TANGAZO


Friday, February 6, 2015

BUNGENI LEO MJINI DODOMA

Waziriwa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, akijibu hoja Bungeni. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma)
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid akijibu hoja za kamati na wabunge.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba akifafanua hoja Bungeni.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa akijibu hoja za kamati.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri akijibu maswali ya wabunge. 
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga akijibu maswali Bungeni.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarwa akijibu swali la Mbunge Bungeni. 
Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Christopher Ole Sendeka.Kamati hiyo iliundwa kuchunguza na kuchambua Sera mbalimbali zinazohusu masuala ya Aridhi, Kilimo, Mifugo,Maji na Uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya Ardhi. 
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Bungeni.
Baadhi ya wageni waliohudhuria Bungeni Dodoma leo. 


Viongozi na Wabunge watakiwa kuzisimamia Halmashauri zao
Na Hussein Makame-MAELEZO, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara, amewataka viongozi na wabunge kuzisimamia Halmashauri zao ili kuhakikisha zinatekeleza Sheria na agizo la Rais Jakaya Kikwete  la kutenga asilimia 10 kwa ajili ya mfuko wa vijana na wanawake.

Ametoa agizo hilo wakati akijibu hoja za wabunge na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, zilizowasilishwa wakati wakichangia taarifa ya kamati hiyo iliyowasilishwa Bungeni, Dodoma.
Alisema pamoja na Wizara yake kushirkiana na Wizara ya TAMISEMI, kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo, ni halmashauri 38 tu kati ya halmashauri 158 ndizo zimetenga fedha kwa ajili ya mfuko wa Maendeleao ya Vijana na Wanawake.

“Naomba niombe sisi sote ni viongozi basi tusimamei halmashauri zetu ili tuhakikishe wanatekeleza hili kwa nguvu zote kama inavyotakiwa kwa sababu hizi fedha zikipatikana mfuko huo ambao hauna fedha za kutosha, utapata ahuweni” alisema Dkt. Mukangara.
Aliongeza kuwa pamoja na halmashauri hizo kutenga fedha hizo, lakini hazikutenga kiasi kinachohitajika cha aslimia 10 kama inavyotakiwa.
Waziri Dkt. Mukangara aliwataka wabunge na viongozi mbalimbali wasitumie muda mrefu sana kulalamikia mfuko wa vijana kwani Wizara yake inafanya kazi kubwa sana kwa fedha inayoipata kuitoa kwa vikundi vya vijana.

“Kwa mwaka huu tumepata Shilingi Bilioni 2 lakini hata katika hizo Bilioni 2 pamoja na uhamasishaji ambao tumeufanya kwa kupitia halmashauri mbalimbali, maombi yamekuja machache sana” alisema.
Aidha aliwataka wabunge na viongozi mbalimbali kuwahamasisha vijana kuunda vikundi na kuomba fedha hizo kutoka Wizaya hiyo kwani hadi sasa ni halmashauri 30 zilizotuma mambo kupitia vikundi vya vijana 1,390.

“Ni halmashauri 30 tu kati ya zile tulizozihamasisha nchi nzima zimeleta maombi wizarani na yale maombi yaliyoletwa yana vikundi vya vijana 1,390 na vikipewa pesa yake yote vinagharimu karibu shilingi Bilioni 10” alisema Dkt. Mukangara.

Aliwataka kuwahimiza na kuwasimamia vijana ili kusaidiana na juhudi ambazo wizara inazifanya na kuhakikisha maombi yao yanafika na kuutumia mfuko huo.

Alisema Wizara imezunguka mikoa mingi nchini kutoa mafunzo lakini bado mwitikio ni mdogo, hivyo aliwaomba wabunge wakusanye vijana kwenye maeneo yao na kubadilisha mitazamo yao katika kuhakikisha wanajituma na wanajitolea na kutambua kwamba suala la ajira linawategemea wao wenyewe.

“Sasa hili ni muhimu sisi kama viongozi kuweza kuchukua hiyo nafasi ya kuhakikisha vijana tunaowaongoza na kuwaita kama vile ni bomu wasigeuke boma kwa sabau kama ni bomu tutakuwa tunalitengeneza sisi wenyewe” alisema.

Aliongeza “Kwa sababu hawa vijana tunaowalalamikia kwamba hawana nidhamu au ni bomu au hawana ajira hawatoki sayari ya Mars wanatoka katika jamii zetu wanatoka katika sehemu ambazo tumesema  tunazoziongoza”.

Hivyo aliwataka wahakikishe kuwa kero zinazowazunguka vijana wakae na  kuhakikisha kwamba wanazishughulikia.

Alisema kupitia mfuko wa vijana pesa kidogo walizozipata wamezifanyia kazi na wale ambao wameleta maombi yao mchakato bado unaendelea ili kuhakikisha wanapata fedha zinazostahili.

Mfuko wa Vijana na Wanawake uliundwa kisheria mwaka 1993, na Rais Jakaya Kikwete alitoa agizo la kutaka kila halmashauri inatakiwa itoe taarifa ya kiasi ilichotengwa cha asilimia 5 kwa ajili ya vijana na asilimia 5 kwa wanawake.

Akizungumzia madai kwamba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatoa huduma zake kwa kukipendelea Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri Dkt. Mukangara alisema madai hayo si kweli na wanayoyatoa wanataka kufurahisha jamii.

Alisema TBC inafanya kazi kwa wananchi na jamii yote, CCM kikitumia TBC kinalipa na hata katika sherehe zilizopita kimelipa, lakini hata NCCR-Mageuzi wameshawahi kufanya mkutano wao na TBC ikaurusha moja kwa moja na walilipa.

