WATAALAMU wa Ukadiriaji Majenzi wameelezewa kuwa ni kada muhimu katika
kukabiliana na tatizo la rushwa pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za umma
katika sekta ya ujenzi dunia kote.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Hassan Suluhu wakati akimuwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika
hafla ya uzinduzi wa mkutano wa Kimataifa wa Wakadiriaji Majenzi barani Afrika
uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
“Ni matumaini yetu kwamba umuhimu wa huduma zinazotolewa na Wakadiriaji
Majenzi zina mchango mkubwa sana kwenye mapambano dhidi ya rushwa katika sekta
ya ujenzi”. Alisema Makamu wa Rais.
Mkutano huo wenye kauli mbiu isemayo “Kuelekea kufikia Malengo ya
Maendeleo Endelevu – Mchango wa huduma za Wakadiriaji Majenzi” umekuja wakati
muafaka ambapo Tanzania inahitaji kupata uzoefu kutoka kwa Wataalamu kutoka nje
ya nchi kwa kuwa ipo mbioni kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na imekusudia
kuwatumia Wataalamu wa ndani zaidi.
Aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa Wakadiriaji Majenzi hasa katika
kuleta uwazi Serikali itawatumia wataalamu hao katika kutekeleza mipango yake
ya ujenzi wa miundombinu iliyopangwa kutekelezwa ambapo ametaja baadhi ya
miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya kati kwa Kiwango cha Kimataifa
(Standard Gauge) na ujenzi wa Bomba la mafuta kutoka Bandari ya Tanga hadi
Uganda ujenzi unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais alipata fursa ya kutembelea baadhi
ya mabanda ya Taasisi zinazojihusisha na ujenzi ambapo alitoa pongezi kwa
Baraza la Ujenzi la Taifa (NCC) kwa jitihada zake katika utatuzi wa migogoro
itokanayo na sekta ya ujenzi, na kuwashauri kuongeza bidii katika kuhakikishi
inatoa huduma zake maeneo mengi zaidi.
Huduma zingine zitolewazo na baraza hilo
ni pamoja na ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu pamoja na majengo,
utafiti na ushauri wa kitaalamu.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa rai kwa
Wakadiriaji Majenzi kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili
kuepusha hasara zitokanazo na udanganyifu katika miradi ya ujenzi.
Aliongeza kuwa ni bora kuwa na Wakadiriaji Majenzi wachache ambao ni
waadilifu kuliko kuwa na lundo la wataalamu hao wasio waadilifu na kuongeza
kuwa uadilifu ndiyo sifa kuu katika taaluma yeyote.
“Bora kuwa na Wakadiriaji wachache wenye sifa ya uadilifu kuliko kuwa na
Wataalamu hao wengi wasio kuwa na maadili”. Alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Ukadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS)
Samuel N. Marwa ameiomba Serikali kuwatumia Wataalamu wa Ukadiriaji Majenzi kwa
kuwa wataalamu hao ni muhimu na kutapunguza mianya ya rushwa.
Wakadiriaji Majenzi wamejipanga kuhakikisha wanafanya majukumu yao ili
kutekeleza malengo ya manedleo endelevu na kuongeza kuwa karibu sekta zote
zinahitaji ujenzi akitolea mfano wa huduma ya Afya kwa kusema ili maendeleo
katika sekta hiyo yapatikane ni lazima kuwepo na majengo kwa ajili ya huduma
hiyo.
“Wakadiriaji wa Majenzi wakitumika vizuri kutapunguza sana mianya ya
rushwa kwa kuwa kabla ya hatua ya kumpata mkandarasi tayari utakuwa umeshajua
gharama halisi ya ujenzi husika.”
Utalaamu wa Ukadiriaji Majenzi unaweka uwazi katika mchakato mzima
katika shughuli za miradi ya ujenzi.
|
No comments:
Post a Comment