Ofisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga akiangalia Cheti cha usajili wa Kikundi cha Wapakaya kinafanya kazi ya kutengeneza Pikipiki kilichopo Wilaya ya Mpwapwa walipowatembelea wanakikundi kwa ajili ya kukagua mradi wa wanakikundi hao. Kushoto ni Afisa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Mpwapwa Bw. Paschal Jeremiah.
Ofisa Maendeleo ya
Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga
akishika jiko banifu linalotengenezwa kwa kutumia udongo mfinyanzi kuangalia
ubora wa jiko hilo lililotengenezwa na wanakikundi cha Kujiamini kilichopo
Wilaya ya Kongwa wakati wa kukagua miradi ya Vijana wa Wilaya ya Kongwa Mkoa wa
Dodoma. (Picha
zote na: Genofeva Matemu – Maelezo)
Na Genofeva Matemu –
Maelezo (Mpwapwa, Dodoma)
Tarehe 18/01/2015
VIJANA kutoka Wilaya ya
Mpwapwa na Kongwa mkoani Dodoma, wameshauriwa kutokimbilia mikopo inayotolewa
kwa vijana kabla ya kujipanga na kuwa na malengo ya matumizi ya mikopo hiyo kwa
maendeleo ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa na
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Bw. Christopher Ryoba Kangoye wakati wa ziara ya maafisa kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo walipomtembelea ofisini kwake na baadae kukutana
na vijana wa wilaya hizo jana Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
“Vijana wamekua na
tabia ya kukimbilia mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali za serikali na
zisizo za serikali kabla ya kujipanga hivyo kushindwa kutumia fedha hizo kwa
uangalifu na hatimaye kushindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati”, alisema Bw.
Kangoye.
Aidha Bw. Kangoye
amesema kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa hivyo wanapaswa kujitambua na
kutumia nguvu hizo zitakazozalisha matunda mazuri kwani ili mtu aweze kuendelea
lazima afanye kazi kwa bidii na kwa ufanisi.
Akizungumza kwa niaba
ya maafisa kutoka Wizarani waliofika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mwezeshaji
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa amesema
kuwa Wizara inayosimamia masuala ya Vijana imepanga mikakati mingi ya kuwainua
vijana wa taifa hili hivyo kuiomba Wilaya ya Mpwapwa kushirikiana na Wizara
inayosimamia vijana kuwaongoza vijana wa Wilaya yao kuwa lulu ya taifa
itakayomulika vijana wengine kutoka Wilaya zote nchini Tanzania.
Kwa upande wake Afisa
Maendeleo ya Vijana kutoka Wilaya ya Mpwapwa Bw. Paschal Jeremiah amesema kuwa
vikundi vya vijana kutoka Wilaya ya Mpwapwa vilipatiwa mkopo wa shilingi
milioni 10 mnamo mwaka 2009 na urejeshaji wa mkopo huo umefanyika kwa asilimia
90 hali inayoonyesha kuwa vijana wa Wilaya yake wako makini na wanastahili
kupatiwa mkopo mwingine kuendeleza shughuli walizozianzisha.
Naye kijana Briton Ivan
Majele kutoka kikundi cha Umoja wa Vijana Ng’ambo kilichopo Wilaya ya Mpwapwa
kinachofanya kazi ya kufyatua matofali amewataka vijana wenzake nchini
kutobweteka bali wathubutu na kuamini kuwa mtaji mdogo unaposimamiwa vizuri
huzaa na kuwa mkubwa hivyo kuthamini kile kidogo walichonacho na kukiendeleza.
No comments:
Post a Comment