Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na Ujumbe wa Mamlaka ya Uwekezaji (Qatar Holding) mjini Doha, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne nchini Qatar.
Mkurugenzi wa maendeleo ya biashara wa mamlaka ya uwekezaji ya Qatar Sheikh Faisal Bin Soud Al-Thani, akizungumza na ujumbe wa Zanzibar ukiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad mjini Doha.Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiongozana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar Sheikh Faisal Bin Soud Al-Thani, baada ya mazungumzo yao mjini Doha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar Sheikh Faisal Bin Soud Al-Thani, baada ya mazungumzo yao mjini Doha.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar Sheikh Faisal Bin Soud Al-Thani, baada ya mazungumzo yao mjini Doha.(Picha zote na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, Doha.
11/02/2015.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewakaribisha wawekezaji nchini Qatar kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali zikiwemo utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Akizungumza na uongozi wa Mamlaka ya Uwekezaji nchini Qatar ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake nchini humo, Maalim Seif amewatoa hofu wawekezaji wa nchi hiyo, na kwamba Zanzibar yako maeneo mengi ya uwekezaji kwa makampuni yanayotaka kufanya hivyo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imejipanga kupokea wawekezaji hasa katika sekta za utalii, viwanda vidogo vidogo na uvuvi wa bahari kuu, na inaendelea kuimarisha miundombinu katika maeneo ya uwekezaji ili kurahisisha kazi hiyo.
Amesema Serikali imekuwa ikijidhatiti kuimarisha viwanja vya ndege, bandari na ujenzi wa barabara katika maeneo ya uwekezaji, sambamba na kuimarisha huduma za umeme na maji katika maeneo hayo, ili kuondosha usumbufu kwa wawekezaji.
Aidha Maalim Seif amesifu hatua nzuri ya maendeleo iliyofikiwa nchini Qatar katika kipindi kifupi kilichopita, na kwamba Zanzibar ina mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa ndugu zao wa Qatar.
Akizungumzia kuhusu sekta ya mafuta na gesi asilia, Maalim Seif amesisitiza kuwa eneo hilo litapatiwa ufumbuzi mara baada ya kuondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Qatar (Qatar Holding), Sheikh Faisal Bin Soud Al-Thani, amesema atawasiliana na Makampuni ya uwekezaji nchini humo, ili kuona maeneo wanayoweza kuweka vitega uchumi vyao.
Hata hivyo ameomba kuwepo na mawasiliano ya karibu kati ya mamlaka hiyo ya Qatar na mamlaka ya vitega uchumi ya Zanzibar (ZIPA), ili kuweka wazi sheria na taratibu za uwekezaji za Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Sheikh Faisal amesisitiza haja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa kipaumbele katika uimarishaji wa miundombinu katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, ili kuweza kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
“Miundo mbinu ni muhimu sana katika maeneo ya uwekezaji kwani ni vigumu kwa muwekezaji kujenga kila kitu, kwa hivyo Serikali pia ina jukumu kuhakikisha kuwa baadhi ya mambo ya msingi yakiwemo barabara, maji na umeme yanapatikana katika maeneo hayo”, alishauri Sheikh Faisal.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana nchini humo, Sheikh Faisal amesema yametokana na mashirikiano mazuri yaliyopo kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi.
Akionekana kupendezwa na mazingira ya Zanzibar, Sheikh Faisal amesisitiza kuwa kabla ya kutembelea na kuyashawishi makampuni ya Qatar kuwekeza Zanzibar, atawasiliana na mamlaka ya vitega uchumi Zanzibar (ZIPA) ili kujua taratibu za uwekezaji, na kutaka ushirikiano baina ya Zanzibar na Qatar uendelezwe.
No comments:
Post a Comment