TANGAZO


Friday, January 8, 2016

Tanzania ina vyanzo vingi vya umeme-Profesa Muhongo

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiongoza kikao kilichoshirikisha watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen. Balozi huyo alifika wizarani hapo kujadili fursa za uwekezaji zilizopo nchini. 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia), akizungumza jambo wakati wa mkutano wake na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen (katikati), ofisini kwake jijini. 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) katika picha ya pamoja na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen (wa pili kushoto) pamoja na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk. Mhandisi Juliana Pallangyo (kulia) akifuatiwa na Profesa James Mdoe.  
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akipeana mkono na na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kujadili fursa za uwekezaji nchini.

Na Mohamed Seif, Ofisa Mwasiliani
Nishati na Madini
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalishia nishati ya umeme na hivyo kutoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye miradi ya kuzalisha umeme.

Aliyasema hayo jana Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es salaam, alipokutana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Einar Jensen ambaye alifika wizarani hapo kujadili fursa za uwekezaji.

“Wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza kwenye miradi ya kuzalisha umeme nchini kwani fursa ni nyingi na zinahitaji wawekezaji makini,” alisema Prof. Muhongo

Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vyanzo mbalimbali vya kuzalishia umeme ambavyo alivitaja kuwa ni gesi asilia, makaa ya mawe, maporomoko ya maji, jua, upepo, jotoardhi na mawimbi ya bahari.

Alisema lengo ni kuhakikisha kwamba baada ya miaka kumi ijayo Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha. “Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025, umeme unaongezeka hadi kufikia megawati 10, 000,” alisema.

Balozi Jensen alisema zipo kampuni nyingi Nchini Denmark ambazo zinao uwezo na uzoefu wa kutosha kwenye masuala ya uzalishaji umeme.

Alisema tayari kuna kampuni za Denmark ambazo zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye umeme wa upepo na hivyo alisema kinachohitajika ni taarifa zaidi kuhusiana na uwekezaji wa aina hiyo.

Mbali na hilo, Balozi huyo alisema lengo jingine la kutembelea wizarani hapo ni kujenga na kuendeleza mahusiano na Serikali na vilevile alimuhakikishia Waziri Muhongo kuwa atazungumza na kampuni nyingine kwa ajili ya kuwekeza nchini.

“Nitakuja na ujumbe kutoka Denmark ambao utafika hapa kwa ajili ya kujionea na kutambua fursa za uwekezaji zilizopo nchini hapa,” alisema Balozi Jensen.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo, Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (Madini) na Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (Nishati) walimuhakikishia Balozi huyo ushirikiano wa kutosha na vilevile walisema wanasubiri ujio wa kampuni hizo kutoka nchini Denmark ambazo zitakuwa tayari kuwekeza nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na watendaji wa wizara ya ya Nishati na Madini, Wawakilishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

No comments:

Post a Comment