Wananchi wakimsikiza Frank Kibiki, alipokuwa maeneo ya Stand Kuu, mjini Iringa.
Na Fredy Mgunda, Iringa
MATOKEO ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Southern Highland Zone Election Research (SHZER), katika jimbo la Iringa mjini umeonyesha kuwa nyota ya Mwanahabari , Frank Kibiki aliyetangaza nia kuwania Ubunge jimbo la Iringa mjini (CCM) inazidi kung’ara baada ya kuongoza huku akichuana vikali na Mbunge wa sasa Mchungaji Peter Msigwa(CDM).
Utafiti huo uliofanywa kwa miezi minne tangu, kuwepo kwa wimbi la watu wengi kutangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo la Iringa mjini, wakiwemo makada lukuki wa CCM unaonyesha kuwa Nyota ya Frank Kibiki inazidi kung’ara kutokana na kuungwa mkono na makundi mengi ya kijamii hasa vijana, wanawake, walemavu na wazee.
Akizungumza na mtandao huu, Mtafiti mkuu wa SHZER, Patson William alisema utafiti huo umefanywa katika kata 14 za jimbo la Iringa mjini huku wagombea vijana wakiwa ndio wanaoongoza kupendwa ikilinganishwa na wagombea wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea.
Kibiki anaongoza kwa asilimia 40.7, Mchungaji Msigwa 20.9, Jesca Msambatavangu 11.7, Dr Yahaya Msigwa 7.6, Fredrick Mwakalebela 2.8, John Kiteve 2.4, Mahamoud Madenge 1.2 na wengine waliobaki wanagawana asilimia 12.7.
Utafiti huo unaonyesha kuwa, kinachomfanya Kibiki kuendelea kung’ara ni siasa zake za kistaarabu, taaluma ya uana habari, uwezo mkubwa wa kujenga na kujibu hoja anazokumbana nazo sambamba na uzoefu katika utendaji wake wakati akiwa Katibu wa UVCCM katika wilaya mbalimbali alizowahi kufanya kazi.
Alisema utafiti huo umefanywa kwa njia ya madodoso ambapo watu 400 walijibu na maswali ya papo kwa papo ambapo watu 1000 waliyajibu.
Alitaja kata zilizohusishwa kuwa ni Makorongoni, Miyomboni/kitanzini, Kihesa, Kwakilosa, Mlandege, Mivingeni, Gangilonga, Kitwiru, Igumbilo, Nduli, Ruaha, Mkwawa, Mtwivila na Isakalilo.
Mambo ya msingi ambayo utafiti huo uliangalia ili kutafuta majibu ni Changamoto za jimbo la Iringa mjini kwa sasa,sifa za Mbunge anayetakiwa kukabiliana na changamoto hizo, mapendekezo ya jina la atakayesimamia vizuri changamoto hizo na mazingira ya siasa za sasa za jimbo la Iringa mjini.
Hata hivyo CCM na Chadema ndiyo vyama pekee vinavyochuana kwa kasi katika jimbo la Iringa mjini, tangu CDM iliponyakua jimbo hilo mwaka 2010.
Hata hivyo utafiti huo unaonyesha kuwa CCM itakuwa na wakati mgumu ikiwa watateua jina la mtu asiyechaguo la wananchi jambo ambalo, litampa Mchungaji Msigwa ushindi usio na jasho.
“Utafiti huu unaonyesha kuwa CCM inanafasi nzuri ya kuchukua jimbo la Iringa mjini ikiwa tu watafuata nini wana Iringa wanasema vinginevyo, nafasi ya Msigwa kuendelea itakuwa kubwa,”anasema
No comments:
Post a Comment