Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Hawa Ghasia akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam uliolenga kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa Serikali uliofanyika jana kote nchini.
Baadhi ya
waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Waziri wa nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.Hawa
Ghasia (hayupo pichani) na vyombo vya habari uliofanyika leo jijini Dar es
salam ukilenga kueleza hatua zitakazochukuliwa na Serikali kwa wale wote
waliosababisha kasoro mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika jana kote nchini. (Picha zote na Maelezo)
Na Frank
Mvungi- Maelezo
Serikali
imesema uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliofanyika jana Kote Nchini umefanikiwa kwa Zaidi ya asilimia 98% katika Mikoa
yote.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia wakati wa mkutano na
waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam uliolenga kutoa ufafanuzi kuhuzi
mafanikio ya uchaguzi huo.
Akifafanua
Mh. Ghasia amesema kwa kiwango kikubwa wananchi walijitokeza kupiga kura na
kuchagua viongozi wao katika ngazi ya Mitaa,Vijiji, na Vitongoji.
Akizungumzia
mafanikio ya Uchaguzi huo Mh. Ghasia
alitaja Mikoa ambayo uchaguzi umefanyika katika Halmashauri na Kata zote kuwa
ni Arusha, Mbeya, Kagera, Njombe, Singida, Lindi, Ruvuma, Katavi na Geita.
Mikoa Mingine
iliyofanya vizuri katika uchaguzi huo ni Iringa,Dodoma,Mtawara ambapo Mh. Ghasia
aliwapongeza Viongozi na wataendaji wote wa Mikoa na Halmashauri hizo pamoja na
wananchi kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya hadi kufanikisha uchaguzi huo.
Akitoa
ufafanuzi Zaidi kuhusu maboresho yaliyofanywa na Serikali katika uchaguzi huo
Mh. Ghasia amesema kuwa mojawapo ni kuwepo kwa utaratibu wa kupiga kura kwa
kutumia karatasi maalum zilizochapishwa kitu ambacho katika uchaguzi uliopita
hakikuwepo.
Akizungumzia
Mikoa ambayo baadhi ya Halmashauri zimeahirisha uchaguzi ama Halmashauri yote
au sehemu ya Kata zake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kufika kwa vifaa
vya kupigia kura Mh.Ghasia aliitaja kuwa ni Kilimanjaro katika Halmashauri ya
Wilaya ya Rombo na Hai,Manyara katika Halmashauri za Hanang na mbulu.
Mikoa
Mingine ni Morogoro katika Halmashuri ya Wilaya ya Ulanga na Mvomero,Mkoa wa
Shinyanga Halmashauri ya Wilaya ya Msalala,Mkoa wa Simiyu Halmashauri ya Wilaya
ya Busega na Itilima ambapo Mikoa mingine ambayo kasoro ndogondogo zilijitokeza
na kupelekea uchaguzi kuahirishwa katika baadhi ya Kata ni
Kigoma,Mwanza,Tabora,Tanga,Mara,Rukwa,Pwani na Dar es Salaam.
Akizungumzia
Hatua zitakazochukuliwa na Serikali kufuatia dosari zilizojitokeza katika
baadhi ya maeneo Mh. Ghasia amesema Mikoa yote imetakiwa awasilishe taarifa
rasmi na kamilifu kuhusu yaliyojitokeza katika Halmashauri zao ambapo Wizara
yake itachambua taarifa hizo ili kubaini chanzo cha kasoro zilizojitokeza ili
hatua stahiki zichukuliwe.
Kuhusu
Halmashuri ambazo hazikufanya uchaguzi kutokana na kasoro mbalimbali Mh. Ghasia
amesema kwa mujibu wa Kanuni zinatakiwa kurudia
uchaguzi huo ndani ya siku saba kama kanuni za uchaguzi huo
zinavyoelekeza.
Naye Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bw.
Jumanne Sagini alitoa wito kwa vyombo vya habari kuweka uzalendo mbele katika
kuripoti habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kusaidia Taifa kukamilisha
mchakato huo muhimu.
Akifafanua
Sagini amesema ni vyema vyombo vya Habari vikaonyesha mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika uchaguzi huo pamoja na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza.
Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa katika ngazi ya Mitaa,Vijiji, na Vitongoji ulifanyika tarehe
14/12/2014 kote nchini ambapo taarifa za awali zimeonyesha kuwa zoezi la kupiga
kura lilienda vizuri katika Mikoa Mingi.
No comments:
Post a Comment