Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Twahir Nzalawahe (katikati) akiwaeleza wakulima kupitia waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hatua za kufuata wakati wa mvua kubwa ili kulinda mazao yasiharibiwe na mvua hizo. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Bw. Richard Kasuga na kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Pembejeo Bw. Shenal Nyoni.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Richard Kasuga akitoa ufafanuzi leo jijini Dar es Salaam kuhusu mgawanyo wa pembejeo za kilimo kwa wakulima nchini kote. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo Bi. Zamaradi Kawawa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Fatma Salum-Maelezo)
Na Georgina Misama -
MAELEZO
WAKULIMA wapatao milioni
moja wameanza kunufaika na usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo ambazo Serikali
inazitolea ruzuku kwa ajili ya wakulima katika mikoa 24 ya Tanzania bara (ukitoa
mkoa wa Dar es Salaam) ili zitumike
kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora kwa mwaka 2015/2016.
Akiongea na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika Bw. Richard Kasuga amesema kwamba pembejeo za kilimo zenye thamani
ya zaidi ya shilingi bilioni 78 zitawanufaisha wakulima wanaojishughulisha na
kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga.
“Usambazaji wa vocha
hizo umeshaanza, Serikali kwa kushirikiana na makampuni 23 ya mbolea na 27 ya
mbegu bora ya mahindi na mpunga yanaendelea kutoa huduma ya usambazaji wa pembejeo katika mikoa
husika” amesema Bw Kasuga.
Bw. Kasuga amesema
kwamba ili kuhakikisha mbolea na pembejeo zinatumika ipasavyo, Serikali inatekeleza
jukumu hilo kwa kugawa majukumu kwa ngazi mbalimbali ikianza na Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika, Kamati ya Taifa ya Uendeshaji wa Utaratibu wa Vocha,
Mikoa, Wilaya, Kata mpaka Vijiji.
Akijibu swali la mwandishi
aliyetaka kujua Serikali inafanya juhudi gani katika kudhibiti ubora wa
pembejeo hizo, Kaimu Mkurugenzi, Mamlaka ya udhibiti wa Ubora wa Mbolea Bw.
Lazaro Kitandu amesema toka kuundwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea
tatizo la ubora limepungua kwa kiasi kikubwa kwani mamlaka hiyo inasimamia
zoezi zima la utengenezwaji na usambazaji wa mbolea na pia wakulima wanapewa
elimu ya matumizi sahihi na namna bora ya kuhifadhi.
Aidha, Serikali imetoa
rai kwa wakulima kutumia ruzuku inayotolewa ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa
kuboresha kilimo, na kuwasihi baadhi ya wakulima wanaouza vocha zao
wasidanganyike kwa kupokea hela na kuuza haki yao.
Serikali ilianzisha
utaratibu wa matumizi ya vocha mwaka 2008/2009 ili kuboresha mfumo wa
usambazaji mbejeo kwa wakulima. Utaratibu huu umesaidia kuongeza uzalishaji wa
mazao ya chakula, hivyo Taifa kufaidika
na kujitosheleza kwa chakula.
No comments:
Post a Comment