TANGAZO


Friday, January 16, 2015

Rais Dk. Shein aongoza maziko ya Mwasisi wa CCM, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Makame Suleiman

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (wa tatu kulia) akijumuika na Waislamu na Viongozi katika Kumswalia aliyekuwa Mwenyekiti wa Wazee wa CCM Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman katika Msikiti wa Ijumaa  Mgenihaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja Marehemu alifariki jana Nyumbani kwake Amani Mjini Unguja.
 Wananchi na Waislamu wakilibeba Jeneeza la Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman aliyekuwa Mwenyekitiwa Wazee wa CCM na kuzikwa lao kijijini kwako Mgenihaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (katika) akijumuika na Waislamu na Viongozi katika Maziko ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Wazee wa CCM Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman aliyezikwa leo kijijini kwao  Mgenihaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein  akitia udongo katika kaburi la aliyekuwa Mwenyekiti wa Wazee wa CCM Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman aliyezikwa leo kijijini kwao  Mgenihaji Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. (Picha zote na Ikulu)

Na Ikulu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Zanzibar.

Mazishi ya Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman yalifanyika Mgenihaji, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuali Ali Vuai, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Mawaziri, Wawakilishi na viongozi wengine wa serikali, vyama vya siasa pamoja na viongozi wa dini na wananchi.

Mapema Alhaj Dk. Shein alishiriki katika sala  ya kumsalia Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman iliyofanyika huko katika Msikiti Mkuu wa Mgenihaji.

Akisoma wasifu wa Marehemu, Katibu wa CCM, Wilaya ya Kati, Bwana Ali Yussuf alisema kuwa Marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman kifo chake kimetokea usiku wa tarehe 16 Januari, 2015 nyumbani kwake Amani, mjini Unguja.
Alieleza kuwa Marehemu Makame Mzee Suleiman alizaliwa tarehe 14 Aprili, 1926, katika kijiji cha Mitakawani, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini, Unguja na kupata Elimu ya Msingi katika Skuli ya Uzini mwaka 1936.

Aidha, alijiendeleza na masomo ya Qur-an katika kijiji hicho cha Mitakawani ambapo mnamo mwaka 1945, marehemu alijiendeleza na elimu ya Sekondari.

Marehemu Mzee Makame Mzee, alijiunga na Chama Cha Afro Shirazi Party (ASP) mwaka 1957 na ni miongoni mwa Waasisi wa Chama cha Mapinduzi kilichozaliwa mwaka 1977,akiwa katika Tawi la Mitakawani.

Katika uhai wake, marehemu aliwahi kushika nyazifa mbali mbali ndani ya Chama na Serikali. Kwa upande wa Chama na kutokana na uhodari, uwezo na weledi mkubwa wa masuala ya kisiasa, Chama Cha ASP kilimteua kushika nafasi za uongozi zikiwemo Mwenyekiti wa ASP Tawi la Mitakawani mnamom mwaka 1957-1977.

Mwaka 1961-1977 aliteuliwa kuwa Katibu wa ASP wa Wilaya ya Kati pamoja na kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa ASP Taifa. Pia, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Wilaya, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM wa Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa upande wa Serikali, marehemu alibahatika kushika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Katibu wa Baraza la Mapinduzi mnamom mwaka 1964-1972, Mkuu wa Wilaya ya Kati, Unguja mnamo mwaka 1972-1974, Mkuu wa Wialaya ya ChakeChake, Pemba mnamo mwaka 1974-1978 pamoja na kuwa Mshauri wa Rais wa Mambo ya siasa mwaka 1978.
Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika uongozi na Utumishi wa Umma, mwaka 2014, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, alimtunuku marehemu Nishani ya Miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Kati alieleza kuwa Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu na kuwaomba wawe na moyo wa subra katika wakati huu mgumu wa maombolezi ya Mzee Makame Mzee Suleiman. Aidha, alieleza kuwa kifo cha marehemu kimeacha pengo kubwa kwa Taifa.

Hadi kufariki kwake, marehemu Mzee Makame Mzee Suleiman  alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar.
Marehemu ameacha vizuka wawili na watoto ishirini (20). Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.

No comments:

Post a Comment