Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye semina yao, iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaa.
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO, Dodoma
WATANZANIA wameaswa
kujenga tabia ya kujiwekea akiba kupitia mabenki kwa manufaa yao na taifa kwa
kwa ujumla ikiwa ni mchango wao katika kutekeleza kaulimbiu ya Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ili kufikia malengo
waliojiwekea katika kujiletea maendeleo endelevu.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Fedha na Utawala kutoka Bodi ya
Bima na Amana (DIB) iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Richard Malisa wakati
akitoa mada juu ya bodi hiyo katika semina ya waandishi wa habari iliyoandaliwa
na benki hiyo kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi hao katika kuandika, kutoa
na kusambaza habari za sekta ya uchumi biashara na fedha.
“Pesa zinapowekwa na kuwa benki hutumika kuchangia kuinua na
kuimarisha usalama wa akiba ya mtu binafsi na kwa upande wa nchi zinatumika
katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuinua sekta ya elimu, afya,
maji, ujenzi wa barabara na kilimo”
alisema Malisa.
Katika kuonesha umuhimu wa bodi hiyo nchini, Malisa alisema
kuwa taasisi ama mtu binafsi anapoweka pesa zake benki, hiyo ni amana kubwa na
muhimu kwa kuwa tabia hiyo ya uwekaji pesa ina tija na inaongeza usalama wa
pesa ambayo ni njia salama ikilinganishwa na kutumia njia za zamani za watu kuweka
pesa kwenye godoro ambayo sio salama.
Faida nyingine za mtu binafsi ama taasisi kuweka pesa zao
benki ni kuongeza mtaji wake kwa kupata riba kulingana na muda pesa hizo zinapokuwa
benki na mteja anauhakika pesa yake ipo salama kwa kuwa ipo mikononi mwa Bodi
ya Bima na Amana endapo litatokea tatizo lolote kwenye benki alipoweka pesa
zake.
Katika kufanikisha na kutekeleza majukumu yake, DIB inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa mtu mmoja mmoja katika masuala
ya kibenki na fedha kwa undani wake ili aweze kufanya maamuzi yatakayomfanya
awe bora zaidi kiuchumi ikilinganishwa na hapo awali kabla ya kufahamu masuala
ya kibenki na fedha ikiwemo kuongeza nidhamu ya matumizi.
Akitolea mfano Malisa amewaasa Watanzania wawe makini
wanapochukua mikopo ambapo alisema kuwa watu wasikope kwa kufuata mkumbo ama
kwa shinikizo fulani, bali wakepo kwa lengo la kuwekeza ili kuinua hali zao za kiuchumi
katika maisha.
Hadi kufikia Juni 30, 2015 Bodi ya Bima na Amana ina akiba
ya jumla ya kiasi cha Sh. biloni 220.5 ikilinganishwa na wakati ilipokuwa inaanzishwa
na Serikali mwaka 1994 ambapo kianzio kilikuwa kiasi cha Sh. bilioni 1.5.
Aidha, katika semina hiyo Bw. Bernard Dadi kutoka Kurugenzi
ya Mifumo ya Malipo ya Taifa alisema kuwa BoT itaendelea kuboresha mifumo ya malipo
ya hundi, kielektroniki ili kuongeza ufanisi kwenye mifumo hiyo, kuongeza
usalama, kuongeza njia mbalimbali za malipo ili kupunguza malipo kwa fedha
taslimu na kuongeza kasi ya malipo yaweze kuwa ya wakati kwa wateja popote
walipo ndani na nje ya nchi.
Ili kuendana na wakati BoT kupitia Kurugenzi ya Mifumo ya
Malipo ya Taifa katika kuwahudumia wananchi katika masuala ya fedha na mabenki,
imeanza kutumia mfumo
wa TACH unaohusisha malipo ya hundi na malipo madogo ya kielektroniki (EFT) ambao
umeanza kutumika tarehe 30 Aprili 2015 nchini.
Mfumo wa TACH unatumika na mabenki kutuma na kupokea hundi
za wateja wao ikiwemo kulipa malipo madogo madogo yaliyojumishwa pamoja, mishahara,
pension na hata malipo ya mtu mmoja mmoja.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa TACH nchini, awali hundi
zilikua na muda tofauti wa siku za
kuhakiki kulingana na kanda hali
iliyopelekea muda wa siku za kuhakiki za
hundi ulikua ni siku 3, 7 na 14 kutegemeana na kanda.
Baada ya kuanzishwa mfumo wa TACH hali imekuwa tofauti
ambapo kwa mfumo huo sasa, hundi zote za
Tanzania popote zitakapowasilishwa zitakuwa zinafanyiwa kazi ndani ya siku moja
ya kuzihakiki hundi hizo (T+1) mpaka
hapo itakapolipwa.
Hatua hiyo imewapunguzia muda wateja ili waweze watapata
hela zao mapema na hivyo kuzitumia kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, Bw. Dadi aliongeza kuwa nchi
washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zenyewe zinatumia unaojulikana kama EAPS ikiwa ni jitihada za kuunda
umoja wa kiuchumi miongoni mwa nchi
hizo.
Mfumo huo wa malipo umeunganisha mifumo ya malipo (RTGS) ya
nchi washiriki wa Afrika Mashariki ili kurahisisha malipo kati ya nchi
washirika.
Kwa maana hiyo mabenki ya kibiashara ya nchi husika zina
uwezo wa kutumiana na kupokea pesa za wateja wao kwa kutumia sarafu za nchi wanachama kufanya
muamala.
Hadi sasa, mfumo huo umeunganishwa kwa Tanzania, Kenya,
Uganda, Rwanda, wakati Burundi na Sudan ya Kusini wako mbioni kujiunga.


No comments:
Post a Comment