Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), Zaitun Hokororo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mwenyekiti Cecilia Augustino, Katibu Mwajuma Naty na Mjumbe Ziada Athumani.
Katibu wa Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania (UWASATA), Mwajuma Naty akisisitiza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kupinga maandamano ya yasiyo na ukomo.Kulia ni Mjumbe wa umoja huo Ziada Athumani.
Katibu wa UWASATA Mwajuma Naty, akieleza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kupinga maandamano yasiyo na ukomo yaliyoitishwa na Chadema. Kushoto ni Mwenyekiti Cecilia Augustino na Kulia ni Mjumbe wa umoja huo Ziada Athumani.
Mmoja wa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano
wa UWASATA akiuliza swali kwa Mwenyekiti wa umoja huo (hayupo pichani).
Na Hussein Makame-MAELEZO
UMOJA wa Wanawake Viongozi wa Vyama vya Siasa
Tanzania (UWASATA), umepinga maandamano yasiyo na ukomo yaliyotanganzwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa hayana tija kwa wananchi
na Tifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam leo, Mwenyekiti wa umoja huo Cecilia Augustino, alisema maandamano hayo
yanaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi wa Taifa la Tanzania.
Alisema wamefikisha tamko lao kwa Msajili wa Vyama
vya Siasa Jaji Francis Mutungi na kumtaka msajili kutoacha chokochocko hizo
ziendelee kwani zitasababisha kutoweka kwa amani nchini.
“Sisi wanawake viongozi wa vyama vya Siasa
Tanzania tunapinga azimio la maandamano yasiyo na kikomo yanayoandaliwa na
chama cha Chadema, hakika maandamano hayo hayana tija kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla” alisema Hokororo na kuongeza:
“Mheshimiwa Msajili, chokochocko hizi zinazofanywa
na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila ya kukemewa tunaamini tunu
yetu ya amani ambayo ni urithi wetu tulioachiwa na waasisi wetu itatoweka.”
Aliongeza kuwa hatma ya maandamano hayo ni kuingia
kwenye machafuko na hatimaye mauaji na mateso kwa wanawake, watoto na walemavu,
mambo ambayo hawatakubali yatokee.
Alibainisha kuwa wanawake viongozi wa vyama vya
siasa wanaamini kuwa siasa ni kushindana kwa hoja na si uvunjifu wa sheria kwa
njia ya maandamano yasiyo na tija kwa wananchi na Taifa.
Aliliomba Baraza la Vyama vya Siasa kuhakikisha
linawajibika katika kulinda demokrasia, amani na ustawi wa jamii nzima ya Watanzania.
Katika hatua nyingine, umoja huo unaojumuisha wanawake
viongozi wa vyama 22 vya siasa nchini, umeomba kufanya kongamano la amani lenye
lengo la kuhamasisha amani na utulivu nchini.
Hivyo, Hokororo aliwaomba viongozi wakuu wa nchi
kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
wadau wa amani na mashirika binafsi kushirikiana na umoja huo kufanikisha
kongamano hilo.
“Hakika tunaumia wanasiasa wanapokuwa chanzo cha
migogoro na vurugu kwa Taifa letu.Hivyo tunamuomba Rais wetu tunajua ni
msikivu aweze kuona namna nzuri ya
kutafuta suluhu ya mgogoro huu wa kisiasa” alisema Mwenyekiti Cecilia Hokororo.
Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la Vyama vya
Siasa Agost 31, mwaka huu ili kutoa fursa kwa pande vyama husika kukaa meza moja na kujadili tofauti zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja huo Ziada Athumani
alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwani ndio njia muwafaka ya pande husika ili
kufikia muwafaka kwa njia ya amani.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari,
wanawake viongozi wa vyama vya siasa waliwakilishwa na wenzao kutoka vyama vya
Demokrasi Makini, ADA TADEA na Chama cha Umoja wa Demokrasi ya Vyama Vingi
(UMD).
No comments:
Post a Comment