TANGAZO


Saturday, December 5, 2015

Watendaji wa Tamisemi watakiwa kusimamia Sheria kuhusu Usafi, Ujenzi holela, Wafanyabiashara maeno ya DART

Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakimsilikiza  Katibu Mkuu wa ofisi ambaye hayupo pichani. (Picha zote na Magreth Kinabo-Maelezo) 
Baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakimsilikiza  Katibu Mkuu wa ofisi ambaye hayupo pichani.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Jumanne Sagini  wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa ofisi hiyo leo  katika mkutano wa kikazi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dares Salaam , ambapo lengo kuu lilikuwa ni kutoa maelekezo ya utendaji kazi kama ilivyoagizwa na  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.Kulia ni  Naibu Katibu Mkuu Afya -Tamisemi, Dkt. Deo Mutasiwa.

Na Magreth Kinabo – maelezo
4/10/2015
SERIKALI  imewataka  watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha kwamba wanafanyakazi kwa uadilifu weledi wa taaluma zao na kufuata sheria zilizopo  katika kusimimia suala la usafi wa mazingira, likiwemo la kudhibiti biashara holela, gereji bubu, uegeshaji wa magari holela.

Pamoja na hayo wasimamie, upigaji holela wa muziki katika vilabu, baa  na kumbi  zaidi  ya saa zilizopangwa na kuzuia bodaboda  zinazosafirisha abiria hadi maeneo  ya miji katikati, pia kuzuia ujenzi holela.

Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne  Sagini  wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa ofisi hiyo  katika mkutano wa kikazi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Karimjee, jijini Dar es Salaam ambapo lengo kuu lilikuwa ni kutoa maelekezo ya utendaji kazi kama ilivyoagizwa na  Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu suala la usafi wa mazingira kufuatia  ziara iliyofanyika hivi karibuni imeonekana kuwa na changamoto mbalimbali  alisema;
“Kazi zetu  haziendi vizuri  kwa sababu hatusimamii  sheria zilizopo ndio kumekuwa na malalamiko katika utendaji wa kazi zetu, mfano katika suala la  gharama za usimamizi wa usafi wa mazingira ni kubwa . Lakini kinachofanyika ni kweli  kinalinganishwa na gharama hizi?” alihoji  Katibu Mkuu huyo.

Akitolea mifano  gharama zinazotumika  katika suala hilo, kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2014/2015  alisema kwa upande wa manispaa ya Kindondoni wanatumia Sh. bilioni 2.6, Ilala  ni Sh. bilioni 2.6, wakati Temeke wanatumia Sh. bilioni 1.2.

“Kilichobainika  ni kwamba  mikataba ya watu wanaojishughulisha na  usimamizi wa usafi wa mazingira ni ya mwaka mmoja na wanaopewa  mikataba hiyo ni watu ambao hawana uwezo wa kutosha wa kutekeleza jukumu hilo.

“Ama  watu wasio na uwezo ama mnaofahamiana nao.  Au kampuni zenye mahusiano na baadhi ya watumishi wa mamlaka za serikali za mitaa au wenye uhusiano  na viongozi wenu, Jiepusheni  na kuwapa watu hawa kwa sababu  kutokana na hali hiyo hamtaweza kukabiliana  nao. Kama   kuna kiongozi ambaye mmempatia nafasi hii  lazima athibitishe kuwa na uwezo. Na kama pia ni miongoni mwenu hakikisheni kuwa ni mtu mwenye uwezo. Kazi zetu haziendi vizuri kwa sababu ya nasaba au viongozi wenu,” alisisitiza  Katibu Mkuu huyo, huku akisema lazima  wabadilike na kuangalia kama hawana uwezo wajitoe au wafukuzwe.

 Aliongeza kwamba katika suala hilo kumekuwa na migongano  ya watumishi  wa halmashauri ambao wanatakiwa kufanya kazi kama timu; mfano Maofisa Afya, mazingira na usafishaji, lakini akasema wanaonana kama maadui.

“ Hawa  wangepaswa kufanya kazi kwa kushirikiana lakini ni maadui kwa sababu ya maslahi … hili ni lenu wakurugenzi  kwani hata watoto wako wakisambaratika ni lazima uwaketishe chini ili mambo yaende,  asiyekubali unamwajibisha,” alisema.

Sagini alisema watendaji hao , wote ni wadau wa usafi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, hivyo aliwataka wapeane  mikono katika kikao hicho, ambapo walifanya hivyo ikiwa ni hatua ya kuonesha ushirikiano.

Pia alisema watu wanaosafirisha  bidhaa za vyakula kwa kutumia  majani ya migomba au matenga wasiruhusiwe kufanya hivyo wapewa muda wa wiki moja au mbili kutumia utaratibu mwingine.

 Aliwataka pia watendaji mbalimbali wa TAMISEMI kuwa na ushirikishwaji katika ngazi za chini kwenye halmashauri kwa kuwa haliko vizuri.
 Sagini alisema ni vizuri kukawekwa mfumo wa TAMISEMI  wa  kushirikisha ngazi za chini kama ilivyo kwa mjumbe wa nyumba kumi kwenye masuala ya vyama.

“Ni lazima tuingie katika mfumo huu wa  kuwa na watendaji  wa kaya 30  ambao watakuwa chini ya TAMISEMI . Suala hili lina faida  ya ulinzi na  usalama  na kuwatambua wageni… tunaangalia jinsi ya kulitekeleza,” alisema.

Aliwataka wakurugenzi wasikae maofisini kwenye madawati bali watembelee maeneo mbalimbali  ili kutatua kero za wananchi na kuangalia mipangilio ya miji na majiji.

Katika suala hilo la usafi wa mazingira alisema mtu mwenye uwezo wa kusafisha jiji liwe safi apewe nafasi huku akisisitiza suala la kushirikisha sekta binafsi ni muhimu katika mambo mbalimbali likiwemo la ujengaji wa maegesho ya magari, ambapo sasa  yanahitajika kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka(DART).

“ Kwenye  eneo hili la DART lazima  mbadilike tunataka barabara za DART ziwe nyeupe yaani watu wasifanye biashara,” alisisitiza huku akitaka kuanzia Jumatatu wiki ijayo yatekelezwe.

Aliwataka watu wanaohusika  na vyombo vya usafiri na usafirishaji kutovunja sheria, akatolea mfano boda boda.

No comments:

Post a Comment