Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati) akiongoza kikao cha Wizara ya Kilimo na Maliasili kilichozungumzia utekelezaji mpango kazi wa Wizara ya hiyo kwa kipindi cha mwezi Julai-Disemba 2014 katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi
Waziri wa Kilimo na Maliasili Sira Ubwa Mamboya (katikati) akitoa taarifa ya utekelezaji mpango kazi wa Wizara ya hiyo kwa kipindi cha mwezi Julai-Disemba 2014 katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo asubuhi wakati wa kikao cha pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) Katibu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na (kushoto) Naibu Waziri Mtumwa Kheir Mbarouk,
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amepongeza juhudi
zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo na Maliasili katika kuhakikisha sekta hiyo
inaimarika sambamba na hatua yao mpya ya kuendeleza kilimo cha biashara likiwemo
zao la alizeti.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika Mkutano wa Utekelezaji Mpango Kazi wa Wizara ya
Kilimo na Maliasili kwa kipindi cha Julai 2014 hadi Disemba 2014, uliofanyika
huko Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo
yake, Dk. Shein alisema kuwa hatua hiyo ina umhimu mkubwa katika katika
kuimarisha sekta hizo kwa pamoja na kueleza haja kwa Wizara ya Kilimo na
Maliasili kuendeleza kilimo hicho na baadae kutamfuta mwendelezaji wa biashara
hiyo mwanga wa mafanikio umeshaonekana.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alieleza haja ya Wizara hiyo kuwashajiisha wananchi kupanda minazi kwa
kutambua kuwa bado zao hilo linathamani hapa nchini huku akisisitiza kuwepo na
kujua idadi kamili ya upandaji wa minazi kwa mwaka na kuepuka kuikata ovyo.
Aidha, alieleza
juhudi za makusudi kufanywa katika kuhakikisha miti ya matunda inapandwa kwa
wingi ikiwa ni pamoja na kuongeza vitalu vyake sambamba na kuwashajiisha
wananchi kupanda miti hiyo ikiwemo miti ya matunda ya asili.
Dk. Shein pia,
alieleza haja ya kuwekewa mazingira mazuri watafiti wa kilimo ikiwa ni pamoja
na kuwapa motisha ili waendelee kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Nae Makamo wa
Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, kwa upande wake alizipongeza
juhudi za Wizara hiyo huku akieleza haja kwa Wizara hiyo kuwahamasisha wananchi
kupanda minazi kutokana na kuwepo kwa bidhaa mbali mbali zkinazotokana na mnazi
huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha kilimo cha mboga mboga.
Balozi Seif pia,
alieleza haja ya kuimarishwa juhudi katika kuweka maghala wka ajili ya uhifadhi
wa chakula.
Akitoa maelezo ya
Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara hiyo, Waziri wa Kilimo na Malisili Mhe. Dk.
Sira Ubwa Mamboya alieleza kuwa Wizara yahiyo katika kuendeleza juhudi za
kilimo cha biashara, imefanya majaribio ya ukamuaji wa mafuta yanayotokana na
zao la alizeti.
Alisema kuwa
Wizara imenunua mtambo wa kukamulia mafuta wenye uwezo wa kukamua tani 6.5 za
alizeti kwa siku kwa hapa Unguja na
juhudi za kununua mtambo huo kwa ajili ya Kisiwani Pemba zinaendelea.
Dk. Mamboya
alisema kuwa Wizara ya Kilimo imenunua tani tatu za mbegu ya alizeti ambayo
itapandwa katika ekari 3000 ambapo ekari 1500 maeneo ya juu na ekari 1500 kwa maeneo ya mabondeni baada ya kuvuna mpunga
kwa upande wa Unguja na Pemba.
Waziri huyo
alieleza kuwa uimarishaji wa Kilimo kwa njia ya Mageuzi ya Mapinduzi ya Kijani
ndio mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ina nia ya kutekeleza kwa
vitendo dhamira ya kuwakomboa wakulima wa Zanzibar kutoka kilimo duni
kisichokuwa na tija na kuweka mazingira bora ya uzalishaji.
Alieleza kuwa
katika kipindi cha mwaka wa 2014/2015 Wizara inatekeleza dhamira ya Mapinduzi
ya Kilimo yatakayopelekea kutoa mchango zaidi katika kukuza uchumi wa Taifa
sambamba na kupunguza umasikini.
Aidha,
alisisitiza kuwa mwelekeo huo unatoa fursa endelevu za kuwawezesha wakulima
kuongeza kipato na tija katika kilimo na kuwa na uhakika wa chakula na lishe
bora
Sambamba na hayo,
Dk. Mamboya alisema kuwa sekta za Kilimo na Maliasili bado zinaendelea kuwa ni
muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar ambapo inatoa mchango wa moja kwa moja
katika kujikimu kimaisha, kuwa na uhakika wa chakula, lishe na afya za wananchi
walio wengi vijijini na mijini.
Kwa mwaka wa
fedha 2013/2014 sekta hizo zilichangia asilimia 30.2 ya Pato la Taifa na inakadiriwa
kuwa zaidi ya asilimia 70.3 ya wananchi wanategemea sekta ya kilimo kwa
kuwapatia ajira na mapato.
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Cuba
nchini Tanzania Mhe. Jorge Luis Lopez ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao
walieleza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo wa muda mrefu.
Balozi wa Cuba
alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya afya ambapo nae Dk. Shein kwa
upande wake alieleza jinsi Zanzibar inavyothamini juhudi za nchi hizo.
No comments:
Post a Comment