TANGAZO


Wednesday, February 4, 2015

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Idd azungumza na Ujumbe wa Mfuko wa Bima ya Afya

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka Kulia akizungumza na Uongozi wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania ukiongozwa na Bwana Ezekiel Olouchi aliyepo kati kati yao. Kushoto ya Balozi Seif ni Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya Kanda ya Zanzibar Nd. Ismail Kangeta, kulia ya Bwana Ezekiel Olouchi ni Mkurugenzi wa Wizara ya Afya  aliyenyoa Nywele Dr. Moh’d Mohammed na Mkurugenzi wa ICT Nd. Ali Othman.
Kiongozi wa Ujumbe wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania Bwana Ezekiel Olouchi aliyevaa Miwani akimuelezea Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanzishwa kwa mfuko huo.
Balozi Seif akiupongeza Uongozi wa Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania kwa jitihada za kuwajengea mazingira bora ya huduma za afya wanachama wake. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/2/2015.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuona haja kwa Taasisi zake kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya Tanzania ili wafanyakazi  wa Taasisi hizo wapate fursa za kupata huduma bora na ya uhakika ya afya inayotolewa na Hospitali mbali mbali hapa nchini.

Ombi hilo limetolewa na Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania Bwana Ezekiel Olouchi wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Ezekiel Olouchi  aliyeuongoza ujumbe wa Viongozi wanne wa Bodi hiyo ya Bima ya Afya walikuwepo Zanzibar kukutana na viongozi wa Taasisi mbali mbali za Muungano ambazo wafanyakazi wake ni wanachama wa Mfuko huo kuangalia huduma zinazotolewa kupitia mfuko huo.

Alisema licha ya kwamba sheria ya Bima ya Afya haitumiki Zanzibar lakini zipo baadhi ya Taasisi na wafanyakazi wa umma wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioonyesha shauku  ya kutaka kujiunga na mfuko huo wakiwa na lengo la kutaka kustawisha afya zao.

Bwana Olouchi alisema kwamba mfanyakazi ye yote aliye mwanachama wa mfuko huo wa Bima ya Afya  ana haki ya kutibiwa katika muda wote wa maisha yake hata kama ameshastaafu kazi katika Taasisi iliyokuwa akiifanyia kazi.

Mjumbe huyo wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania ameushauri uongozi wa Hospitali ya Umma Zanzibar kujitahidi kujijengea miundo mbinu imara  ya vifaa itakayotoa ushawishi kwa Tasisi zenye wanachama wa mfuko huo kupeleka wafanyakazi wao kutibiwa katika Hospitali hizo.

Alisema wanachama wengi wa mfuko huo wamekuwa wakizitumia Hospitali na Vituo vya Afya Binafsi kupata huduma za Afya  jambo ambalo makusanyo ya fedha wanazotoa yangeingia katika hospitali ya Umma  ili kusaidia kutunisha mfuko Mkuu wa Serikali.

Bwana Ezekiel alifahamisha kwamba mfuko wa Bima ya Afya umekuwa ukitenga zaidi ya shilingi Milioni 10,000,000/- kwa ajili ya ununuzi wa dawa kwa wanachama wa mfuko huo.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba licha yaSerikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka huduma za Afya bila ya malipo mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 lakini haizuii watu binafsi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya.

Balozi Seif alisema wazo la Uongozi huo wa Bodi ya Mfuko wa Bima ya Afya litazingatiwa ipasavyo na Serikali ili kuona namna ya kuzipa fursa Taasisi zake kuamuwa kujiunga na mfuko huo kulingana na sheria iliyopo.

“ Kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya Tanzania ni wazo zuri na ipo haja kwa Taasisi za Zanzibar kuangalia utaratibu wa kujiunga na mfuko huo “. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Jumla ya shilingi Bilioni 1.1 zimekusanywa na Hospitali binafsi kutokana na michango ya huduma za afya zinazotolewa na Wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya tokea mwezi Aprili Mwaka 2014 wakati Hospitali za Serikali ni Shilingi Milioni Mia 1.7 tu.

Huduma  ya Afya kwa wanachama wa Mfuko huo wa Bima ya Afya kwa Vituo vya Majeshi ilifikia zaidi ya shilingi Milioni 200 wakati vituo vya Kiraia huduma hiyo ilifikia shilingi Milioni 80.4.

No comments:

Post a Comment