Msimamizi wa mradi wa kompyuta shuleni wa Shirika lisilo la kiserikali la Learning In sync, Lisa Walker (kushoto) akiwaelekeza jinsi ya kutumia kompyuta, Mary Lyimo na Faraja John ambao niwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Shimbwe iliyopo kata ya Uru Wilaya ya Moshi vijijini, wakati walipokuwa wakiunganishiwa mfumo wa teknolojia ya kisasa kwenye kompyuta zao zilizotolewa msaada na Vodacom Foundation ikiwa ni jitihada za mfuko huo kwa wanafunzi wa shule hiyo kuweza kupata mafunzo ya masomo mbalimbali kupitia kompyuta.
Lisa Walker ambaye ni msimamizi wa mradi wa kompyuta shuleni wa Shirika lisilo la kiserikali la Learning In sync, akiwafundisha wanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Shimbwe iliyopo kata ya Uru Wilaya ya Moshi vijijini, wakati walipokuwa wakiunganishiwa mfumo wa teknolojia ya kisasa kwenye kompyuta zao zilizotolewa msaada na Vodacom Foundation ikiwa ni jitihada za mfuko huo kwa wanafunzi wa shule hiyo kuweza kupata mafunzo ya masomo mbalimbali kupitia kompyuta.
Na Mwandishi wetu, Moshi.
WANAFUNZI wa shule mbalimbali za sekondari zilizoko vijijini wameanza kunufaika na somo la Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta (ICT ) hii inatoka na msaada wa Kompyuta kutolewa na mfuko wa kusaidia jamii wa Vodacom Foundation ili kusaida wanafunzi wanaohitimu elimu yao kuendana na soko la ajira kama ilivyo kwa wanafunzi wanaomaliza masomo yao kwa shule za mijini.
Mbali na msaada wa kompyuta ,Vodacom kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Learning In sync, Tanzania wameweka Programu maalumu katika kompyuta hizo ili kurahisisha wanafunzi kuweza kujifunza kwa urahisi pamoja na upatikanaji wa vitabu vya masomo mbalimbali.
Mkuu wa Vodacom Tanzania Kanda ya Kaskazini, Henry Tzamburakis aliyasema hayo jana wakati wa mafunzo ya matumizi ya Programu hizo yanayotolewa na Shirika la Learning In sync kwa walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari, Shimbwe iliyopo kata ya Uru Shimbwe wilaya ya Moshi vijijini.
“Nia ya kuja hapa kijijini, tunajaribu kuangalia shule zenye wanafunzi ambao hawana uwezo wa kupata material ya kujifunzia kwa njia rahisi,tukiangalia wanafunzi wa mjini kidogo wana unafuu lakini vijijini wako nje ya mji hata zile facilities zinakuwa ni shida kidogo,”alisema Tzamburakis.
Alisema Vodacom imeamua kupeleka somo la Teknolojia ya Mawasiliano ya Kompyuta (ICT ) vijijini ili wanafunzi wanao maliza masomo yao waweze kuwa sawa na wanafunzi wanaohitimu katika shule za mijini.
“Kwa ujumla somo la ICT kwa sasa tunalielekeza vijijini ili ile dhana ya dunia kuwa kijiji itimie ,tayari tumetoa Kompyuta 30 kwa shule hii ya sekondari ya Shimbwe ingawaje bado hatujawa na uwezo wa kufikia idadi kubwa ya wanafunzi,” alisema Tzamburakis.
Tzamburaki aliziomba taasisi mbalimbali na watu binafsi kuungana na Kampuni ya Vodacom katika kuinua kiwango cha elimu ya kisasa na kuweza kutoa msaada wa kompyuta katika shule hizo ili vijana waweze kuendana na dunia ya sasa kama ilivyo kwa nchi nyinginezo zinazotuzunguka.
Naye Mkurugenzi mkuu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Learning In sync Tanzania ,Lisa Warker alisema shirika lake limekuwa likifanya shughuli za kuongeza ujuzi kwa walimu na wanafunzi juu ya masuala ya matumizi ya Kompyuta pamoja na kujifunzia.
“Kwa sasa katika darasa hili la Kompyuta katika shule ya Shimbwe ,tumejaribu kuweka Programu maalumu ya kujifunza matumizi ya Kompyuta kwa walimu pamoja na kujifunzia kwa upande wa wanafunzi lakini pia tunasaidia katika masuala ya uongozi”alisema Wolker.
Alisema Programu zilizowekwa katika Kompyuta hizo kwa sasa zitasaidia kupunguza changamoto ya vitabu inayozikabali shule nyingi nchini kutokana na kwamba ina uwezo kusaidia uapatikanaji wa aina zote za vitabu kwa njia ya picha na Video.
Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo,Jacob Constantine alisema matarajio makubwa sasa baada ya Kompyuta hizo kuwekewa programu maalumu za kufundishia na kuongeza ufaulu kwa wafunzi katika shule hiyo ambao kwa sasa si mzuri.
Alisema shule inaanza mchakato wa kuwasiliana na halmashauri ili kuweza kusaidia upatikanaji wa mwalimu ambaye ni mtaalamu wa kompyuta pamoja na kufanya usajili kwa wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne hapo waweze kufanya mitihani ya Kompyuta hapo mwakani.
Mkuu huyo wa Shule aliishurukuru Vodacom Foundation kwa msaada huo huku akiwasilisha ombi pia la kutaka kuwekwa kwa mnara wa mawasiliano ya simu katika maeneo ya kijiji hicho ili kurahisisha zaidi mawasiliano.
Uwekwaji wa Programu za kujifunzia katika Kompyuta hizo shuleni hapo ni utekelezaji wa ahadi ya Ofisa Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa kampuni hiyo,Georgia Mutagahywa alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment