TANGAZO


Thursday, November 12, 2015

Dk. Yamungu Kayandabila: “Sayansi ni muhimu sana katika kufanikisha malengo ya Agenda 2030”

DSC_1572
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Yamungu Kayandabila akizungumza na wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika mkutano maalum wa siku ya Sayansi Duniani. Kushoto kwake ni Afisa utawala na fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam Novemba 10. 2015. (Picha zote na Andrew Chale, Modewjiblog).

Na Andrew Chale, Modewjiblog
Dar es Salaam-Tanzania. 
TANZANIA kupitia wadau wa Sayansi nchini imedhamilia kupiga hatua zaidi katika kufikia malengo ya Agenda 2030 kwa kuchangamkia fursa za maendeleo katika Sayansi.

Hayo yameelezwa jijini hapa wakati wa wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, walipokutana katika majadala wa Siku ya Sayansi Duniani kwa ajili ya Amani na Maendeleo (World Science Day for Peace and Development).

Akisoma neno, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Yamungu Kayandabila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), katika kukuza Sayansi nchini.

Dkt. Yamungu ameelezea kuwa, nchi yoyote ile ilikuendelea, inategemea Sayansi hivyo kwa Tanzania ni wakati wa kuchangamkia fursa ili kufikia malengo na Agenda 2030.

“Tanzania tuna fursa nyingi na za kutosha. Tuna Nyuklia na hii ni uchumi tosha tutakapofanyia kazi kwa malengo tutafika mbali kwani inahitaji Sayansi ya kina.

Navipongeza vyuo mbalimbali vilivyopo nchini ikiwemo DIT, Nelson Mandela cha Arusha, Chuo cha Sayansi Mbeya na vingine vingi” ameeleza Dk. Yamungu.

Aidha, Dkt. Yamungu ametaka Sayansi kuendana na suala la ulinzi wa chakula na miundombinu mingine ikiwemo suala la maji huku akihimiza wanafunzi kuyapenda na kuyasoma masomo ya Sayansi na suala la umuhimu wa Sayansi na namna inavyoweza kuathiri maisha ya watu kila siku.
DSC_1570
Ofisa Utawala na Fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkuu wa ofisi na Mwakilishi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues akisoma ujumbe maalum wa siku ya Sayansi Duniani wakati wa mkutano huo wa wadau wa Sayansi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sayansi na Teknolojia Prof. Evelyn Mbede amepongeza wadau wa Sayansi na Teknolojia kwa kujimuika katika maadhimisho ya siku hiyo ya Sayansi Duniani ambapo ameelezea kuwa Wizara yake milango ipo wazi kwa wadau wote katika kuhakikisha wanapiga hatua katika kukuza na kuendeleza Sayansi hapa nchini.

Kwa upande wake, Afisa Utawala na Fedha wa UNESCO, Spencer Bokosha ambaye alimwakilisha Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa UNESCO- Tanzania, Bi. Zulmira Rodrigues alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kutilia mkazo suala la Sayansi na Teknolojia na kufanya suala hilo kuwa mtambuka kwa maendeleo ya vizazi vya sasa na baadae.

Akisoma ujumbe maalum kutoka UNESCO, Bw. Bokosha alieleza kuwa kupitia Sayansi na Teknolojia na ubunifu, maendeleo ya Taifa endelevu, uimarishaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa maandalizi kwa ajili ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na madhara yake hivyo Sayansi inahitajika kwa kiwango kikubwa juu ya hilo.

Aidha, ameeleza kuwa, UNESCO imekuwa mstari wa mbele katika kuanzishwa kwa moduli za elimu ya Mazingira katika shule za Sekondari.
DSC_1565
Profesa John Kondoro Mkuu wa Chuo cha Teknolojia cha jijini Dar es Salaam – (DIT) akitoa mada katika mkutano huo wa wadau wa Sayansi wakati wa maadhimisho ya siku ya Sayansi.

Akinukuu ujumbe maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Bi Irina Bokova katika ujumbe alieleza:

“Hii ni siku ya Sayansi Duniani kwa amani na Maendeleo na imekuja miezi miwili baada ya makubaliano ya Agenda 2030 ya maendeleo endelevu.

Hivyo Serikali zote zitambue nguvu ya Sayansi ya kutoa majibu muhimu kwa usimamizi mzuri wa maji kwa ajili ya hifadhi na matumizi endelevu ya bahari, ulinzi wa mazingira na viumbe hai, ilikukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na majanga na kuendeleza uvumbuzi na kuondokana na umasikini na kupunguza tofauti” alieleza katika nukuu hiyo.
DSC_1557
Afisa kutoka UNESCO NAT.COM, Bw. Joel Samuel akitoa mada katika mkutano huo wa wadau siku ya Sayansi Duniani.
DSC_1580
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, akifafanua jambo wakati wa mjadala huo juu ya maendeleo ya Sayansi na Teknolojia nchini katika mkutano uliowakutanisha wadau wa Sayansi katika maadhimisho ya Siku ya Sayansi Duniani.
DSC_1584
Wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa siku ya Sayansi Duniani.

No comments:

Post a Comment