Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS mkoani Morogoro. Waziri Magufuli amewapongeza TANROADS kwa utendaji kazi wao mzuri ujenzi wa Barabara nchini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara TANROADS Eng. Patrick Mfugale akisoma risala kwa Mgeni Rasmi Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli.TANROADS imepata TUZO ya mfanyakazi bora na mwajiri bora kutoka TAMICO.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli katikati akiwa ameshikana mikono na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, TANROADS Eng. Patrick Mfugale kushoto pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Rutengwe kulia wakiimba wimbo wa Mshikamano Daima kabla ya ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS.
Baadhi ya Wajumbe kutoka mikoa mbalimbali wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi katika ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia tuzo aliyokabidhiwa na Wafanyakazi wa TANROADS kwa kutambua uongozi wake bora katika kuanzisha na kule Wakala huo tangu mwaka 2000-2015. (Picha zote na Dotto Mwaibale)
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS mara baada ya mkutano uliofanyika mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Rutengwe mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS mkoani Morogoro. Picha kwa Hisani ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Ujenzi.
Na Suleiman Msuya
WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli amewataka wafanyakazi wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kufanyakazi kwa ubunifu, uzalendo na uadilifu ili kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Akifungua mkutano wa tano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanroads mjini Morogoro Waziri Magufuli alisema asilimia 14.3 ya pato la taifa linatokana na kukua kwa sekta ya usafirishaji ambayo asilimia 99.3 ya usafirishaji wote nchini unatumia barabara.
“Ni asilimia 0.7 tu ya bidhaa zote nchini zinatumia usafiri wa anga, reli na bahari hivyo ni wazi kuwa sekta ya barabara ni nguzo muhimu ya uchumi wa nchi”, amesisitiza Waziri Magufuli.
Waziri Magufuli ameipongeza Tanroads kwa mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka 15 tangu ianzishwe na kufanikiwa kuwa mwajiri bora wa TAMICO mwaka 2014/2015.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rajabu Rutengwe amepongeza Tanroads mkoani Morogoro kwa kazi nzuri wanazofanya na kuitaka kushirikiana na taasisi nyingine katika kudhibiti ajali za barabarani.
Amehimiza umuhimu wa Tanroads kudhibiti magari yanayoegeshwa kiholela barabarani na kuongeza mizani zinazotembea ili kudhibiti uharibifu wa barabara unaosababishwa na magari kuzidisha uzito.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mtendaji Mkuu wa Tanroads na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhandisi, Patrick Mfugale amewataka wajumbe kuwa huru ili kuwezesha kujitathmini kwa haki na hivyo kuongeza tija katika utendaji kazi.
Mfugale amewataka Wahandisi kuwa wabunifu na wanaozingatia thamani ya fedha ili miradi ya ujenzi idumu kwa muda mrefu na kuchochea maendeleo ya nchi.
Amesema Tanroads imechaguliwa kuwa ya tatu kwa utendaji bora wa kazi kwa taasisi za ujenzi barani Afrika ikitanguliwa na nchi za Afrika Kusini na Namibia.
Mtendaji Mkuu huyo alisema Tanroads ilianzishwa mwaka 2000, kwa ajili ya kusimamia ujenzi wa barabara kuu na za mikoa hapa nchini ambapo hadi sasa inasimamia ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 35,000.
No comments:
Post a Comment