New Zealand waliweka historia ya kuwa timu ya kwanza kutetea kombe la dunia la mchezo wa raga walipoinyuka Australia katika fainali iliyoandaliwa huko Uingereza
Try za Nehe Milner-Skudder na Ma'a Nonu ziliwaweka ''All Blacks'' kifua mbele alama 21-3 kufikia mapema katika kipindi cha pili.
Hata hivyo Australia walijikakamua na kufunga try mbili kupitia kwa David Pocock na Tevita Kuridrani .
Mambo yaliendelea kuwa magumu kwa New Zealand katika kipindi cha mwisho lakini Dan Carter akafunga penalti zikiwa zimesalia dakika 15 na kuzika kabisa matumaini ya Australia kunusuru hadi yao.
All Blacks hawakukomea hapo, mchezaji wa akiba Beauden Barrett aligonga msumari wa mwisho katika jeneza la Australia alipotifua kivumbi na kufunga try ya ushindi.
Try hiyo iliwapa All Blacks ushindi mkubwa wa alama 34 -17.
Ushindi wa kihistoria kwani wao ndio timu ya kwanza kutwaa taji hilo mara tatu.
Dan Carter alifunga alama 19 na tayari ametangaza kuwa anastaafu.
Wakati huohuo kijana mmoja shabiki wa All Blacks alipata kumbukumbu ya maisha baada ya kutunukiwa medali ya dhahabu waliotuzwa mabingwa haoa.
Charlie Lines alikimbia na kuingia uwanjani kipenga cha mwisho kilipopulizwa.
Maafisa wa kulinda usalama walimfata na kumwangusha chini.
Hata hivyo mshimshike hiyo ilivutia jicho la mchezaji Sonny Bill Williams aliyekimbia kwenda kumuokoa kijana huyo kutoka mikononi mwa maafisa wa kulinda usalama uwanjani Twickenham.
Alimruhusu kushangilia na timu hiyo anaiyoienzi ya All Blacks kabla hajamtunuku medali yake ya dhahabu.
''kila mmoja wetu hapa amefurahi, bila shaka naye amefurahi kupita kiasi, na kwa juhudi yake na ujasiri wa kuingia uwanjani huku akifahamu fika kuwa alikuwa akijihatarisha ,bila shaka ilinibidi nimtunuku kwa jitihada zake.'' alisema Bill Williams.
No comments:
Post a Comment