TANGAZO


Monday, May 11, 2015

DAWASCO kuanza msako wa kuwakamata wezi wa maji na kuwashitaki kama wahujumu uchumi

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco), Mhandisi Cyprian Luhemeja (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu mkakati wa shirika hilo wa siku 180 katika kupambana na uhujumu wa maji na uboreshaji wa huduma za maji katika jiji la Dar es Salaam. Wa pili kushoto ni Ofisa Uhusiano wa Dawasco, Everlasting Lyaro.

Na Dotto Mwaibale
SHIRIKA  la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (Dawasco), linatarajia kuendesha msako mkali ili kuwabaini watu wanaoliibia maji na mtu atakayetoa taarifa za mtu anayeiba maji atapewa motisha ya sh. 500,000.

Hayo yalibainishwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo.

“Tutatoa motisha ya sh.500,000 kwa mtu atakayeleta taarifa za wizi wa maji zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa na pia kesi tutakapozifungua hatutawashtaki kama waharibifu wa miundombinu ya maji bali watashtakiwa kama wahujumu uchumi wa nchi ili kesi zao zipatiwe ufumbuzi mapema” alisema Luhemeja.

Akizungumzia mikakti ya shirika hilo alisema wamekuja na mkakati mzito wa siku 180 za kuhakikisha hujuma zote za maji katika jiji la Dar es salaam zinakoma ili upatikanaji wa maji uwafikie wananchi kwa muda muafaka na kwa maeneo mengi jijini.
Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na operesheni maalum isiyokuwa na kikomo ya wezi wa Maji, wanaojiunganishia Miundombinu ya Dawasco kinyume na taratibu, wanaotengeneza tofali na wote wanaohujumu miundombinu ya Maji kwa namna moja au nyingine.

Alisema shirika hilo linazalisha lita milioni 300 kwa siku lakini mahitaji halisi ni lita milioni 515 hivyo kuna upungufu wa maji kwa kiwango cha lita milioni 215. Hapohapo upotevu wa Maji ni asilimia 57 kwa takwimu za sasa. 

Kwa hali hii hatuna budi kuingia mtaani na kujifunga ipasavyo kuhakikisha kiasi hiki kinapungua ili kuweza kuendesha shirika na kuleta nafuu kwa wananchi ambao hawapati huduma hii” alisema Luhemeja.

Alitoa wito kwa jamii husika kutoa taarifa hizo kupitia namba ya simu 0658-198889 na taarifa hizo zitatunzwa kwa ajili ya usalama wa mtoa taarifa na zitafanyiwa kazi kwa wakati. 

No comments:

Post a Comment