Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All Ministry (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kuongezeka kwa joto duniani na athari zake pamoja na tatizo la ulevi nchini ambapo kanisa hilo limeshauri kuwepo na mjadala wa wazi kujadili jambo hilo. Kutoka kushoto ni Mchungaji, Martin Ndaki na Katibu wa huduma hiyo, Palemo Massawe.
Mchungaji Fabian Msimbe akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Mchungaji Leons Kajuna.
Mchungaji Martin Ndaki (kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Askofu Charles Gadi wa Huduma ya Good News for All Ministry (katikati), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu kuongezeka kwa joto duniani na athari zake pamoja na tatizo la ulevi nchini ambapo kanisa hilo limeshauri kuwepo na mjadala wa wazi kujadili jambo hilo. Kutoka kushoto ni Mchungaji Martin Ndaki, Katibu wa huduma hiyo, Palemo Massawe, Mchungaji Fabian Msimbe, Mchungaji Leons Kajuna, Mchungaji Denis Kumbiiho na Mchungaji James Manyama.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
.........................................................................................
Taarifa kwa Umma
KUONGEZEKA
KWA JOTO DUNIANI NA ATHARI ZAKE KWA NCHI ZETU NA HIVI KARIBUNI NCHI YA INDIA.
Ndugu waandishi wa habari,
nawasalimu katika jina la Yesu. Kwanza nawashukuru kwa kufika kwenu kuja kunisikiliza.
Jina langu ni Askofu Charles Gadi wa huduma ya Good News for All Ministry.
Ndugu waandishi wa habari
napenda kuchukua nafasi hii kuzungumzia hali ya joto la la dunia. Tunashukuru
Mungu kwa nchi yetu kupata mvua nyingi mwaka huu, ingawa baadhi yetu
zilituathiri kwa njia moja ama nyingine kutokana na mafuriko. Lakini tunapaswa
kujua kuwa hali ya joto la dunia kwa ujumla siyo nzuri hasa ukichukulia taarifa
za mara kwa mara za kupungua kwa barafu ya mlima Kilimanjaro na kuyeyuka kwa
mabonge ya barafu katika mabara ya barafu ya Actic na Antarctica. Taarifa hizo
za kisayansi zinaonyesha kuwa ongezeko hilo la joto linatokana na uharibifu wa
mazingira na kuongezeka kwa hewa ya ukaa (CO2) CARBON DIOXIDE.
Upungufu wa misitu ambayo
husaidia kunyonya hewa ya ukaa inayotumiwa na miti kutengeneza chakula yaani
phososynthesis na utumiaji wa madawa mbali mbali yanayoharibu mazingira pia
huchangia ongezeko hilo la Joto. Sote ni mashuhuda wa jinsi misitu yetu
inavyoendelea kuangamia kutokana na shughuli za kibinadamu.
Ndugu waandishi wa Habari,
Hivi karibuni imeripotiwa kuwa wimbi kubwa la upepo wa Joto (heat wave)
limeikumba limeikumba nchi ya India na kuua zaidi ya watu 2000 na bado wengine
wanaendelea kupoteza maisha yao. Hiyo si habari njema kwetu sisi tunaokaa
duniani kwani jambo kama hilo linaweza kutufika sisi wakati wowote maana hatuna
kinga yoyote inayotuzuia na ongezeko hilo la joto Duniani. Cha kusikitisha ni kuwa waliokufa wengi ni
wazee, maskini na watoto ambao hawana uwezo wa kujikinga na wimbi hilo la joto
kwani unahitaji uwe na viyoyozi (air conditioning) au maji baridi ya
kujinyunyuzia wakati wimbi hilo la joto likipita.
Kwa sababu hiyo tumesukumwa
na Mungu kuandaa mkutano wa maombi huko India ili Mungu atukinge na madhila
hayo ya mawimbi ya hewa ya joto. Katika safari hiyo ya India tutaambatana na
wachungaji zaidi ya 10 pamoja na waandishi wa Habari kadhaa ili kufanya maombi hayo, yatakayoambatana na
kutoa misaada kwa waathirika wa upepo joto huo. Ni muhimu kwetu kutoa misaada
kwa sababu wale walioathirika ni maskini na wahitaji wa nchi ile na Biblia
inasema kuwa unapomsaidia Maskini unamkopesha Bwana. Ina maana Mungu anaweza
kutumia sadaka hiyo kutuepusha na sisi kupata tatizo linalofanana na hilo
katika nchi yetu.
Ili kufanikisha safari hiyo,
tunawaomba wananchi wote wenye moyo kutuchangia nauli na msaada wa kuwapelekea
waathirika hao. Tunaiomba jamii ya kiasia katika nchi yetu kusaidia katika
hilo, na hata taasisi mbali mbali za fedha na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Safari hiyo ni ya uhamasisho na itahusisha pia kushauri au kuelimisha dhana
nzima ya utunzaji wa mazingira hasa misitu na kupunguza hewa ya ukaa
inayochochea ongezeko hilo la joto duniani.
