TANGAZO


Saturday, April 9, 2016

Waziri Jenista Mhagama atoa ubani kwa wafiwa maafa ya Kawe

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa ubani kwa Gaudensia Deogratius, aliyefiwa na watoto wawili na mume wake, baada ya kufunikwa na kifusi Kawe Ukwamani juzi Aprili 7, 2016 jijini Dar es Salaam. (Picha Zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa mkono wa pole kwa mama wa marehemu Ephrahim Mangule (aliyefariki kwa kuangukiwa na kifusi Kawe) wakati wa msiba huo Kinondoni jijini Dar es Salaam leo, tarehe 9 Aprili, 2016. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akitoa Salamu za pole kwa wafiwa waliopotelewa na ndugu 3 baada ya mvua zilizonyesha Aprili 7, 2016 na kuangukiwa na nyumba Kawe jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Raymond Mushi.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Raymond Mushi akizungumza na moja ya familia ya wafiwa walioangukiwa na kifusi Kawe Dar es Salaam wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alipowatembelea leo, tarehe 9, Aprili, 2016. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiangalia chumba kilichoangukiwa na kifusi baada ya mvua kubwa zilizonyesha Aprili 7, 2016 na kuua watu 5 wa familia moja Kawe jijini Dar es Salaam. 

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Uratibu,Ajira,kazi na watu wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama amewatembelea wananchi waliopatwa na majanga ya kuangukiwa na kifusi eneo la Kawe na kuwapa mkono wa pole.

Akiongea na moja ya familia zilizopatwa na maafa hayo Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya tukio hilo na kwa vifo vilivyojitokeza na kuahidi kutoa ushirikiano kwa familia ya wafiwa na waathirika wa tukio hilo.

“Ndugu zangu tumekuja kushirikiana nayi kwenye msiba huu mzito, ambao wenzetu wamepoteza karibu familia nzima kutokana na haya maafa, poleni sana kwa msiba na Serikali ipo pamoja nayi katika kipindi hiki kigumu.” Alisema Mhe Jenista. 
 `
Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati Serikali inapokuja kwa ajili ya kujadili jinsi ya kutatua mambo yanayowezesha kuhatarisha maisha yao hasa, tatizo la makazi yaliyopo mabondeni kwa ajili ya usalama wao na familia zao katika kuzingatia suala la mipango miji ili kuepukana na majanga kama haya.

Aidha kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Raymond Mushi amesema kwa upande wake amesikitishwa na tukio hilo na kuongeza kuwa Wilaya imejipanga kwa kushirikiana na kamati ya maafa ya Wilaya na Idara ya  Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuendelea kuangalia ni kwa namna gani wataweza kuwasaidia wananchi waliobaki katika maeneo hayo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya familia ya wafiwa Bi Gaudencia Deogratius ambaye amepoteza mume na watoto wawili ameishukuru Serikali kwa faraja aliyopata kutoka kwa Waziri na hakutegemea kupata ugeni huo na ameiomba Serikali kuwasaidia wale waliopo mabondeni ili kuepusha majanga mengine zaidi kutokea.

Tukio la hili la nyumba kuangiwa na kifusi katika eneo la kawe Jijini Dar es Salaam lilitokea April 7 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watano wa familia moja.

No comments:

Post a Comment