TANGAZO


Monday, January 19, 2015

Rais Dk.Shein afungua Semina ya Matokeo Makubwa na Yaharaka

Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifurahia jambo wakati wa semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein. (Picha zote na Ikulu)
Mshauri wa Rais Uchumi Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa alipokuwa akielezea dhamira nzima ya semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumikwa wajumbe wa Semina hiyo na kuwatambulisha Watoa mada katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja leo ambapo Mwenyekiti wa Semina hiyo akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akifungua semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini,ufunguzi huo ulifanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kuwashirikisha Viongzi wa ngazi za juu wa serikali ya Mapinduzi  wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu,Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wengine.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (kulia) akifungua semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini,ufunguzi huo ulifanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kuwashirikisha Viongzi wa ngazi za juu wa serikali ya Mapinduzi  wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na Watendaji wengine.
Baadhi ya Mawaziri na Manaibu Waziri na watendaji wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifuatilia kwa makini wakati zilipokuwa zikitolewa mada katika semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein. 
 Mtaalam kutoka Malaysia Dk. Idris Jala Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuupia Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa utafutaji ufumbuzi wa matatizo kwa njia za vikao vya wataalam mbali mbali wa(maabara) ya Malaysia (PEMANDU) akitoa mada katika semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayoshuhulikia utafiti katika ufumbuzi wa matekeo makubwa na ya haraka Bw. Omari Issa kutoka Tanzania Bara wakati alipokuwa akitoa mada yake wakati wa semina ya siku moja kuhusu matokeo makubwa na ya haraka katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuleta maendeleo nchini iliyofanyika leo katika ukumbi wa Ikulu Mjini Unguja na kufunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein (katikati)akiwa Mwenyekiti wa Semina hiyo.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha uchumi wake unazidi kuimarika ikiwa ni pamoja na kutafuta mbinu bora na matokeo yenye ustawi katika mageuzi ya kiuchumi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa mkutano uliojadili juu ya matokeo stawi katika kukuza uchumi, uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuwashirikisha viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakiwemo Mawaziri, Manaibu Waziri pamoja na Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na watendaji wengine wa Serikali.
Makamo wa Kwaza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd nao walishiriki ambapo ujumbe wa Wataalamu kutoka Malaysia na Tanzania Bara walitoa mada mbalim mbali na baadae ziliweza kujadiliwa na viongozi hao walioshiriki katika mkutano huo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha ustawi na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi yanafanyika hapa nchini hatua ambayo imeanza kuonesha matumaini na kuleta mwanga katika ukuaji wa uchumi huo.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa wataalamu kutoka Malaysia akiwemo Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia, ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Utafutaji ufumbuzi wa matatizo kwa njia za vikao vya wataalamu mbali mbali (Maabara) ya Malaysia ( PEMANDU) Dk. Idris Jala ambaye ni miongoni mwa watoa mada katika mkutano huo.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazithamini na kutoa pongezi kwa mtaalamu huyo pamoja na ujumbe wake kutoka nchini Malaysia kwa kuja Zanzibar na kutoa mafunzo hayo sambamba na kuweza kubadilishana uzoefu juu ya matokeo ustawi na mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na utekelezaji wake.
“Tumevutiwa na juhudi zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Malaysia katika programu zake za matokea makubwa na ya haraka katika kukuza uchumi wake.. aidha,  napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Dk. Idris Jala kwa matokeo na mwelekeo mzuri wa kitengo anachokiongoza cha PEMANDU ”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein  alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazipongeza hatua inazozichukua Malaysia katika kuisaidia Zanzibar kwa kuipa nafasi za masomo nchini humo katika kada mbali mbali zikiwemo programu za kiuchumi.

Alieleza kuwa nafasi hizo za mafunzo inazozipata Zanzibar ni muhimu na zimekuwa zikisaidia katika kufikia lengo ililojiwekea katika utekelezaji wa masuala ya kiuchumi na kukuza maendeleo.

Dk. Shein alisema kuwa mnamo mwaka 2014 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitayarisha mbinu za  kupata matokea ya ustawi na ya haraka katika suala zima la kukuza uchumi wake.

