Naibu Waziri Ofisi ya Wazikri Mkuu (watu wenye Ulemavu) Mhe. Dkt. Abdallah Possi (kulia), akifuatilia uwasilishwaji wa takwimu za Watu wenye Ulemavu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk.Albina Chuwa wakati wa Uzinduzi wa kanzi data hiyo Aprili 11, 2016 Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa wasioona Bw. Luis Benedicto akichangia hoja wakati wa Uzinduzi wa Kanzidata ya watu wenye ulemavu katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 11, 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk.Albina Chuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu Kanzidata mara baada ya uzinduzi wa kanzidata hiyo ya watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Aprili 11 2016.
Na Raymond Mushumbusi, Maelez
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Dkt. Abdallah Possi amezindua rasmi kanzidata ya watu wenye ulemavu, ambayo itasaidia katika upatikanaji wa taarifa zinazohusiana na watu wenye ulemavu nchini na kuwawezesha wadau wengine katika kuboresha sera na programu zinazolenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu nchini.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa kanzidata hiyo Katika Ofisi ya Waziri Mkuu leo Jijini Dar es Salaam, Dkt Abdallah Possi amesema kanzi data hiyo itakayotumika kutoa takwimu ya watu wenye ulemavu nchini iwe ni fursa ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa, kujikwamua kiuchumi na kuondokana na unyanyapa unaofanywa na baadhi ya watu.
“Ni matarajio yangu kwamba kanzidata hii itasaidia mambo kadhaa muhimu, kubwa zaidi ni upatikanaji wa taarifa katika mfumo rafiki utakaosaidia watumiaji kufanya uchambuzi wa kina zaidi kulingana na mahitaji yao yatakayosaidia kuleta uelewa kwa watu kuhusu ulemavu kwa ujumla na umuhimu wa kuhusisha mahitaji ya watu wenye ulemavu kwa ajili ya maendeleo endelevu” alisema Dkt. Possi.
Aidha Mkurugenzi wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa wajibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa ni kutunza na kutoa kumbukumbu kwa ajili ya makundi mbalimbali na katika kufanikisha hilo ameomba ushirikiano kutoka chama cha watu wenye ulemavu na mashirikisho yake ili kuboresha kanzidata hii ya watu wenye ulemavu.
Dkt. Chuwa alisisitiza kuwa, ili kanzidata hii iweze kufanya kazi kwa urahisi inahitaji ushirikiano kutoka Sekta binafsi ili kuwezesha kukamilisha andiko lililoko katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kanzidata na kwa kuanzia kanzidata hiyo imeanza kwa majaribio katika Wilaya ya Bagamoyo.
Kanzidata hii imetayarishwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa na dhumuni la kurahisisha upatikanaji wa taarifa kwa urahisi na ufuatilia wa takwimu ya masuala ya Watu wenye Ulemavu.
No comments:
Post a Comment