Na Mwandishi wetu, Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemteua Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Maalim seif ambaye pia ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye alikuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuomba ateuliwe kugombea wadhifa huo kupitia chama hicho, alipitishwa kwa asilimia 100 baada ya kupata kura zote 56 za wajumbe wa baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho Vuga, Mjini Unguja, Mkurugenzi Mipango na Uchaguzi Omar Ali Shehe alisema uamuzi huo ulifanywa na kikao cha baraza hilo kilichoketi Juni 3, mwaka huu ambacho kilitanguliwa na kikao cha kamati tendaji taifa kilichokaa Juni 1 kuandaa ajenda za mkutano huo.
Alisema pamoja na kazi hiyo pia baraza hilo lilifanya uteuzi wa wagombea wa uwakilishi na ubunge wa majimbo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kueleza kua hatua hiyo inakamilisha mchakato wa uchaguzi wa ndani ya chama na kwamba chama chake kinajipanga kikamilifu kwa ajili uchaguzi mkuu ujao.
Katika orodha ya wagombea hao, majimbo ya Rahaleo, Makunduchi na Mtambwe wagombea hawajapatikana kutokana na sababu mbambali ikiwemo wagombea kukatiana rufaa iliyopelekea baraza hilo kuamuru uchaguzi wa maeneo hayo kurudiwa na maeneo mengine chama kinaangalia namna ya kuwapata wagombea wa majimbo hayo.
“Safari hii tulibadilisha mfumo wa kuwapata wagombea ndani ya chama chetu, na kutokana na ushindani uliokuwepo tunalazima kurejea uchaguzi wa jimbo la Rahaleo kutokana na rufaa iliyokatwa na mmoja wa wagombea ambaye alilalamikia kuwa kuna watu wasiohusika walipiga kura na kamati ya rufaa ilipojiridhisha ilipendekeza kurudiwa kwa uchaguzi huo”, alisema Shehe ambaye ametetea nafasi yake ya uwakilishi wa jimbo la Chake chake.
Aidha aliwataja walioteuliwa kugombea katika jimbo la Mji mkongwe na nafasi zao kwenye mabano kuwa Ismail Jusa Ladhu (uwakilishi) na mwandishi mwandamizi Ali Abdalla Ali Saleh (ubunge) aliyembwaga mbunge wa sasa Ibrahim Sanya wakati ali juma mwdini (uwakilishi) na Mohamed yussuf maalim (ubunge) waliteuliwa kugombea katika jimbo la jang’ombe.
Aliyewahi kushika nyadhifa mbali mbali katik serikali ya Zanzibar Mohamed Hashim Ismail ameteuliwa kugombea uwakilishi katika jimbo la Dimani wakati katika ubunge nafasi hiyo itagombewa na Khalid Said Suleiman huku Mansour Yussuf Himid akijaribu kurudia wadhifa wake wa uwakilishi alioutumikia kupitia CCM kabla ya kufukuzwa ambaye atashirikiana na Mohamed Nassor Mohamed aliyeteuliwa kugombea ubunge katik jimbo la Kiembe samaki.
Wagombea wengine ni Mohamed Khamis Sultani (uwakilishi) katika jimbo la Kikwajuni ambapo mgombea wa ubunge anatarajiwa kutokea katika chama cha CHADEMA, Maulid Suleiman Juma (uwakilishi) na Omar Ali Khamis (ubunge) waliteuliwa kugombea katika jimbo la Chumbuni.
Katika jimbo la Kwa mtipura Amina Rashid Salumu (uwakilishi) na Abdi Seif Hamad (ubunge), jimbo la Mpendae Ali Hamadi Ali (uwakilishi) na Omar Mohamed Omar (ubunge), katika jimbo la Amani, Khamis Rashid Abeid (uwakilishi) na Khamis Silima Ame (ubunge).
Jimbo la Kwahani Hassan Juma Hassan (uwakilishi) na Khamis Mussa Haji (ubunge), katika jimbo la Magogoni mwakilishi wa sasa ambaye pia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdilahi Jihad Hassan atagombea tena nafasi hiyo pamoja na Saleh Mohamed Saleh (ubunge), wakati walioteuliwa kugombea katika jimbo la Bububu ni Makamo Mwenyekiti wa CUF Taifa, Juma Duni Haji (uwakilishi) na Juma Khamis Juma (ubunge).
Wengine ni Waziri wa Biashara , Viwanda na Masoko wa SMZ, Nassor Ahmed Mazrui atakayetetea nafasi yake ya uwakilishi sambamba na Ame Ali Ame atakayegombea ubunge katika jimbo la Mtoni, wakati katika jimbo la Dole Baraza Kuu liliwateua Yussuf Omar Muhine (uwakilishi) na Khamis Msabaha Mzee (ubunge), jimbo la Mwanakwerekwe walioteuliwa ni Ussi Juma Hassan (uwakilishi) na Ali Salum Khamis (ubunge).