Wafungwa kupatiwa haki ya kupiga kura
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma
SERIKALI imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wafungwa wote wanaotumikia kifungo chini ya miezi sita na mahabusu wanawapatia haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje  aliyehoji kuhusu wafungwa kutoruhusiwa kupiga kura,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Uratibu na Bunge, Jenister Mhagama alisema kwa mujibu wa ibara ya 5(2) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wafungwa wote wenye vifungo chini ya miezi sita wanaruhusia kupiga kura.

Aliongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshaanza  kufanya utafiti pamoja na mazungumzo kupitia taasisi mbalimbali zinazohusika na wafungwa  kuweka utaratibu  wa kuwawezesha kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

‘Wafungwa wanaotumikia vifungo vyao chini ya miezi sita wana haki ya kupiga kura ya kuchagua viongozi wao na hiyo imeainishwa katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Waziri Mhagama.

Aidha aliongeza kuwa kwa wale wanaotumikia vifungo zaidi ya miezi sita Serikali itangalia namna ya kuwasidia kwa kuzingatia sheria na kanuni zinavyosema na kama katiba hairusu basi hawataweza kushiriki kupiga kura.

 Naye Mbunge wa Viti Maalum  Maryam Msabaha alihoji kuhusu mpango wa Serikali katika kuwapatia  ajira  wafungwa walioweza kuhitimu taalum mbalimbali waliokuwa wakitumikia vifungo, ambapo Waziri Mhagama alifafanua kuwa wafuate taratibu na sheria za kuomba ajira.

“Kwa upande wa wale wafungwa wanaohitimu mafunzo mbalimbali yanayotolewa gerezani kabla ya kupata ajira ni vyema wakapata ushauri na baadaye kuajiriwa au kujiajiri wenyewe ” alisema Mhagama.


Hata hivyo alisisitiza kwamba wafungwa wanapomaliza vifungo vyao huwa watu huru wenye maamuzi yao binafsi katika kuendeleza maisha yao ya kila siku  katika kujiletea maendeleo yao.

Serikali yaingia Mkataba wa kubadilishana wafungwa
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma
SERIKALI ya Tanzania imeingia mkataba  wa kubadilishana wafungwa kwa nchi za Thailanda na Mauritius ambapo hadi sasa Tanzania imeweza kupokea wafungwa kumi kutoka nchi hizo kutekeleza mkataba huo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Silima alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati aliyetaka kujua u ni nchi zipi Tanzania imesainiana nazo mkataba wa kubadilishana wafungwa.

Naibu Waziri Silima aliongeza kuwa katika kutekeleza mkataba kati ya wafungwa hao 10, tisa wameshamaliza hukumu za vifungo vyao huku mmoja anategemea kumaliza kutumikia kifungo mwaka 2021.
“Mpaka sasa Serikali yetu imeweza kuhudumia wafungu kumi kutoka nchi hizo mbili  ambapo mwanamke mmoja na wanaume tisa” alisema Silima.

Aidha aliongeza kuwa kupitia diplomasia ya mahusiano baina ya nchi na nchi, Serikali inaweza kuingia mkataba na nchi nyingine tatu ambazo ni Kenya, China na India ambako wananchi wake waamekuwa wakitumikia vifungo mbalimbali.

Vilevile alitoa wito kwa Watanzania wanaosafiri katika nchi mbalimbali  kuzijua sheria na taratibu za nchi hizo ili kutoingia  katika matatizo pamoja na wajiupushe na biashara haramu ikiwemo ya dawa za kulevya.

Pia kwa upande wa wale wanaotumikia vifungo katika nchi ambazo Tanzania haina mkataba nao wa kubadilishana wafungwa, waweze kuwasiliana na balozi za Tanzania ili kupata msaada wa kisheria.

Wakazi karibu na mito watakiwa kukaa mbali kuepuka madhara ya viboko
Na Lorietha Laurence-Maelezo,Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa wito kwa wananchi wanaoishi kandokando ya mito kukaa umbali wa mita 60 toka vyanzo hivyo vya maji ili kuepuka madhara ya viboko.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Clara Mwatuka, Bungeni Dodoma  kuhusu utaratibu wa serikali katika kuwaondoa viboko katika bonde la mto Lukuledi, Naibu Waziri wa Fedha Mwiguru Nchemba kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ameeleza  serikali katika kutatua tatizo hilo wameweza kuajiri watumishi watatu wa wanyamapori pamoja na askari.

Aliongeza  kuwa  kumekuwepo na matukio mbalimbali ya viboko kuvamia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao ambapo kwa kipindi cha mwezi Desemba 2013 hadi Machi,2014  viboko wawili waliuawa  katika vijiji vya Nanganga na Nangookata na wengine watano kurudishwa katika maeneo yao. 

“Matukio mbalimbali yameripotiwa hatua madhubuti  zimechukuliwa ikiwemo kuwarudisha katika sehemu husika pamoja na kupanga bajeti ya kuongeza watumishi wa wanyamapori” alisema Naibu Waziri Nchemba.

Aidha aliongeza kuwa sababu ya kuongezeka kwa matukio ya viboko katika vijiji hivyo hutokana na  shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazofanywa kandokando ya Bonde la mto Lukuledi ikiwemo kukatwa kwa miti pamoja na kilimo.

Hata hivyo alisema Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili watambue athari za uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kutoa elimu ya kuwalinda wanyamapori kupitia WMAs (Wildlife Management Areas) itakayowanufaisha wananchi  kiuchumi kupitia utalii.

No comments:

Post a Comment