TANGAZO


Thursday, November 12, 2015

Putin aagiza madai ya dawa yachunguzwe

Putin

Image copyrightAFP
Image captionPutin alikutana na waziri wa michezo Urusi Vitaly Mutko mjini Sochi
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameagiza uchunguzi ufanywe kuhusiana na madai kwamba wanariadha nchini humo wamekuwa wakitumia dawa za kusisimua misuli.
Putin alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza tangu tume huru ya shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli duniani (Wada) kutoa ripoti yake Jumatatu.
Alisema anataka kuwepo “ushirikiano” kati ya Urusi na mashirika ya kupambana na matumizi ya dawa hizo haramu.
“Kinyang’anyiro lazima kiwe wazi,” alisema Putin. “Shindano lolote la michezo linaweza tu kuvutia iwapo litakuwa wazi.”
Waziri wa michezo wa Urusi Vitaly Mutko alikuwa awali amesema mfumo wa kukabiliana na dawa za kusisimua misuli Uingereza ni mbaya zaidi hata kushinda wa Urusi.
Wizara ya michezo na utamaduni nchini Uingereza imekanusha madai hayo.
Putin alizungumzia madai yanayohusu Urusi pekee, akisema lazima atakayepatikana na hatia awajibishwe.
Image copyrightAFP
Image captionPutin amemtaka waziri wa michezo kuangazia suala hilo kikamilifu
"Ninamtaka waziri wa michezo na wenzetu wote ambao wanahusika kwa njia moja au nyingine na michezo kuangazia suala hili kikamilifu,” alisema kabla ya kukutana na maafisa wa michezo katika mji wa Sochi kwenye ufuo wa bahari ya Black Sea.
"Ni muhimu kwetu kufanya uchunguzi wetu wa ndani, na ninataka kusisitiza, kutoa ushirikiano wazi wa kitaalamu na mashirika ya kimataifa ya kukabiliana na matumizi ya dawa hizi haramu.”
Lord Coe, rais wa shirikisho la riadha duniani IAAF ameliambia shirikisho la riadha la Urusi kwamba lina hadi Ijumaa kujibu madai yaliyopo kwenye ripoti hiyo ya Wada.
Mwandishi wa ripoti hiyo, Dick Pound, alipendekeza wanariadha wa Urusi wazuiwe kushiriki Michezo ya Olimpiki ya 2016 mjini Rio de Janeiro.
Lakini rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach alisema Jumatano kwamba shirika hilo halina “mamlaka” ya kuchukua hatua kama hizo, na kwamba ni IAAF pekee inayoruhusiwa kufanya hivyo.
Bach alisema IOC haitavumilia hata kidogo matumizi ya dawa za kutitimua misuli, na kwamba wanariadha wa Urusi watakaopatikana na hatia ya kutumia dawa hizo watapokonywa nishani walizoshinda Olimpiki.

No comments:

Post a Comment