Pages

Wednesday, June 29, 2016

VIWANDA VISIVYOENDELEZWA KURUDISHWA KWA WATANZANIA

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
29/06/2016
VIWANDA vilivyobinafsishwa na Serikali ambavyo haviendelezwi kutwaliwa ili kutolewa kwa wawekezaji wenye uwezo wa kuviendesha. 

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa juu ya mwekezaji wa kiwanda cha nyuzi Tabora kwa kushindwa kuendeleza kiwanda hicho.

“Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa na Serikali kikiwemo kiwanda cha nyuzi cha Tabora ili kujiridhisha kama wawekezaji wa viwanda hivyo wanatimiza matakwa ya mkataba na Serikali,” alifafanua Mhe. Mwijage.

Aliendelea kwa kusema kuwa, ikiwa viwanda hivyo vitabainika kubadilishwa matumizi yake au kutoendelezwa basi Serikali itavirudisha kwa watanzani ili viweze kuendelezwa.

Aidha Mhe. Mwijage amesema kuwa, kwa sasa mwitikio wa kuviendeleza viwanda ambavyo vilikuwa havizalishi ni mzuri kwani viwanda vingi vimeanza kufanya kazi lakini kwa wale ambao watashindwa kabisa  kuviendeleza basi viwanda hivyo vitarejeshwa kwa watanzania.

Vile vile Mhe. Mwijage amesema kuwa dhana ya Serikali ya awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda inaenda pamoja na kurejesha Serikalini viwanda vyote vilivyobinafsishwa lakini haviendelezwi ili vitolewe kwa wawekezaji wengine. 

Sambamba na hayo Mhe. Mwijage amesema kuwa kufufua viwanda, hasa viwanda vya nguo ni pamoja na wakulima wa pamba kulima zao hilo kwa wingi kwa ajili ya uchakataji pamoja na kudhoofisha uingizaji wa nguo za mitumba nchini.

Wizara hiyo inaendelea na kushawishi wawekezaji mbalimbali ili kujenga viwanda vingi iwezekavyo kwa ajili ya uchakataji wa mazao yanayolimwa nchini pamoja na mifugo.

BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA  YA MWAKA 2016

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju

Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
29/06/2016
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2016 wenye lengo la kupunguza gharama na muda wa mchakato wa manunuzi Serikalini.

Marekebisho hayo yametokana na gharama kubwa ambayo Serikali imekuwa ikitumia kutokana na huduma na Bidhaa zinazonunuliwa na Serikali kuwa za juu ikilinganishwa na bei ya wastani ya soko.

“Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma wa mwaka 2016 una lengo la kuongeza ufanisi katika ununuzi wa Umma kwa kuondoa mapungufu yaliyopo katika Sheria ya sasa kwa kupunguza gharama na muda wa michakato ya ununuzi, kutoa upendeleo kwa kampuni za ndani, vikundi maalum, malighafi na bidhaa zinazozalishwa nchini pamoja na kuweka viwango mahsusi kwa bidhaa zitakazotumiwa na Serikali,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju.

Mhe. Masaju ameendelea kwa kusema kuwa sheria hiyo imeweka kifungu cha dharura  ili kuwezesha vitu vya kuokoa uhai na vinginevyo kununuliwa kwa dharura pindi inapobidi.

Kwa upande wake Mbunge wa Babati Vijijini Mhe. Jitu Soni yeye ameiomba Serikali kuruhusu kununua vifaa tiba vilivyotumika ambavyo muda wake wa kutumia hauna mwisho, kwa mfano vitanda vya kujifungulia  ili kupunguza gharama ya kununua vitanda vipya na kuweza kununua vitanda vingi kwa wakati mmoja.

Aidha Mhe. Jitu ameiomba Serikali kuirudisha tena Sheria hiyo Bungeni baada ya mwaka mmoja ili kufanyiwa marekebisho na kuziba mianya yote ambayo itakuwa imebainika mara baada ya utekelezaji wake kuanza.

Muswada wa marekebisho ya sheria hiyo yanasubiri kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli ili kuanza utekelezaji wake.

No comments:

Post a Comment