Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (katikati) akimsikiliza Meneja wa kampuni ya NCC, Sadeesh John (wa kwanza kushoto) akimpatia taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Electricity V katika kituo cha kupoozea umeme cha Sokoine cha jijini Dar es Salaam mara baada ya Mhandisi Luoga kutembelea kituo hicho.
Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja Mradi wa Electricity V, Mhandisi Florence Gwang’ombe (wa pili kulia) wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kupoozea umeme cha Ilala.
Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Vituo Vipya vya Umeme unaofadhiliwa na JICA, Takayuki Kojima (kulia) akimfafanulia jambo Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga alipofanya ziara katika kituo cha kupoozea umeme cha Ilala.
Mradi wa Electricity V- Ilala: Transfoma mpya iliyofungwa kwenye kituo cha kupooza umeme cha Ilala mara baada ya majaribio ya awali.
Na Mohamed Seif
WAKANDARASI wa
miradi ya kuboresha miundombinu ya umeme kwenye vituo vya kupoozea umeme jijini
Dar es Salaam wametakiwa kuhakikisha wanakamilisha miradi hiyo ndani ya muda
uliopangwa.
Wito huo umetolewa hivi
karibuni na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga wakati wa ziara
yake ya ukaguzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme ujulikanao kwa jina la Electricity
V unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao unahusisha ujenzi
na ukarabati wa vituo vya kupoozea umeme vya Sokoine, Ilala na Njiro.
Aidha, ziara hiyo pia
ilihusisha ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya Ilala na New
City Centre pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya Ilala na Muhimbili ambao
unafadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA)
na vilevile Mradi wa Mfumo wa Kusimamia na Kudhibiti Usambazaji wa Umeme Dar es
Salaam ujulikanao kama Distribution SCADA System uliopo Mikocheni unaofadhiliwa
na Serikali ya Finland.
Mhandisi Luoga alielezea lengo
la ziara hiyo kuwa ni kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi
hiyo ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zinazokabili utekelezaji wa miradi
husika.
Katika taarifa yake ya
utekelezaji wa Mradi wa Electricity V, Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Florence
Gwang’ombe alisema kutokana na sababu mbalimbali huenda mradi huo ukachelewa
kukamilika tofauti na makubaliano ya awali kitendo ambacho kilimkera Mhandisi
Luoga na hivyo kumuagiza Meneja huyo kukaa na wakandarasi wa Mradi na kurejea
makubaliano ya awali.
Mhandisi Florence alisema moja
ya sababu inayopelekea Mradi huo kuwa na kasi ndogo ni wakandarasi kushindwa
kuajiri wafanyakazi wa kutosha.
Mhandisi Luoga aliwaagiza
wakandarasi hao ambao ni kampuni ya National Contracting Company Ltd (NCC) ya
India na ELTEL Group kutoka Finland kuhakikisha wanaajiri wafanyakazi wa
kutosha na pia kuandaa ratiba ya shughuli zinazotakiwa kufanywa ili kuepuka
kuchelewa kukamilika kwa miradi husika.
Aidha, Mhandisi Luoga
aliwaagiza Mameneja Miradi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuhakikisha
kunakuwepo na usimamizi madhubuti wa miradi iliyo chini yao ili kuleta matokeo
yanayotarajiwa.
Alisema lengo la Serikali ni
kuhakikisha taifa linakuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya kukuza uchumi na
hivyo aliwaasa mameneja hao kuhakikisha azma hiyo inatimia.
“Ninawasisitiza muhakikishe
kunakuwepo na ufatiliaji makini wa miradi mnayoisimamia na sio kuwaachia
wakandarasi wafanye kila kitu bila usimamizi wenu,” aliagiza Mhandisi Luoga.
Kwa
upande wake Meneja wa kampuni ya NCC Ltd, Sadeesh John alimuahidi Mhandisi
Luoga kuwa atahakikisha kasi ya utekelezaji inaongezeka na kutimiza maagizo
husika ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
No comments:
Post a Comment