Na
Anitha Jonas – MAELEZO.
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania
laanda Tamasha la Tuzo za Filamu (TAFA) linalotarajia kufanyika Mwezi Mei 2015 katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini
Dar es Salaam lenye lengo la kuonyesha wachezaji filamu chipukizi wanaofanya
vizuri katika tansia ya filamu nchini.
Hayo yamesemwa na Rais
wa Shirikisho la Filamu Tanzania Bw. Simon Mwakifwamba alipotembelewa ofisini kwake
na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu nchini
Bibi Joyce Fisoo kwa ajili ya kujua
maendeleo ya maandalizi ya Tamasha hilo lenye nia ya kukuza tansia ya filamu
nchini na kudhamini mchango wa filamu katika kuongeza kipato kwa vijana, kuelimisha
na kuburudisha jamii.
“Tuzo hizi zitakuwa na
majaji wenye uzoefu mkubwa kutoka Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda
na Tanzania na pia ushindani
umegawanyika katika vigezo kumi na tatu na washindani katika vigezo hivyo ni
kati ya wasanii watano mpaka nane ambapo kwasasa namba ya kuwapiga kura
washiriki hao kwa njia ya simu imeshapatikana na mchakatao wa kupanga namba za
washiriki kulingana na vigezo vyao
wanavyoshindania vinaendelea na mchakato huo utakamilika hivi karibuni,”alisema
Bw. Mwakifamba.
Rais wa Shirikisho hilo
aliendelea kusema kuwa maandalizi ya tuzo hizo yamekuwa na changamoto kubwa ikiwemo
ukosekanaji wa fedha za kutosha na ufadhili hivyo ombi lake kwa watanzania wote
na wadau mbalimbali kujitokeza kutoa ufadhili katika kufanikisha utolewaji wa
tuzo hizo kwani ni jambo lenye manufaa kwa wasanii wa filamu kutokana na kazi
nzuri ya kuburudisha na kuelimisha jamii hivyo ni vyema tutambue mchango wao.
Aidha Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi Joyce Fisoo alimsihi Rais
wa Shirikisho la Filamu Tanzania kuandaa mwongozo wa kutengeneza video za kampeni ya uhamasishaji
wa tuzo hizo na kuziwasilisha ofisi ya Bodi ya Filamu kuzihakiki na kuandaa namba maalum ya mitandao
ya simu ambayo wananchi wanaweza kutuma michango yao kupitia M-PESA, TIGOPESA, AIRTEL MONEY na EZY PESA kwa
ajili ya kufanikisha tamasha hilo.
“Ni vyema muwe mnaleta
taarifa fupi Wizarani kuhusu maandalizi ya tuzo hizo ili uongozi
ujue namna gani mmejipanga na maandalizi yanakwenda vipi na Serikali iwasaidie
wapi ili kufanikisha tamasha hilo na kwa kufanya hivi mnaweza kupata ushauri na
maelekezo muhimu ya kuzingatia katika maandalizi hayo,”alisema Bibi Fisoo.
Halikadhalika Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu aliwataka viongozi
wa Shirikisho la Filamu nchini kuwa na mshikamano
miongoni mwao ili kuweza kufanikisha tamasha
hilo kwani Umoja ni nguvu hivyo kufanya kazi kwa umoja.
No comments:
Post a Comment