Mwezeshaji kutoka
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa kulia akifafanua
jambo walipotembelea mradi wa kikundi cha vijana cha Miranaco wanaomiliki duka
la madawa muhimu katika Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Mbeya. Kushoto ni Afisa Utamaduni
Wilaya ya Mbozi Bw. Godfrey Msokwa, wapili kushoto ni Mkuu wa Kituo cha Vijana
Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele na wapili kulia ni Mwenyekiti wa kikundi cha
Miranaco Bw. John Maige.
.
Na Genofeva Matemu –
Maelezo, Mbeya
Tarehe 22/01/2015
HALMASHAURI ya Wilaya
ya Mbozi imeshauriwa kupeleka vijana wa wilaya hiyo katika Vituo vya Vijana
kupata mafunzo mbalimbali ili kuweza kupata mbinu mbadala za kiujasiriamali.
Rai hiyo imetolewa na
Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Bw. Laurean Masele wakati wa semina ya
Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana hivi
karibuni katika Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Mbeya.
Bw. Masele amesema kuwa
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inasimamia Kituo cha Vijana
Sasanda Mbeya kinachotoa mafunzo ya ujasiriamali katika fani za Kilimo na
Ufugaji, Kituo cha Vijana cha Ilonga Morogoro kinachotoa mafunzo katika fani ya
teknolojia ya habari na mawasiliano na Kituo cha Vijana cha Marangu Moshi
kinachotoa mafunzo ya uthubutu/ujasiri kwa vijana.
Aidha Bw. Masele
amesema kuwa moto uliowashwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kuhamasisha vijana mbinu za kiujasiriamali unalenga kuwajengea vijana ujasiri
wa kuthubutu na kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumza wakati wa
kufungua semina hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi
Bw. Elisey Ngowi amewataka vijana kuzingatia elimu inayotolewa na kuifanyia kazi
kwani vijana bado wanauwezo mkubwa wa kufikiri hivyo kutumia akili nyingi na
nguvu nyingi kufanya mambo mbalimbali kwa maendeleo ya Wilaya hiyo.
Kwa upande wake kijana
Yohana Chaula kutoka kikundi cha Bodoboda B. Mloo Wilaya ya Mbozi amesema kuwa
kundi la vijana wasiokua na ajira kwa sasa linazidi kuongezeka hivyo kuiomba
Wizara inayosimamia masuala ya Vijana kuongeza fungu katika Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana ili vijana wote nchini waweze kunufaika na Mfuko huo.
Naye mwakakikundi wa
kikundi cha Umoja wa Vijana Wilaya ya Mbozi Bw. Chemli Ndema ameushukuru ujumbe
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kufika Wilaya ya Mbozi na
kutoa elimu ya ujuzi kwa vijana kwani elimu aliyoipata katika semina hiyo
imemtoa katika giza nene na kukiri kuwa atakuwa chachu ya maendeleo na kiongozi
bora katika jamii.
No comments:
Post a Comment