*Bodaboda wamfungia Ofisi za CCM wakidai fedha zao
Madereva wa bodaboda walioshiriki maandamamo ya kumpokea mtiania wa
nafasi ya Urais kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hamis Kigwangala wakiwa
wamezuia gari lake listoke katika ofisi za chama Wilaya ya Mbeya mjini
baada ya kushindwa kuwalipa fedha kiasi cha shilingi 15000/ kwa kila
mmoja ambazo waliahidiwa jana.
Na Moses Ng’wat, Mbeya.
MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hamis Kigwangala, ameonja joto la jiwe baada ya kujikuta akifungiwa ndani ya uzio wa ofisi za chama hicho, Wilaya ya Mbeya Mjini na kundi la vijana 20 wa bodaboda waliopokea na kusindikiza msafara wake, wakishinikiza kulipwa ujira wao.
Tukio hilo lilitokea jana katika ofisi za chama hicho, Wilaya ya Mbeya mjini, zilizopo eneo la Sabasaba, ikiwa ni muda mfupi baada ya mgombea huyo kumaliza kuwashukuru baadhi ya wanaCCM wenzake waliojitokeza kuja kumdhamini.
Kigwangala ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Igunga, Mkoani Tabora akiwa anajiandaa kutoka ndani ya ofisi hizo za chama ghafla alikuta lango Kuu la ofisi hizo za chama likiwa limefungwa kwa vijana hao kupanga pikipiki zao.
Vijana hao walipanga Pikipiki zao na wao kukaa pembeni huku wakiimba nyimbo za kulalamika kudhulumiwa fedha zao za malipo kiasi cha shilingi 15,000 kila mmoja wao kama walivyokubaliana awali.
Hali hiyo ilionekana kumchanganya mgombea huyo ambaye hata hivyo alilazimika kurudi ndani ya ofisi hizo na kuacha wapambe na waratibu wa ziara yake hiyo wakihaha kumalizana na vijana hao.
Tukio hilo lilichukua takribani dakika zaidi ya 2o na baadae lilipatiwa ufumbuzi na vijana hao kuruhusu mgombea huyo kupita kwa kuziondoa Pikipiki zao.
Kiongozi wa vijana hao wa Bodaboda ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu la Eliya, ambaye hufanya shughuli zake katika eneo la Kabwe, Jijini hapa alisema walifikia hatua hiyo ya kumfungia mgombea huyo kufuatia waratibu wa ziara hiyo kukiuka makubaliano.
“Tulikubaliana kwa saa moja watatulipa kiasi cha shilingi 5000 na tumekaa hapa kwa zaiodi ya saa tatu halafu wanatupa shilingi 5000 tu”.
Elia alisema kuwa, muda wa saa tatu waliutumia kuwa na mgombea huyo, kila mmoja wao alipaswa kulipwa shilingi 15,000 badala ya shilingi 5000 iliyotolewa na waratibu hao.
Gazeti hili lilishuhudia mratibu wa ziara hiyo na mpambe wa mgombea huyo ambaye hata hivyo, hakuwa tayari kutaja jina lake akihaha kutafuta fedha za kumalizia kuwalipa vijana hao, ambapo aliwaomba vijana hao waruhusu mgombea aondoke na yeye abaki ili kumaliza tatizo hilo.
Kauli hiyo iliwaridhisha vijana hao na kuamua kuondoa pikipiki zao na mgombea huyo kuondoka na wao kubaki na mpambe wake .
Tatizo hilo lilitatuliwa na mmoja wa waandishi wa habari wa kituo cha Redio ya kijamii (jina tunalo) baada ya kujitolea f4edha yake ya mfukoni kwa ahadi ya kurudishiwa na mratibu huyo baadae.
Jitihada za waandishi wa habari kuzungumza na Kigwangala kuhusiana na tukio hilo ziligonga mwamba kwa kuwa muda wote wakati tukio hilo likitokea alikuwa amejifungia kwenye gari lake.

No comments:
Post a Comment