SERIKALI imempongeza Mwandishi wa Kamusi ya Ukristo Padre
Jordan Nyenyembe pamoja na wadau wengine waliohusika katika kufanikisha
uandishi wa Kamusi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni katika Wizara ya Habari Utamaduni
Sanaa na Michezo, Bibi. Lily Beleko ambaye alimwakilisha mgeni rasmi Mhe.
Waziri Nape Nnauye wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kamusi hiyo.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Mhe. Waziri Nape Nnauye, Bibi.
Beleko amesema kwamba Padre Jordan Nyenyembe anapongezwa kwa uandishi wa Kamusi
hiyo kwani kunaonyesha juhudi za kukuza na kuitangaza lugha ya Kiswahili.
Alisema kwamba uandishi wa Kamusi ni kazi ngumu na endapo
maneno ndani ya Kamusi hayatafsiriwi sawa sawa basi kuna uwezekano wa
kusababisha chuki, ghasia na hata mapigano na hasa maneno yanayohusiana na
masuala ya imani ya dini Fulani.
“Ni matumaini yangu kwamba, Kamusi hii itahamasisha na
kurahisisha uelewa wa vitabu na maandiko mbalimbali kwa usahihi na ufasaha kwa
jamii na kuleta upendo, utulivu na amani”, alisema Beleko.
Aliongeza kuwa Wamisionari wa mwanzo wa imani ya kikristo
walisaidia katika usahihishaji na uenezaji wa lugha ya Kiswahili kupitia vitabu
na nyaraka mbalimbali, aidha walishiriki katika kuandika sarufi za Kiswahili,
kamusi za kiswahili na kutafsiri Biblia kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine
hali ambayo ilisaidia kukuza dini ya Ukristo
na kukuza lugha ya Kiswahili.
“Lugha yetu ya Kiswahili kila kukicha inazidi kukua na
kupitia Kamusi hii tunaamini kwamba wasomaji wataongeza maarifa na ufasaha na
kudumisha umoja, amani na uzalendo”, alisema Beleko.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC) Padre Ubadius Kidavuri ambaye aliliwakilisha Baraza hilo
alieleza kwamba, ushirikiano kati ya serikali na taasisi za kidhni ni jhambo
mhimu katika kusukuma maendeleo ya taifa.
“Katika Kanisa la Katoliki Tanzania linaunga mmkono jitihada
zote za Wasomi na Wataalam wote wanaowezesha ujuzi na maarifa mbalimbali kidini
na hata kielimu kuwafikia Wananchi katika kukabiliana na changamoto, hivyo
nachukua nafasi kwa niaba ya Baraza, kumshukuru na kumpongeza Padre Jordan kwa
jitigada zake za kubuni na kufanya kazi hii njema kwa Watanzania”, alisema
Padre Ubadius.
Naye Mwandishi wa Kamusi hiyo, Padre Jordan Nyenyembe alisema
kwamba Kamusi hiyo inakamilisha kazi iliyoanza mwaka 2004 kama Makala katika
Gazeti la Kiongozi iliyoitwa ‘Kiswahili
cha Mwanakanisa’.
Alisema kwamba, wasomaji watakaokuwa wanaitumia Kamusi hiyo
wawe huru kumshirikisha kwa kutoa maoni yao mbalimbali ili aweze kuboresha
katika matoleo yajayo.
“Mtakaoisoma Kamusi hii msisite kutoa maoni yenu ambayo
yataniwezesha kuboresha katika matoleo yajayo”, alisema Padre Jordan.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uchapishaji Vitabu ya
Mkuki na Nyoka, Bw. Walter Bugoya alieleza kwamba, kuandaa kamusi kama hiyo
kunahitaji mtu kufahamu masuala mengi ambayo anatarajia kuyaandika, hivyo
anakuwa na kazi kubwa ambayo inahitaji umakini, kutafuta maana sahihi ya maneno.
“Pia katikia suala la uhalili Mwandishi anahitaji kusaidiwa
na Wahariri ili kazi yake iwe rahisi kwa wasomaji kwa kupata maana sahihi ya
maneno ndani ya kitabu husika”, alisema Bw. Bugoya.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Kiswahili la Taifa
(BAKITA) Dkt. Selemani Sewangi alisema kuwa, suala la lugha kwenye Makanisa ni
muhimu sana kwani litasaidia kukuza uelewa wa mafundisho ya imani ya dini hiyo,
hivyo amepongeza kazi ya uandishi wa Kamusi hiyo.
No comments:
Post a Comment