TANGAZO


Tuesday, January 20, 2015

Elimu kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana yawafikia Vijana wa Mbeya Vijijini

Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini Bibi Upendo Sanga akifungu semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo jana katika Mkoa wa Mbeya. Waliokaa katikati ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa na kulia ni Afisa Vijana kutoka Wizara hiyo Bi. Amina Sanga. 
Afisa Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga akiwaelimisha vijana wa Wilaya ya Mbeya Vijijini kuhusu mwongozo unaosimamia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyofanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri hiyo Mkoa wa Mbeya. 
Afisa Ushirika wa Wilaya ya Mbeya Vijijini Bw. Isaya Mwamarobo akifafanua jambo wakati wa semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana iliyotolewa kwa vijana wa wilaya hiyo jana katika Mkoa wa Mbeya. 
Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoa wa Mbeya walioudhuria semina ya Ujasiriamali, Stadi za Maisha, Ujuzi na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa semina hiyo. 
Afisa Maendeleo ya Vijana  kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga wapili kulia akizungumza na wanakikundi wa Wasamba Saccoss Wilaya ya Mbeya Vijijini walipowatembelea kukagua mradi wanaouendesha. Wakwanza kulia ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele na watano kulia ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari,  Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa. 
Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Amina Sanga watatu kulia akizungumza na wanakikundi cha Njelenje Bee Keeping kinachojishughulisha na ufugaji nyuki kilichopo kijiji cha Njelenje Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendeshwa na vijana Wilayani humo. Kulia ni Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa na wapili kulia ni Mkuu wa Kituo cha Vijana Sasanda Mbeya Bw. Laurean Masele. (Picha zote na Genofeva Matemu – Maelezo)


Na Genofeva Matemu – Maelezo, Mbeya
Tarehe 20/01/2015
VIJANA wa Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Mbeya Vijijini wametakiwa kutokuwa na tafsiri hasi kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuwa ni takrima inayotolewa na serikali kwa vijana hivyo kuchezea fedha hizo na kushindwa kurejesha mkopo watakaouomba kupitia mfuko huo.

Hayo yamesemwa na Mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bibi Ester Riwa wakati wa semina iliyotolewa kwa Vijana wa Mbeya Vijijini kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Stadi za Maisha, Ujuzi na Ujasiriamali jana Mkoani Mbeya.

Bibi Riwa amesema kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unahudumia vijana wote nchini bila kuangalia itikadi za kisiasa ukiwa na lengo la kuwakomboa vijana na kuinua vipaji vya vijana nchi nzima.

“Vijana ni taifa la leo na kesho likiwezeshwa taifa zima limewezeshwa, Wizara yenye dhamana na Vijana inalenga kuwafikia vijana wote nchini bila kuangalia itikadi za kisiasa kwani vijana wote ni wetu na tunatamani kuona vijana wanajiendeleza kufikia ndoto walizonazo” amesema Bibi Riwa.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini Bibi Upendo Sanga amesema kuwa ni bahati ya pekee kutembelewa na ugeni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivyo kuwaomba vijana wa Wilaya yake kuzingatia elimu watakayoipata na kusambaza elimu hiyo kwa vijana wengine wa Wilaya yake ambao hawakuweza kufika katika semina hiyo.

Bibi Sanga ameiomba Wizara yenye dhamana na Vijana kuendeleza programu ya kuwaelimisha vijana mara kwa mara na kuwahamasisha vijana kujiunga katika vikundi kwani ni raisi kusaidia vijana wakiwa katika vikundi kuliko kumsaidia kijana mmojammoja.

Akichangia wakati wa semina hiyo kijana Evans Bembeja kutoka Shirika la Efao linalojishughulisha na kilimo cha mbogamboga amesema kuwa vijana wengi hawaangalii mbele wamekua kwenye mwamko wa kisiasa wakiamini kuwa siasa ndio sehemu ya kupata pesa za haraka hivyo kuachana na fursa nyingine kama vile kilimo na ufugaji.

No comments:

Post a Comment