Mabalozi wa mataifa ya kigeni wameonya kuwa huenda mataifa yao yakawapiga marufuku maafisa wa serikali wanaojihusisha na ufisadi kuzuru nchi hizo.
Kupitia taarifa ya pamoja, mabalozi hao kutoka mataifa 11 wameahidi kusaidia katika uchunguzi dhidi ya maafisa wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi.
Aidha, wameahidi kusaidia kutwaa mali na pesa zilizofichwa nje ya nchi na maafisa wafisadi.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya mkutano wa faraghani kati ya mabalozi hao na wakuu wa tume ya maadili na kupambana na rushwa Kenya, EACC.
Mabalozi hao, waliojumuisha balozi wa Marekani Robert Godec na mwenzake wa Uingereza Christian Turner, pia wameitaka serikali kuisaidia tume ya EACC kutekeleza majukumu yake.
Taarifa yao imetokea wakati ambapo visa vya ufisadi serikali vimekuwa vikiripotiwa sana katika vyombo vya habari.
Wakuu wa wizara za serikali zilizotajwa kwenye tuhuma hizo, wakiwemo Waziri wa Usalama Joseph Nkaissery na Waziri wa Mipango Anne Waiguru, wamekanusha tuhuma hizo.
Mabalozi wengine waliohudhuria kikao cha leo ni Jamie Christoff (Canada), Tarja Fernández (Finland), Remi Marechaux (Ufaranca), Jutta Frasch (Ujerumani), Mikio Mori (naibu balozi, Japan), Marielle Geraedts (naibu balozi, Uholanzi), Victor Rønneberg (Norway), Johan Borgstam (Sweden) na Ralf Heckner (Uswisi).
No comments:
Post a Comment