Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiagana na Balozi Mdogo wa China Mhe. Xie Yunliang baada ya kumalizika kwa ghafla ya uzindizi wa mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule ya sekondari ya kiembe Samaki mjini Zanzibar leo Januari 06,2015, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kilele chake tarehe 12 Januari 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Balozi Mdogo wa China Mhe. Xie Yunliang kwa pamoja wakikata utepe kuzindua rasmi mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule ya sekondari ya kiembe Samaki mjini Zanzibar leo Januari 06,2015, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kilele chake ni tarehe 12 Januari 2014.
Wazee na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiembe Samaki Zanzibar wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, alipokua akihutubia kwenye uzinduzi na mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule ya sekondari ya kiembe Samaki mjini Zanzibar leo Januari 06,2015, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kilele chake ni tarehe 12 Januari 2014.
Wazee na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiembe Samaki Zanzibar wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, alipokua akihutubia kwenye uzinduzi na mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule ya sekondari ya kiembe Samaki mjini Zanzibar leo Januari 06,2015, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kilele chake ni tarehe 12 Januari 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal akihutubia kwenye uzinduzi cha mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule ya sekondari ya kiembe Samaki mjini Zanzibar leo Januari 06,2015 ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kilele chake ni tarehe 12 Januari 2014.
HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE UZINDUZI WA MRADI WA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO KATIKA SKULI YA SEKONDARI YA
KIEMBE SAMAKI NA JAMII ILIYOIZUNGUKA, ZANZIBAR TAREHE 6 JANUARI 2014
Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Waziri;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Mjini/Magharibi, Unguja;
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge;
Mheshimiwa Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China, Zanzibar;
Ndugu Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Serikali;
Viongozi wa Kampuni ya ZTE Corporation ya China;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Ndugu Walimu na Wanafunzi;
Ndugu Wanahabari;
Mabibi na Mabwana;
Assalam Aleikum!
Awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana hapa Kiembe Samaki kushiriki katika tukio hili muhimu la kusherehekea kutimiza miaka 51 tangu kufanyika Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964. Pili natoa shukrani zangu za dhati kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa kunialika na kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mradi wa Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Skuli ya Sekondari ya Kiembe Samaki na Jamii iliyoko katika maeneo ya karibu na skulihii. Nimefurahishwa sana kunialika tena kuja hapa Skuli ya Kiembe Samaki, kwani mwaka jana wakati wa sherehe za kutimiza Miaka 50 ya Mapinduzi yetu,mulinialika kuifungua skuli hii tarehe 10 Januari 2014 na leo nimefika tena kwa kuzindua mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Skuli hii na Jamii. Ahsante sana kwa ukarimu wenu.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Serikali zetu mbili ziliahidi kuchukua hatua thabiti ya kuandaa mazingira ya kusambaza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini. Katika hatua hizo, Serikali ziliahidi kujenga mkongo wa Taifa wa mawasiliano. Mikongo hiyo yote hivi sasa imeshajengwa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na matunda yake ndio haya tunayoyashuhudia hapa Skuli ya Sekondari ya Kiembe Samaki. Uzinduzi huu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika elimu ni mojawapo ya utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali zetu wakati wa Uchaguzi Mkuu. Hivi sasa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa ajili ya kufundishia imerahisika sana kutokana na mkongo wa mawasiliano wa Zanzibar kufika katika maeneo mengi ya visiwa vyetu.