TATIZO
LA ULEVI KWA TAIFA
Ndugu waandishi wa habari,
Kuna habari kwenye vyombo mbali mbali vya habari na mitandao ya kijamii, na
hata Bungeni jambo hilo limetajwa kwamba vijana wetu na wanandoa wengi
wameathirika sana kwa ulevi wa kupindukia utokanao na matumizi ya pombe za
kienyeji zenye vilevi vikali. Eneo la Rombo limetajwa kwa taarifa iliyotolewa
na mkuu wa Wilaya hiyo na kushuhudiwa pamoja na baadhi ya akina mama waliohojiwa na vyombo vya habari kuwa limeathirika sana. Lakini napenda
kuwaambia kuwa wilaya hiyo ni mfano tu, hilo nitatizo la kitaifa kwani tunaona
mara nyingi katika vijiji, miji na mikoa watu walivyoathirika na ulevi, hadi
kushindwa kutimiza majukumu yao ya kulijenga taifa hilli. Pamoja na kuwepo kwa
habari ya aibu kuwa baadhi ya wanawake wanakodisha wanaume toka nchi jirani ya
Kenya, lakini kinachotakiwa kuangaliwa hapa ni hali halisi ya kuathirika
kwa wananchi wetu.
Sisi tunatoa ushauri kuwa
uwepo mjadala wa wazi juu ya tatizo hilo la ulevi badala ya kutumia nguvu
nyingi kumkemea Mkuu wa wilaya aliyejaribu kutumia nguvu zake kukomesha unywaji
huo mbaya wa pombe. Inasemekana kuwa ndani ya wilaya hiyo kuna aina za pombe za
kienyeji zaidi ya 50 na nyingi huwekwa kweye chupa maalum kama zile za
kiwandani huku zikiwa hazina viwango vya TBS. Baadhi yake zina kilevi (Alkohol)
zaidi ya asilimia 58% jambo ambalo ni hatari kubwa kwa maini na figo za
wanywaji. Uwezekano wa kupuguza nguvu za kiume upo kwani wengi huamka asubuhi
na mapema kunywa vilevi hivyo na hivyo kushindia bila kula jambo ambalo
linawathoofisha kimaumbile.
Hivi karibuni dada mmoja
mwanasheria alitufuata na kutaka tuombe sana kwa ajili ya tatizo la ulevi
katika taifa kwa wanaume kwani amefanya
utafiti katika kazi yake na kugundua kuwa kwenye ndoa nyingi wanaume hawana
nguvu za kiume baada ya kuzoelea ulevi na wamama wengi wanalalamika. Hii
inaonyesha kwamba hili si tatizo la wilaya moja tu, bali ni la kitaifa, na
tunashauri lichukuliwe kwa uzito na kuwekewa mjadala mpana zaidi wa kitaifa ili ufumbuzi upatikane. Tunamwomba
waziri mkuu aliundie tume ili hatua za haraka na za kimakusudi ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja
na za kiroho, kwa kushirikisha wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na serikali,
vyombo vya sheria, vyombo vya kiroho (viongozi wa dini) kutafuta usuluhishi.
Sisi tunaona kuwa ni tatizo
la kiroho kwani upo msemo kuwa ulevi unachangia uzinzi, lakini kinyume chake
sasa inaharibu nguvu za kiume. Ukisoma Kumbukumbu la Torati 28:30 katika Biblia inasema, “Utaoa mke na mume
mwingine atalala naye . . . .” Andiko hilo linamaanisha mtu aliyelaaniwa. Kama
mtu akishindwa kulala na mkewe amelaaniwa.
Maana ikiwa kwa sababu ya pombe wanawake wa
Rombo wanaazima wanaume Kenya, basi na wa Mtwara wataazima Msumbiji na wa
Kagera na Kigoma wataazima Burundi Rwanda na uganda. Sasa ikiwa ulevi huo uko
nchi nzima, wale walio mikoa ya kati wataazima wapi? Napenda muone kuwa tatizo
hili litafika pabaya kama halijachukuliwa hatua stahiki.
Kutokana na hali hiyo
tunashauri itafutwe namna ya kuwashauri wananchi na vijana kwa ujumla nchi
nzima namna ya kuepukana na ulevi huo, na pia sisi kama viongozi wa dini
kushirikiana kuwaelimisha kwa kanuni za kiroho na kimwili, kwani bahati nzuri
madhehebu mengi ya dini hukemea utumiaji wa pombe. Pia watengenezaji wa vilevi hivyo washauriwe kutafuta miradi
mingine ya kuwaingizia kipato badala kutegemea pombe hizo zinazoumiza vijana wetu.
Sasa tatizo la pombe hizo za
viroba na kienyeji ni tatizo kubwa kwa vijana wa primary, secondary, waendesha
bodaboda, madereva wa noa, bajaji nk hata kupunguza kiwango cha elimu, ajali za
mara kwa mara, na nguvu kazi ya nchi kwa ujumla. Hili tatizo ni kubwa mno na
linalenga kuharibu (generation) au kizazi hiki cha vijana na kutengeneza jamii
ambayo haitafundishika au kutawalika kwa urahisi.
Tunawashukuru sana kwa
kutusikiliza.
Wako Charles Gadi Mwenyekiti: GOOD NEWS FOR
ALL MINISTRY. (Imeandaliwa na Dotto Mwaibale)
No comments:
Post a Comment