Alieleza kuwa lengo kubwa la utekelezaji wa ustawi huo ni kuimarisha programu kuu za maendeleo katika sekta zilizopewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Dira ya 2020, Malengo ya Milenia pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar, Awamu ya Pili (MKUZA II).

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa ni bahati ya pekee kupata timu ya wataalamu kutoka nchini Malaysia kuja Zanzibar kwa lengo la kukaa pamoja na kutoa elimu juu ya hatua za kiuchumi zilizoipa mafanikio nchi hiyo  pamoja na kubadilishana uzoefu na wataalamu na viongozi wa hapa nchini.

“Ninaimani kubwa kwamba elimu tutakayoipata katika mkutano wetu huu wa leo itatupa mwelekeo mzuri katika azma yetu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini mwetu...Zanzibar imo katika kujifunza kutoka Tanzania Bara njia zilizotumika katika kufanikisha upatikanaji wa matokeo makubwa ya haraka ya kiuchumi‘Big Fast Result’ambapo imeanza kuona matokeo yake”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mambo matatu makubwa yakiwa na malengo yake yalipitishwa katika vikao vya pamoja vya wataalamu vya utafutaji wa ufumbuzi wa matatizo mbali mbali (Maabara) hapa Zanzibar hapo mwaka jana ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa utafutaji wa rasilimali, uimarishwaji wa mazingira ya biashara na utalii.
Dk. Shein alisisitiza kuwa maazimio hayo yamepitishwa katika Bajeti ya mwaka 2014-2015 ambapo utekelezaji wake ulianza Julai mwaka jana ambapo ni miezi sita tu tokea kuanza utekelezaji huo.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa matarajio yaliopo ni kuhakikisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mbinu za kuendesha vikao hivyo wa wataalamu (Maabara) utekelezaji wake unaipeleka Zanzibar kutoka uchumi wa chini na kuelekea uchumi wa kati.
Dk. Shein alisema,“Lengo la juhudi hizo ni kuhakikisha Zanzibar inabadilika kuanzia hivi sasa kutoka katika uchumi wa chini na kuelekea katika uchumi wa kati mnamo mwaka 2020”.

Alisema kuwa hii inatoa matumaini kutokana na hivi sasa uchumi wa Zanzibar kuimarika kwa kasi kwa kiwango cha asilimia 7.4 kwa hesabu za mwaka 2013 ambapo hali inaonesha kuwa hata mwishoni mwa mwaka 2015 asilimia inaweza kufikia 7.8 ambayo ukuaji wake ni mkubwa  kwa nchi za Afrika Mashariki sambamba na nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara.
Alisisitiza kuwa elimu itakayopatikana katika mkutano huo kati ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wataalamu kutoka nchini Malaysia utatoa mwelekeo na mbinu mpya katika utekelezaji wa matokeo makubwa kwa njia za haraka katika kukuza uchumi.

Nae Dk. Idris Jala alieleza mbinu na mikakati iliyowekwa na Malaysia katika kuhakikisha wanafikia lengo lao la ‘matokeo makubwa kwa njia za haraka’ walizojiwekea katika kuimarisha uchumi wao sambamba na changamoto zilizojitokeza.

Alisema kuwa hatua hiyo imeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa Malaysia huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya kutosha kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Aidha alizitaja baadi ya nchi zilizopanua wigo ikiwemo Afrika Kusini, India, Tanzania, Korea na nyenginezo huku akisisitiza kuwepo mafanikio iwapo hapatakuwa na urasimu hatua mabayo itatokomeza suala zima la rushwa.

Mapema Mshauri wa Rais Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alieleza azma ya mkutano huo wa siku moja pamoja na kutumia fursa ya kutoa wasfu wa wataalamu hao kutoka Malaysia na Tanzania.
Akifunga kikao hicho Dk. Shein amewahakikishia wataalamu hao kuwa azma hiyo itafikiwa kwa mashirikiano ya pamoja na kueleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa dira katika kufikia malengo yaliowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza na kuimarisha uchumi wake.

No comments:

Post a Comment