Ndugu Wananchi,
Ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano umekuwa wa mafanikio na msaada mkubwa katika kuharakisha, kuboresha na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi na kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa letu. Kwa mfano, wananchi walio wengi sasa wanapata huduma mbalimbali za mtandao kwa kutuma na kupokea pesa; kulipia ankara za maji, umeme na tozo mbalimbali kama vile ada na leseni; na mawasiliano ya simu na intaneti pamoja na elimu mtandao na tiba mtandao. Hivyo natoa wito kwa wananchi kuitumia huduma hii kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nimeambiwa kuwa msaada wa vifaa mbali mbali vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na kuunganishwa kwa kompyuta na mkongo wa Taifa wa mawasilaino ni msaada uliotolewa na kampuni ya China ya ZTE. Kwa niaba ya Serikali zetu mbili, napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na uongozi wa kampuni ya ZTE kwa msaada walioutoa kwa ajili ya Skuli hii na Jamii iliyoizunguka. Msaada wao tunauthamini na tutautunza kwani ni kielelezo cha wazi cha uhusiano na ushirikiano wa kidugu wa muda mrefu ulioanza tangu mwaka 1964 baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Serikali inatambua na inathamini sana mchango unaotolewa na sekta binafsi katika maendeleo ya jamii. Pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo, lakini Serikali pekee yake haiwezi kufanya kila kitu. Serikali imejenga Skuli ya Sekondari ya Kisasa hapa Kiembe Samaki. Hivyo haina budi kuungwa mkono na wadau wengine wa maendeleo wakiwemo sekta binafsi kuleta huduma nyingine muhimu kama vile ilivyofanya kampuni ya ZTEkuiunganishia skuli hii mkongo wa Taifa wa mawasiliano kwa matumizi ya kompyuta. Hivyo, napenda nitoe wito kwa kampuni zingine binafsi, kujitokeza kuchangia maendeleo ya jamii . Ninawahakikishieni kuwa Serikali zetu zitawaunga mkono wale wote wenye nia ya dhati ya kuleta mapinduzi katika elimu.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi,
Dunia imepita katika mapinduzi makubwa ya Sayansi na Teknolojia. Mapinduzi hayo ya Sayansi na Teknolojia yamechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa kasi kwa uchumi wa mataifa ambayo yameweza kujenga uwezo mkubwa katika matumizi ya Teknojia ya Habari na Mawasiliano. Nchi yetu nayo imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na imesaidia sana katika juhudi zetu za kuimarisha elimu yetu na harakati za kupunguza umasikini wa wananchi wetu. Kasi ya mawasiliano baina ya watu wa mataifa mbali mbali imerahisisha shughuli za kibiashara kwa watu wa mataifa mbali mbali. Tanzania itapiga hatua katika sekta ya elimu na kuongeza uelewa miongoni mwa wanafunzi iwapo matumizi ya teknolojia ya simu na kompyuta katika kufundishia yatazingatiwa kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu.
Hivyo ili tuweze kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, hatuna budi kujenga miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli zetu kama ni nyenzo muhimu ya kusomea na kujifunzia lakini pia kama ni sehemu nyengine ya kuwaandaa wanafunzi kwa ajira zinazozalishwa na sekta hii. Matumizi ya teknolojia yatasaidia kuboresha mfumo wa ufundishaji na kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa wabunifu na kuepuka tabia ya kukariri masomo, hivyo kuongeza uelewa wao na kuwafanya walimu kubaki kama wawezeshaji.
Napenda kutoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar kuongeza juhudi katika ufundishaji wa somo la Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli zetu. Pia,nitoe wito kwa walimu wetu, kujifunza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwani itawasaidia sana katika ufundishaji wa masomo mbalimbali. Aidha, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli,itasadia sana wanafunzi wetu kujifunza masomo ya Sayansi na Teknolojia ambayo hivi sasa yanaonekana magumu au yana uhaba wa walimu.
Ndugu Wanafunzi;
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya juhudi kubwa katika kuongeza upatikanaji wa elimu katika ngazi zote. Huduma za elimu zimeenea maeneo yote ya mjini na mashambani na inatolewa bila ya ubaguzi wowote. Serikali imejenga skuli 19 za aina hii katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Saba. Hii ni hatua kubwa sana ya maendeleo ya kupigiwa mfano. Katika kuenzi juhudi za Serikali, wanafunzi hamna budi kusoma kwa bidii ili malengo ya kuzalisha wataalamu wetu wenyewe yaweze kufikiwa. Skuli hii nzuri na mpya pamoja na vifaa vyake havina budi kutunzwa na kutumiwa ipasavyo ili mafanikio yaliotarajiwa yaweze kupatikana.
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kwa mara nyengine napenda kutoa shukrani zangu kwa Kampuni ya ZTE ya China kwa msaada wao. Pia naishukuru Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kunialika kushiriki katika uzinduzi wa mradi huu muhimu. Baada ya kusema hayo,kwa heshima kubwa na taadhima, sasa niko tayarikuzindua Mradi huu wa Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika skuli ya Sekondari ya Kiembe Samaki na Jamii ya eneo hili.
IMETOLEWA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS.
No comments:
Post a Comment