Jimbo la Fuoni walioteuliwa ni Suleiman Simai Pandu (uwakilishi) na Mohamed Juma Aminia (ubunge), jimbo la Nungwi, Hassan Haji Jani (uwakilishi) na Yussuf Haji Khamis (ubunge), jimbo la Matemwe, Nahoda Khamis Haji (uwakilishi) na Dunia Haji Pandu (ubunge), wakati katika jimbo la Mkwajuni Haji Keis Haji (uwakilishi), Khamis Masoud Nassor (ubunge), katika jimbo la Chaani walioteuliwa kugombea ni Khamis Amour Vuai (uwakilishi) na Makame Haji Makame (uwakilishi) na Rashid Khamis Rashid.
Aidha Shehe aliwataja wagombea walioteuliwa katika jimbo la Donge kuwa ni Suleiman Ahmed Suleiman (uwakilishi) na Kombo Mohamed Kombo (ubunge), Zahrani Juma Mshamba (uwakilishi) na Mohamed Amour Mohamed (ubunge) katika jimbo la Bumbwini wakati jimbo la Kitope litagombewa na Hassan Khatib Kheir (uwakilishi) na Mwinshaha Shehe Abdallah (ubunge).
Kwa majimbo ya Mkoa wa Kusini Unguja, Shehe aliwataja Asha Simai Issa na Adam Ali Wazir kuwa wateuliwa kugombea uwakilishi na ubunge katika jimbo la Uzini, jimbo la Koani, Khamis Malik Khamis (uwakilishi) na Shaaban Iddi Ame (ubunge), jimbo la Chwaka walioteuliwa ni Arafa Shauri Mjaka (uwakilishi) na ali Khamis Ame (ubunge).
Kwa upande wa majimbo ya kisiwa cha Pemba yanaongozwa na chama hicho baadhi ya wawakilishi na wabunge waliopo sasa wameanguka, huku wengine wakiponea chupu chupu kutokana ushindani na sifa mbalimbali walizokuwa nazo wagombea hao.
Shehe aliwataja wagombea hao kuwa ni Mmanga Mohamed Hemed (uwakilishi) na Rashid Ali Abdalla (ubunge) jimbo la Tumbe, Subeit Khamis Faki (uwakilishi) na Haji Khatib Kai (ubunge) jimbo la Micheweni, jimbo la Konde, Issa Said Juma (uwakilishi) na Khatib Said Haji (ubunge), wakati katika jimbo la Mgogoni, Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abuubakary Khamis Bakary atagombea tena uwakilishi akishirikiana na Juma Kombo Hamad atakayegombea ubunge.
Katika jimbo la Wete, watakaopeperusha bendera za chama hicho ni Dk. Suleiman Ali Yussuf (uwakilishi) na Mbarouk Salum Ali (ubunge), jimbo la Ole mwakilishi wa sasa ambaye pia ni Waziri katika Serikali ya Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa Hamad Masoud Hamad atatetea uwakilishi wake sawa na mbunge wa sasa Rajab Mbarouk Mohamed atakayewania tena nafasi hiyo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk naye emeteuliwa kutetea nafasi yake ya uwakilishi wa jimbo la Gando ambaye atashirikiana na Othman Omar Haji (ubunge), jimbo la Kojani uwakilishi utagombewa na Hassan Hamad Omar wakati Hamad Salum Maalim atagombea ubunge huku katika jimbo la Mtambwe Shehe alimtamka Khalifa Mohamed Issa kuwania ubunge na kueleza kuwa nafasi ya uwakilishi itajazwa baadaye.
Wagombea wengine katika nafasi hizo ni Omar Ali Shehe (uwakilishi) na Yussuf Kaiza Makame jimbo la Chake Chake, Khamis Faki Marango (uwakilishi) na Mohamed Juma Khatib (ubunge) jimbo la Chonga, Mohamed Ali Salum (uwakilishi) na Ahmed Juma Ngwali (ubunge) jimbo la Ziwani wakati katika jimbo la Wawi Khalifa Abdallah Ali atagombea uwakilishi na Juma Hamad Omar atagombea ubunge kuchukua nafasi ya Hamad Rashid Mohamed ambaye aliwahi kuripotiwa kutaka kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama kimoja cha siasa.
Aidha katika jimbo la Chambani walioteuliwa ni Mohamed Mbwana Hamad (uwakilishi) na Yussuf Salim Hussien (ubunge), katika jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija (uwakilishi) na Abdalla Haji Ame (ubunge) wakati katika jimbo la Mkanyageni wagombea ni Tahir Aweis Mohamed na mbunge wa sasa Mohamed Habibu Juma Mnyaa, jimbo la Mkoani nafasi hizo zitagombewa na Seif Khamis Mohamed na Ali Khamis Seif na katika jimbo la Mtambile uwakilishi utagombewa na Abdallah Bakar Hassan na ubunge Masoud Abdallah Salim.
Akizungumzia uchache wa wagombea wanawake katika orodha hiyo Shehe alisema na imetokana na kutojitokeza kwa wingi katika hatua za awali za mchakato huo na kwa waliojitokeza baadhi yao walipungukiwa na vigezo vilivyotumika kufanya maamuzi kama vile uchache wa kura jambo ambalo alisema linatokana na wanawake wenyewe kutowaungana mkono wanawake wenzao katika mikutano ya majimbo na wilaya.
No comments:
Post a Comment