TANGAZO


Thursday, June 4, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Iddi akagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Jamii Kijiji cha Kiwengwa Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Jamii katika Kijiji cha Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kushoto kwa Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo, Bw. Tahir Ali na kulia kwa Balozi Seif Iddi  ni mkewe, Mama Asha Suleiman Iddi, ambapo nyuma yao ni jengo la vyoo lililojengwa kwa kutumia chupa za maji zilizotiwa mchanga. 
Balozi Seif Ali Iddi (kulia), akimpongeza Meneja wa Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka nchini Marekani Bw. Josh Winter kutokana na Taasisi yake kusaidia maendeleo ya Elimu Zanzibar. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/6/2015.
Maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Jamii katika kijiji cha Kiwengwa Kiliomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini “ B “ yanaendelea vyema katika hatua za mwisho zitakazoiwezesha skuli hiyo kuanza kuchukuwa wanafunzi wa Elimu ya maandalizi kuanzia mwezi Januari Mwaka ujao wa 2016.

Ujenzi wa skuli hiyo uliohusisha pia vyoo na Tangi la Kuhifadhia maji ambavyo vinajengwa kwa kutumia Taaluma ya Chupa za Maji  zilizotiwa mchanga unafadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Nchini Marekani.

Makundi ya Wanafunzi wa Vyuo na Skuli mbali mbali za Sekondari Kutoka Nchini Marekani kwa kushirikiana na Wanakijiji  wa Kiwengwa wamekuwa wakipiga kambi wakiendelea na kazi mbali mbali za kujitolea katika ujenzi huo wa aina yake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Bwana Tahir Ali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyepeta fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo kwamba Kamati hiyo kwa kushirikiana na Wananchi kupitia ushauri wa Wizara husika ya Elimu wanatarajia kuanza usomeshaji mapema mwakani kwa hatua ya watoto wa maandalizi.

Bwana Tahir alisema juhudi za Wanakijiji kwa kuungwa Mkono na Shirika la Kimataifa la Give la Marekani zimelenga kuwakomboa Watoto wa Kijiji hicho ambao kwa muda mrefvu walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu.

Naye Meneja Mpya wa Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Marekani Bwana Joshi Winter alisema Uongozi wa Mradi huo umejipanga vyema katika kuhakikisha ujenzi wa Skuli hiyo unakamilika vizuri na kutoa fursa kwa watoto wa Kijiji hicho kupata Elimu.

Bwana Josh alisema hatua zimeandaliwa vizuri katika kuyapatia madeshi madarasa ya skuli hiyo, Huduma za Maktaba sambamba na Kompyuta zitakazowawezesha wanafunzi watakaoingia katika skuli hiyo wanapata taaluma yenye mfumo wa  kisasa wa mawasiliano ya Sayansi na Teknolojia.

Meneja wa Mradi huo wa Give ameuomba Uongozi wa Kijiji hicho kwa kushirikiana na Serikali Kuu kuandaa mazingira ya kupata eneo kubwa zaidi kwa ajili ya matayarisho ya ujenzi wa Majengo ya Sekondari katika Skuli hiyo ya Jamii Kiwengwa ambapo Taasisi yake itakuwa tayari kusaidia ufadhili.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Taasisi hiyo ya Kimataifa inafaa kupongezwa na wapenda Elimu hapa Nchini kutokana na hatua yake ya kuunga mkono makundi ya jamii katika kujikomboa kielimu.

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za taasisi na mashirika ya maendeleo ndani na nje ya nchi yaliyojitolea kusaidia Wananchi hasa wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha ambayo huwa kikwazo cha kupata elimu.

Akizungumza na Wanafunzi wa Kujitolea kutoka Vyuo na Skuli mbali mbali za Marekani alipotembelea maendeleo ya ujenzi huo Mwezi Mei mwaka uliopita Balozi Seif aliwapongeza wanafunzi hao kwa uamuzi wao wa kusaidia Maendeleo ya Elimu katika Visiwa vya Zanzibar.

 Taaluma ya matumizi ya chupa za Maji zinazotiwa mchanga iliyobuniwa Nchini Nicaragua Amerika Ya Kusini katika ujenzi wa majengo mbali mbali ya makazi na huduma za Kijamii inatumika kwa lengo la kutunza  mazingira.

No comments:

Post a Comment