Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) akiendelea kukagua shughuli za maendeleo za vikundi vya wanawake wajasiriamali wa Kata ya Magoweko Wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro. Kulia ni Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Ahmed Shabiby.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) akiendelea akiangalia moja ya mashine ya kufyatua matofali wakati wa ziara yake ya kukagua
shughuli za maendeleo za vikundi vya wanawake wajasiliamali wa Kata ya Magoweko Wilayani Gairo, Morogoro. Kulia ni Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Ahmed Shabiby.
Na Mwandishi –Wetu –Gairo Morogoro. WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.)
leo amefanya ziara katika Wilaya ya Gairo, Mkoa wa Morogoro kwa kukagua
shughuli za vikundi vya wanawake wajasiriamali wa Kata ya Magoweko.
Akihutubia wanawake na wananchi walio jitokeza katika maonyesho ya shughuli
hizo, Mhe Ummy alieleza kuwa Serikali imejipanga katika kumuwezesha mwanamke
kiuchumi.
Alisema,
uwezeshaji huo utafanyika kupitia mifuko mbalimbali ya kuwawezesha wanawake,
ikiwamo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) uliopo katika kila Halmashauri
nchini na Benki ya Wanawake Tanzania.
Katika
hadhara hiyo Mhe Ummy alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo,
Bibi Agness Martin Mkandya, kuhakikisha Halmashauri hiyo inatenga asilimia 5 ya
mapato yake ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ili
fedha hizo ziweze kutumika katika kukopesha wanawake wajasiliamali.
Aidha, aliwaeleza wananchi kuwa serikali itatekeleza ahadi yake ya Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-20 kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa
kila Kijiji kama Mfuko wa Mzunguko (Revolving Fund) kwa ajili ya kukopesha
vikundi vya wajasiriamali kupitia Ushirika wa Kuweka na Kukopa (SACCOS) katika
vijiji husika; hivyo wanawake nao wazichangamkie fedha hizo kwa kuanza
kujiandaa kujiunga katika vikundi ili fursa hiyo isiwapite.
Katika kukabiliana na changamoto ya masoko kwa bidhaa zinazotengenezwa na
wanawake, Mhe Ummy alisema, Ilani ya uchaguzi ya ccm pia inaelekeza Halmashauri
zote kutenga asilimia 30 ya thamani ya manunuzi yake kwa ajili ya bidhaa
zinazotengenezwa na vikundi vya vijana au wanawake. Aidha, mbunge wa Jimbo la
Gairo, Mhe. Ahmed Shabiby aliwaeleza wananchi kuwa wataandaa utaratibu wa kuwa na
maonyesho rasmi ya kutangaza kazi za wanawake wajasiliamali wa Wilaya hiyo.
Baadhi ya Wanawake walioshiriki katika shughuli hiyo walieleza kuwa kupitia shughuli
za vikundi wameweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato
ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vijana kujiunga na vikundi hivyo, wakilenga pia
kuwaelimisha vijana kuacha matumizi ya madawa ya kulevya. Aidha, wanawake hao
waliainisha moja ya changamoto kubwa inayo wakabili kuwa ni ukosefu wa mtaji wa
kutosha kuendesha biashara zao.
Kupitia hadhara hiyo Mhe Ummy aliwataka wazazi kutilia mkazo elimu kwa watoto
wa kike. Alieleza kuwa Wilaya ya Gairo inakabiliwa na tatizo kubwa la mimba na
ndoa za utotoni, tatizo ambalo kwa kiasi kikubwa linafifisha jitihada za
serikali katika kumpatia mtoto wa kike Elimu.
No comments:
Post a Comment