Rais wa Senegal Macky Sall amesema hazina ya $1.9bn (£1.2bn) iliyoundwa na mataifa ya Ulaya ni hatua nzuri lakini akasema pesa hizo hazitoshi.
Hazina hiyo ni moja ya hatua zilizoafikiwa kati ya viongozi wa Ulaya na Afrika kukabiliana na tatizo la wahamiaji ambao wamekuwa wakielekea Ulaya.
Viongozi hao wamesema lengo lao ni kukabiliana na mizizi ya tatizo la wahamiaji.
Mkutano huo uliitishwa baada ya wahamiaji 800 kufa maji meli yao ilipozama baharini baada ya kuondoka Libya.
Rais Sall, ambaye kwa sasa anaongoza muungano wa mataifa ya Afrika Magharibi, aliambia wanahabari pembezoni mwa mkutano huo kwamba pesa hizo zilizoahidiwa “hazitoshi bara lote la Afrika”.
Lakini baadaye, akizungumza katika kikao na wanahabari alisema amefurahishwa na hazina hiyo, lakini akasema angependa kuona pesa zaidi zikitolewa.
Rais wa Niger Mahamadou Issoufou alikariri matamshi ya kiongozi huyo wa Senegal na akaongeza kuwa uongozi wa ulimwengu unafaa kufanyiwa mageuzi, na biashara duniani ifanywe kuwa ya haki zaidi.
Rais wa Baraza la EU Donald Tusk amesema mkutano huo uliofanyika Malta umekubalia kuhusu “orodha ndefu ya hatua zitakazotekelezwa kufikia mwisho wa 2016”.
Hazina hiyo inatarajiwa kuendeleza uthabiti na kuchangia kuthibitiwa kwa wahamiaji, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa EU.
Aidha, inalenga kubuni nafasi zaidi za kiuchumi na kuimarisha usalama katika mataifa 23 yanayoshirikishwa ambazo ni pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda na Somalia.
Fedha hizo $1.9bn ni kando na ufadhili wa $20bn ambao tayari EU hutoa kila mwaka kwa Afrika.
UN inasema watu 150,000 kutoka nchi za Afrika kama vile Eritrea, Nigeria na Somalia hufunga safari hatari ya kupitia bahari ya Mediterranean kila mwaka ili kufika Ulaya.
No comments:
Post a Comment