Mahakama kuu ya Uhispania imeagiza mechi za ligi kuu ya Uhispania La Liga ziendelee pasi na mgomo.
Mahakama hiyo imeamua kuwa mgomo ulioitishwa na shirikisho la mchezo huo (RFEF) uliodumu kwa juma moja unakiuka vipengee vya makubaliano ya upeperushaji wa mechi hizo.
(RFEF) iliiitisha mgomo kupinga sera mpya inayopendekezwa na serikali ya kudhibiti mikataba ya upeperushaji wa mechi za ligi hiyo maarufu.
Kauli hiyo ya mahakama inaruhusu mechi za ligi kuu zilizokuwa zimesalia kabla ya msimu kukamilika kuchezwa wikiendi hii.
Vinara wa soka ya Uhispania Barcelona watakuwa katika nafasi nzuri ya kutawazwa mabingwa iwapo watawacharaza mabingwa watetezi Atletico Madrid siku ya jumapili.
Aidha fainali ya kombe la mfalme huenda ikachezwa mwishoni mwa mwezi huu kufuatia uamuzi huo.
Barca, ambao tayari wamefuzu kwa fainali ya kombe la mabingwa barani ulaya ambapo wameratibiwa kukwaruzana na Juventus, watachuana dhidi ya Athletic Bilbao uwanjani Nou Camp katika fainali ya kombe la Mfalme ama Copa del Rey .
RFEF na shirikisho la wachezaji nchini Uhispania wamelalamikia kiwango cha chini cha marupurupu watakayopata katika mapendekezo ya kandarasi mpya baina ya runinga ya taifa na serikali.
Mashirikika hayo mawili yametofautiana vikali na sera mpya ya kugawanya marupurupu ya fedha za haki miliki ya kupeperusha matangazo miongoni mwa vilabu vyote.
Kwa sasa kampuni inayoendesha ligi hii National Professional Football League (LFP) imekubaliana na sera hiyo ya serikali japo wachezaji wanalalamika mapato yao yatapunguzwa.
Rais wa LFP Javier Tebas aliahidi kwenda mahakamani kupinga mgomo huo akisema utaigharimu takriban Euro milioni 50 kwa siku.
No comments:
Post a Comment