Mimi nayezungumza hapa
niko upande wa upinzani, yanapokuja mambo ya kitaifa hayanizuii kuzungumza kwa
kuwa yana manufaa kwa taifa, nasema kiongozi yeyote anayewashawishi wafuasi
wake waandamane bila sababu za msingi ni kosa na jambo hili ni kupungukiwa na
busara” Amesema mzee Mannoro.
Amebainisha kuwa
kiongozi asiyeheshimu wala kujali maisha ya wananchi wake na kujiona anajua
kuliko wao hafai, anapoteza sifa za kuwa kiongozi akisisitiza kuwa watanzania
wanayo fursa nzuri ya kuchagua mustakabali mwema wa Taifa lao kwa kuwa amani ya
Tanzania haina mbadala.
Akifafanua kuhusu
utendaji wa viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali za Serikali kuanzia
kijiji hadi Taifa amesema kuwa katika nafasi zao wanao wajibu wa kulisaidia
Taifa kwa kuwa wasimamizi wa utekelezaji wa malengo ya Serikali yaliyopangwa.
“Sote tunafahamu Serikali imekuwa ikitekeleza
mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo suala la utoaji wa elimu bure haya
ndiyo mambo ya msingi ya kufuatilia na kusimamia kwa kila kiongozi katika
nafasi yake, tunapaswa kumsaidia Rais wetu kutekeleza malengo ya nchi.”
Amesisitiza.
Kuhusu maboresho ya
sekta ya elimu ameishauri Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuwekeza
katika miundombinu ya elimu hasa ujenzi wa madarasa na mabweni ili kuwawezesha
wanafunzi wanaokaa mbali na shule hususani eneo analotoka la wilaya ya Kilwa
Kivinje ili waweze kuondokana na tatizo la kutembea umbali mrefu.
Ametoa wito kwa watanzania hususan vijana
kujikita katika shughuli za kilimo na shughuli nyingine zinazoweza kuwaongezea
kipato badala ya kupoteza muda mwingi katika masuala yasiyo na tija kwa
maendeleo yao binafsi na taifa.
Amesisitiza kuwa Kilimo
sio adhabu kwa kuwa yeye mwenyewe pamoja na uzee wake shughuli za kilimo zimemsaidia
kujenga familia imara na kuendesha maisha yake akiamini kuwa utajiri wa kweli
uko kwenye ardhi.
“Kinachonigusa mimi ni maisha ya watu, nawaomba
watumishi wa Serikali waliosomea mambo ya kilimo wafanye kazi kwa bidi,
wawasimamie vijana wetu wanaolalamika mitaani kuwa hawana cha kufanya, tukiwajenga
na kuwasimamia vijana wetu katika misingi ya uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii
umasikini utaondoka.”
No comments:
Post a Comment