Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) Bw. Lusekelo Mwaseba akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua
semina ya wadau wa bima kuhusu sheria mpya ya kodi ya mwaka 2014 ambayo imeanza
kutumika Julai Mosi mwaka huu. (Picha na Eleuteri Mangi- MAELEZO)
Na Eleuteri Mangi-
MAELEZO
WADAU wa sekta ya Bima
nchini wameaswa kushirikiana na Serikali kutekeleza sheria mpya ya kodi ya
mwaka 2014 ili waweze kutoa huduma kwa jamii yenye tija kwa wakati na kulipa
kodi stahiki.
Kauli hiyo imetolewa na
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Lusekelo Mwaseba leo
jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua semina ya wadau wa bima nchini kuhusu sheria
mpya ya kodi ya mwaka 2014 ambayo imeanza kutumika Julai Mosi mwaka huu.
“Tumekutana nanyi
katika semina hii tukiwa na lengo la kushirikishana ili kuijua na kuitekeleza
kwa sheria hii mpya kwa mnufaa yetu sote kama Serikali na wa wadau wa sekta hii
ya Bima” alisema Lusekelo.
Akifafanua juu ya
malengo ya semina hiyo, Lusekelo amesema kuwa mojawapo ya malengo ni kuwaelimisha
na kuwahamasisha wadau kuingia katika kutekeleza sheria hiyo mpya na
kuwasikiliza wadau hao maoni yao ili kutoa au kupunguza na kutafuta kwa pamoja
njia ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Kwa upande wake Afisa
Mtendaji wa Kampuni ya Bima ya BUMACO Bw. Ramadhan Mongi amesema kuwa sheria
hiyo ni nzuri na inalenga kuimarisha uchumi wa ndani ya nchi ikizingatiwa kuwa
ni kwa mara ya kwanza sekta ya bima inaingia kwenye masuala ya shughuli za
uchumi nchini.
Aidha, sheria hiyo mpya
ya kodi nchini imejumuisha shughuli zinazofanywa na madalali nchini ambapo katika semina hiyo imeundwa kamati
ndogo ya ya wajumbe watatu kutoka jumuiya inayoundwa na wadau wa sekta ya bima
itafanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka TRA ili kupata ufafanuzi wa
masuala mbalimbali yanayoendana na sheria hiyo ya kodi ya mwaka 2014 katika
kuimarisha na kuboresha utoaji huduma na kulipa kodi stahiki kwa maendeleo
endelevu nchini.


No comments:
Post a Comment